Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kumwezesha kuchangia hotuba hii. Elimu ni ufunguo wa maisha na Taifa. Ikiwa wananchi wake hawana elimu, basi Taifa hilo haliwezi kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu amesema, anayejua hawi sawa na yule asiyejua. Ni lazima anayejua ana upeo mkubwa wa kuona mbali. Kuhusu Walimu, wana kazi kubwa sana na wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapata changamoto nyingi katika mazingira ya kazi, kwanza kufundisha wanafunzi wengi katika Idara moja, upungufu wa vifaa vya kufundishia, ukosefu wa matundu ya vyoo, maji hawana, nyumba za kuishi hawana, usafiri hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetangazwa kwamba elimu ni bure, wakati bado miundombinu ni mibovu. Kwanza tuiboreshe. Naishauri Serikali kwamba bajeti ya Wizara hii iongezwe ili iweze kuboresha miundombinu, madarasa yaongezwe ili kupunguza msongamano wa wanafunzi, vyoo, madawati, nyumba za Walimu na mishahara ya Walimu pia iboreshwe ili waweze kutoa hiyo elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, ikiwa mti huutunzi, hauna mbolea wala maji, utawezaje kutangaza tenda ya matunda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapofika muda wao wa kustaafu, wanapata usumbufu mkubwa kupewa mafao yao. Wastaafu hao hudai mafao yao mpaka wanafariki hawapati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwatizame wastaafu hawa kwa jicho la huruma, pale tu wanapostaafu wapewe haki zao mapema ili wapate kuwasaidia katika maisha ya uzeeni na pia wapatiwe bima ya afya angalau waweze kuhudumiwa, kupata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kuwa mila potofu ya watoto wa kike kuchezwa unyago ni moja ya kichocheo kikubwa kupata mimba za utotoni, kwa sababu mtoto akishachezwa unyago, hujiona yuko huru na tayari amekamilika na kuingia katika daraja la ukubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipige marufuku kwa mtoto wa kike kuchezwa ikiwa bado ni mwanafunzi ili kupunguza tatizo hili. Vilevile sisi viongozi, wazazi, walezi tukemee kwa kupiga vita jambo hilo ili kumpa nafasi mtoto wa kike aendelee na masomo yake. Baadaye akimaliza kusoma atachezwa kama ndiyo mila zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Zanzibar, elimu ya juu bado kuna usumbufu mkubwa kuhusu mikopo ya wanafunzi. Wanacheleweshwa sana na hivyo kuchelewa kuanza kusoma. Tunaomba Serikali ya Muungano iweze kusimamia ili usumbufu uweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia, naomba kuwasilisha. Wako mjenzi wa Taifa.