Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti yetu hii. Kwanza kabisa niungane na Waheshimiwa Wabunge wote waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara hii ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya hasa katika kutatua changamoto zinazohusu makundi mbalimbali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo lakini na makundi ya wakulima kwa kutoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa ni kero kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na suala la muda, napenda nijielekeze hasa katika mambo mawili; kwanza nijikite katika idara yangu ya vyuo vikuu lakini baadaye nitajikita kwenye bajeti kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa wetu Rais mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kushughulikia masuala ya chuo kikuu hasa katika utoaji wa mikopo ambao mwaka hadi mwaka bajeti yake inazidi kupanda. Kwa mfano, mwaka jana takribani wanafunzi 123,000 walipata mikopo na bajeti hii ya 2019/2020 takribani wanafunzi 128,000 wataendelea kupata mikopo takribani bilioni 450, tunapongeza sana Serikali yetu kwa juhudi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kwa nia njema kabisa mikopo hii inalenga katika kuhakikisha makundi yote ya watoto wa Tanzania wakiwemo wakulima, wafanyakazi lakini hasa wale wa kipato cha chini wanaweza kushiriki katika kutengeneza wataalam mbalimbali katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu moja kwa Mheshimiwa Waziri, mikopo hii pamoja na uzuri wake lakini kuna changamoto ambazo zimejitokeza hasa ukiangalia sasa jinsi ilivyoboreshwa kweli mwanzo watu walisuasua lakini baadaye wakatafuta namna ya ulipaji wa mkopo. Mkopo huu unatakiwa mwanafunzi anapomaliza chuo alipe baada ya miezi 24 lakini alipe kwa asilimia 15 lakini pamoja na hiyo kuna hiki kipengele cha Value Retention Fund. Sasa kwa kufuata vigezo hivi, inafanya huu mkopo sasa badala ya kumsaidia huyu mtoto wa maskini imekuwa sasa ni mzigo mkubwa sana hasa kwa sababu ya hii Value Retention Fund.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kijana ambaye amemaliza chuo kikuu mwaka 2015, kama utatoa hii miezi 24 maana yake unahesabu 2016 na 2017, yupo kwenye grace period, ina maana unahesabu 2018 na hii 2019 kidogo. Kijana huyu juzi wakati anakwenda kuangalia anadaiwa shilingi ngapi, kwa sababu ya hii Value Retention Fund; huyu kijana alikopeshwa milioni 10 lakini alivyokwenda kucheki juzi amekuta anadaiwa milioni 16.5. Sasa je huu mkopo kweli nia yake ile njema imetolewa sasa imekuwa kama ni business ambayo kwa kweli itaathiri kwa kiasi kikubwa sekta hii ya chuo kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili suala kuweza kurekebisha kama vile tulivyofanya ile quick appraisal kwenye tozo ya kodi ya pedi. Kwa hiyo, hivi nayo sasa wafanye evaluation kwamba huu ulipaji kwa kweli utamsaidia mtoto wa mtanzania au vipi. Kwa hiyo, hilo ni ombi langu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na asilimia 15 naomba tena nirudie bado ni kubwa mno. Hii sasa implication yake itakuwa kwamba wanafunzi sasa wameshaanza kuambizana burden ya huu mkopo, matokeo yake itafika mahali wakati ule Pride, Finca walitoza kodi kubwa sasa hivi zimepotea baada ya watu kutafuta vyanzo vingine. Kwa hiyo, tunaweza tukakosa hata wanafunzi wa kuchukua mikopo au kozi zile ambazo zinahitaji kusomewa muda mrefu hasa za sayansi, zitaathirika vibaya wanafunzi hawataenda kusoma kule kwa sababu ya huu mzigo ambao umeongezwa na hii Value Retention Fund. Kwa hiyo, naomba sana tuangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja hayo, ninaomba niseme kwamba hawa vijana alipe asilimia 15, mkopo ambao haumaliziki mpaka anazeeka, inaweza pia hata kichocheo kwa upande wa ufisadi na rushwa ambayo Mheshimiwa Rais wetu kila siku anapambana na ufisadi na rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, ninaomba kwamba Serikali itoe zile fedha ambazo zimeahidi katika kujenga hosteli. Juzi tumepoteza binti yetu wa kike ambaye alivamiwa na majambazi wakati anakwenda. Kwa hiyo, hosteli zikijengwa ndani ya chuo, zikawa na ulinzi mkuu, itasaidia sana kuepusha madhara kama haya tuliyoyapata hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niingie sasa kwenye suala la sera mbalimbali katika nchi yetu katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Wengi tumeangalia suala la sera ya huduma bure, sasa huduma bure katika jamii kwa mfano naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuwa sikivu kwa kuweza kuwasaida wanyonge katika kupata huduma mbalimbali. Kwa mfano, tayari tuna Sera ya Huduma Bure kwenye elimu bure, watoto, wajawazito na wazee wanatibiwa bure lakini hata kwa magonjwa ya kansa bure. Kwa hiyo, Serikali imejaribu kupunguza mzigo mkubwa kwa wazazi ili waweze kupeleka watoto wao shule. Pia kuna mpango mzuri wa TASAF ambao unasaidia watu maskini waweze kuwasaidia hasa kwa upande wa mtoto wa kike.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, sasa hivi kuna hii debate inayoendelea kuhusu taulo za kike. Ni wazo zuri sana lakini tuangalie je uwezo wa uchumi wetu, hivi tutaweza kweli kila kitu bure, tayari Serikali jamani imeshatoa mpango wa TASAF. Sasa TASAF package mojawapo ni kumsaidia hata huyu mtoto wa kike kupata taulo. Hata hivyo, tuangalie je, kigezo cha kwamba mtoto anapokuwa kwenye mzunguko wake ule wa mwezi, je, tukitoa hii taulo bure tayari inaweza ika-solve problem?

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, nafikiri kipaumbele tungewekeza kwenye vyoo na maji. Huyu mtoto anaweza akapata taulo lakini kama shule haina choo, hawezi kwenda shule lakini shule kama hakuna maji hawezi pamoja na kwamba ana taulo atabaki nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu, tukiangalia ukisoma kweli kuna nchi zimeweza ku-implement haya masuala ya taulo lakini wameangalia the needy people siyo the whole population watoto wa kike wote kama ilivyokuwa elimu bure hata mtu mwenye uwezo basi umlipie. Tuangalie ni familia zipi kweli hazijiwezi lakini tayari kuna mpango wa TASAF ambao umeshasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tujielekeze sasa kwenye masuala yale ya msingi, tuelekeze suala letu la vyoo, maji na afya kwa sababu huyu mtoto anaweza akawa kwenye mzunguko wa mwezi lakini anaumwa tumbo, atahitaji apate panadol na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tujielekeze kwenye masuala ya kimaendeleo, tuache hivi vitu bure bure kwa sababu ukiangalia sana, dunia ya leo kuna watu watapitia kwenye mgongo wa demokrasia, usawa wa jinsia na harakati za binadamu kutengeneza maslahi yao binafsi. Uchumi wa nchi yetu bado ni wa chini hatujafikia hata uchumi wa kati, hatuwezi kila siku tunatoa kitu burebure, je, nafasi ya mzazi naye katika kuchangia familia yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sababu zinazofanya Afrika ziwe maskini mojawapo ni uvivu pamoja na poor policies. Poor policies maana yake siyo kwamba ni policy mbaya lakini una-implement sera ambayo siyo wakati muafaka kwa wakati huo. It’s not a bad policy lakini it’s a poor policy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sasa hivi unasema kila kitu bure, Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi kila siku mnasema bajeti haitimii, hakuna bajeti hata siku moja ikafika asilimia 100, leo unataka uongezee tena Serikali eti ikatoe tena pedi bure kwa watoto wa kike, fedha zitatoka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwa Serikali katika kusaidia mpango wa TASAF, katika kusaidia elimu bure, mzazi naye aendelee kuchangia katika kumlea huyu mtoto ili sasa tujielekeze kwenye mipango hii ya maendeleo. Mwanamke anahitaji maji na afya ili tuweze kutekeleza mipango hii ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme ukweli pamoja na nia nje, lakini hatujafikia bado wakati muafaka wa kufanya kila kitu burebure, hii sasa ni kuingizana mkenge ili kesho na keshokutwa waje tena watugeuzie kibao ooh mlipanga hivi; nasema hizi zote ni political pressures.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Uganda waliibeba hii ajenda ya pedi bure, ukiangalia Kenya, South Africa kwa nini zote zitokee kwa wakati mmoja; tunajua strategies hizi za watu. Wanajua sasa hivi tuna wataalam, tutawekeza, tutafanya maendeleo wanaturudisha nyuma, wewe kila kitu utoe bure ile hela haizalishi maana yake nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo niliamua nijikite hapo, nashukuru sana kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)