Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye mapendekezo ya bajeti ya 2019/ 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mpango pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na wataalam wote kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema ukweli, bajeti hii iliyosomwa safari hii, mimi nimefanya utafiti huko nje, nimeongea na watu na wasomi na kila mmoja, bajeti hii wameipenda vizuri sana. Wanasema hawajawahi kuona bajeti nzuri kama ya safari hii, Mheshimiwa Waziri songa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa kazi nzuri mnayoifanya, bajeti hii wameipenda, imegusa kila mmoja, wanasema ni bajeti nzuri mbayo hawajawahi kuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kuipongeza Serikali kwa kufanya uhakiki na kulipa madeni ya wazabuni pamoja na watoa huduma, mmefanya kazi nzuri, bado mnahakiki. Licha ya hivyo naomba kukwambia kuwa kuna baadhi ya vyuo ambavyo ni vya kilimo, baadhi ya shule za sekondari kwenye Mkoa wangu wa Morogoro ambao bado hawajalipwa kama MATI Ilonga kuna na sekondari ya Morogoro kuna wanaodai. Naomba waifanyie kazi na ninavyosema hivi, bila shaka kuna na mikoa mingine kuna wazabuni na wakandarasi ambao hawajalipwa naomba waendelee kuhakiki Serikali iweze kuwalipa kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuongelea mambo ya vipaumbele kwenye bajeti hii na nianze kwa viwanda pamoja na kilimo. Ili viwanda viweze kuendelea lazima tuangalie kilimo, kilimo ndiyo kinacholeta malighafi kwenye viwanda na ninaposema kilimo hapa namaanisha kilimo mazao, uvuvi na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo asilimia 65.5 ya wananchi wanategemea kilimo na hasa huko vijijini na asilimia ya chakula asilimia 70 ni wanawake wanaozalisha chakula hiki. Kwa hiyo, naomba tunavyoongelea kilimo tuwape kipaumbele wanawake na hasa kuangalia kwenye upande wa mikopo na kuangalia jinsi watakavyoendeleza kilimo hiki. Hakuna kilimo/chakula bila ya kumuangalia mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ila kuna changamoto kidogo kwenye upande wa kilimo, bado tunatumia kilimo cha jembe sana sana ingawa naipongeza Serikali kwa upande wa matrekta yameongezeka, lakini unakuta bado tuna matatizo tunatumia kilimo cha mvua, bado ni kilimo cha mvua kinashamiri. Kwa hiyo nilikuwa naiangalia na kuiomba Serikali yangu iangalie kilimo cha umwagiliaji. Tukifanya kilimo cha umwagiliaji, tutaweza kusonga mbele na tutaweza kupata malighafi ya kutosha kwenye mazao yote ambayo tunalima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jambo lingine kubwa sana kwenye matatizo ya kilimo ni mbegu. Mbegu hapa nchini tunazalisha asilimia 21 tu, mbegu nyingine zinatoka nje, tatizo ni nini? Tatizo ni ASA ambao ndiyo wanadhibiti na wazalisha mbegu, ASA hawana bajeti ya kutosha. Mheshimiwa Waziri naomba ASA wapate bajeti hiyo waliyoomba fedha ziweze kupitishwa zote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzalisha hizo mbegu, wanaodhibiti hizo mbegu ni TOSCI, TOSCI na wenyewe hawana fedha, naomba na wenyewe waweze kupewa fedha za kutosha kusudi tuweze kupata mbegu za kutosha. Huko ni kwa upande wa mazao hasa nafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye mbogamboga (horticulture) pamoja na matunda ni asilimia moja tu ya mbegu tunazalisha hapa nchini na sanasana ni vitunguu. Kwa hiyo, naomba sana kwa sababu mbegu nyingi zinatoka nje, je, tatizo ni nini? Naomba sana na yenyewe ni ASA hawana fedha za kutosha, naomba muwapatie fedha za kutosha, huo ndiyo ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni mbolea; tunategemea mbolea kutoka nje. Tuna kiwanda kimoja cha Minjingu, Minjingu nayo haipendwi sana hapa nchini, kwa nini, ni baadhi ya wachache wanaipenda. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali yangu na hapa wanaohusika watuambie Kiwanda cha Mbolea cha Lindi ni lini kitaanza kuzalisha mbolea? Kwa sababu tukipata mbolea yetu, naamini tutaweza kulima na kuzalisha vizuri sana kwa sababu mbolea pamoja na mbegu bora tutaweza kupata mazao bora ambayo yanaweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hii programu ya SAGGOT pamoja na ASDP, Serikali wamepanga mkakati mzuri kwenye upande wa kilimo, naomba hela zote zilizopangwa kwenye mkakati huo ziweze kutoka na zikitoka tutaweza kupata mazao ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, masoko yanaenda pamoja na mazao na viwanda. Nashukuru kuona viwanda vimeanza kujengwa, kuna viwanda vya korosho vipo, naipongeza Serikali wanajitahidi kwenye kuangalia na kuangalia wakulima wa korosho wawasaidiaje, siyo kusema wamewaachia wanawasaidia kadri wanavyoweza na najua kila kitu kitakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazao ya mikunde tumeweza kupata kiwanda hata Morogoro tuna kiwanda kimejengwa ambapo tutaweza kununua mbaazi, karanga na maharage. Kwa hiyo, hata matatizo yaliyokuwepo kwa upande wa mbaazi yatakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema kilimo inakwenda na miundombinu/barabara; kuna barabara za mashambani, barabara za mashambani zingine zimesahaulika, naomba sana ziangaliwe. Kuna barabara za uchumi; nikisema barabara za uchumi kwa upande wa Morogoro kuna barabara ya kutoka Kidatu – Lupilo – Malinyi – Songea, Namtumbo. Tumetengewa hela kidogo, naomba Mheshimiwa Waziri hela hizo zilizotoka ziweze kutolewa na zenyewe ni za ukarabati. Hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, iweze kujengwa kwa lami kwa hiyo ndiyo hivyo uchumi utaendelea na kwa sababu inaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Ruvuma pamoja na Mkoa wa Morogoro iweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa upande wa mifugo, mifugo tuweze kufuga mifugo ya tija. Kwa upande wa mifugo waangalie sana kuhusu malisho. Naomba bajeti yote iliyopangwa kwenye malisho iweze kutoka pamoja na matumizi bora ya ardhi. Tulisema kuwa ardhi iweze kupimwa, ikipimwa hakutakuwepo matatizo yoyote na wafugaji wataweza kufuga vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi; uvuvi wa bahari kuu bado hatujautendea haki. Naomba sana Serikali yetu iangalie uvuvi wa bahari kuu, maziwa, mito na uvuvi ambao tunasema ni wa mabwawa. Ili tupate samaki wengi, lazima wananchi wahamasishwe kufuga kwenye mabwawa na hii itasadia hasa na kwenye utapiamlo kwenye mambo ya lishe. Fedha zote zilizotengwa kwenye mambo ya lishe ziweze kutolewa na ziweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukuaji wa uchumi kwa maendeleo; naomba kuongelea kuhusu Stiegler’s Gorge. Stiegler’s Gorge tunaifurahia sana na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuiona hii na kuiendeleza na tunaamini haturudi nyuma, tunasonga mbele pamoja na umeme huu wa Stiegler’s Gorge na ninaamini tutapata umeme mwingi na tutaweza kuzalisha kwenye viwanda vyetu na tunaweza kufanya mambo mengine kuhusu huu umeme. Pamoja na hii Stiegler’s Gorge kuna mambo ya umwagiliaji pamoja na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miradi yote iliyolala iweze kukamilika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. Ahsanteni sana, nashukuru. (Makofi)