Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi niweze kuchangia bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie fursa hii kwanza kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Kivuli kwa jinsi ambavyo ameandaa bajeti vizuri, lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Chama Taifa, Kamanda wa anga ambaye kwa kweli ni kiongozi imara anayesababisha tufanyekazi vizuri na Watanzania waweze kutuamini na chama hiki kinaaminika kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nimekaa hapa nasikiliza michango mbalimbali ya wenzetu watu wa CCM na nilikuwa namsikia pia Mheshimiwa Amina Mollel hapa anazungumza kuhusiana na ukusanyaji wa mapato, anasema kwamba tungepeleka jeshi yaani mpaka leo Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Wabunge wake hawaelewi kwamba masuala ya fedha ni taaluma yaani wanaona jeshi pake yake tu kutumia nguvu, ndiyo kitu pekee ambacho kinaweza kikakusanya mapato katika Taifa hili yaani hapo ndipo milipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nilikuwa nataka kuzungumzia jambo lingine; watu wengi wanasema sisi tunakataa Stiegler’s Gorge, tunakataa standard gauge huu ni mtazamo wa hovyo kabisa. Sisi hata siku moja hatujakataa standard gauge, sisi hata siku moja hatujakataa Stiegler’s Gorge, tulichokuwa tunasema sisi hapa tulikuwa tunatoa ushauri kutokana na matumizi makubwa ambayo yanakwenda kwenye miradi mikubwa miwili badala ya kuwahudumia Watanzania walio wengi, hicho ndicho ambacho tulikuwa tunajaribu kukizungumzia na siku zote tunaposema kwamba Serikali hii inakwenda kufanya shughuli za vitu, inaweka bajeti ya vitu badala ya bajeti inayowahusu wananchi tulikuwa tunamaanisha. Tunajaribu kuangalia ni namna gani bajeti zingine ambazo zimepewa fedha kidogo na hata hizo fedha kidogo ambazo zinakwenda kule hazipelekwi kabisa au zinapelekwa kidogo sana na ndiyo maana tunasema kwamba ni lazima mfike mahali mkubali. Tatizo kubwa CCM mnachokifikiri ni kwamba vyote tunavyoviongea kama uoinzani ndani ya Bunge hili mnaona kama sisi tunapinga kila kitu na kwa sababu ya kiburi mlichonacho ndani ya mioyo yenu hamuwezi kutekeleza ule ushauri ambao tunawapa, mnaendelea kubeza, lakini kesho mnarudi mnaanza kufanya hayo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Rais juzi amewaita wafanyabiashara Dar es Salaam, tuliyoyazungumza mwaka 2016/2017 amekwenda kuyazungumza Mheshimiwa Rais hayo hayo na amefanya mabadiliko. Leo Mheshimiwa Mpango tulichozungumza kwamba mnaleta sheria ambazo ni kero kwa wafanyabiashara zitakazosababisha wafanyabiashara wasifanye biashara mkasema hapana hizi ndiyo sheria nzuri, leo Mheshimiwa Mpango karibu kodi 54 anakwenda kuziondoa. Sasa yote tuliyazungumza yaani mpaka muue biashara mpaka mhakikishe kwamba biashara zinakwenda vibaya ndiyo mrudi nyuma muanze kufikiri kwamba sasa tumekosea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaona sisi ni macho ambayo yanaona kila siku tunafanyakazi ya kuchanbua ni namna gani mambo yanavyokwenda…

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: …tofauti na ninyi mnakoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi…

MBUNGE FULANI: Tulieni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Frank Mwakajoka kuna taarifa. Mhehsimiwa Amina Mollel

T A A R I F A

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.

Naomba nimpe taarifa mchangiaji anayezungumza kwamba anaposema waliishauri Serikali na hatimae leo hii ndiyo yanachukuliwa, naomba tu nimkumbushe kwamba katika Bunge lililopita waliishauri sana Serikali kuhusiana na masuala ya madini na hatimae Serikali ikaonesha usikivu na ikaleta sheria hizo, lakini wale wale waliokuwa wanashauri hatimae ndiyo hao hao waliokuja kupinga sheria hiyo. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Frank Mwakajoka unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya ambayo anayafanya Mheshimiwa Mbunge aliyekuwa anatoa taarifa yaani hii inaonesha ni jinsi gani ambavyo mnandelea kuwa dhaifu sisi kazi yetu ni kushauri na kama hamsikii mtaendelea kufanya hivyo na hamtaweza kupiga hatua na hamtaweza kufanya chochote kwa sababu hamuwezi mkasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Bunge la mwaka 2017/2018 tulizungumzia hapa, ilikuja taarifa hapa kwamba tunataka sasa fedha zote za Taasisi za Serikali ziondoke kwenye benki za kibiashara ziweze kwenda BOT. Jambo hili tulilishauri sana na tukasema yaani sababu ni nini? Sababu waliyoitoa wakasema kwamba mabenki yanapata sana faida, lakini tukashangaa sana kwamba kazi ya benki za biashara katika nchi hii kazi yake zinaisaidia Serikali kuwakopesha wajasiriamali wadogo wadogo na wafanyabiashara wakubwa kuhakikishawkamba wanafanya biashara na wanapata mitaji. Sasa mkapeleka hizo fedha BOT na sasa hivi hizo fedha zimekaa kule na BOT haikopeshi wajasriamali na benki imeshindwa kukopesha wafanya biashara wadogo wadogo na wajasiriamali kwa hiyo mambo hayaendi. Yote haya najua baada ya mwaka huu mtakuja kesho kutwa mtaiondoa na kwasababu ndiyo kawaida yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nia yangu kubwa nilikuwa nataka kuzungumzia sana kwenye kilimo; lengo kubwa la Serikali wanasema ni Serikali ya wanyonge na imekuja kuondoa umaskini kwa wanyonge, lakini nataka kuuliza wanyonge ni watu wa namna gani? Unapozungumzia wakulima, wafugaji na wavuvi unazungumzia asilimia 65 mpaka 75 ya Watanzania wote. Kundi hili la Watanzania ambalo ni kubwa kabisa leo limesahaulika kabisa katika bajeti ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi hasa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikukumbushe; mwaka 2016/2017 tulitenga fedha, tulipitisha fedha hapa shilingi bilioni 101; kati ya shilingi bilioni 101 fedha iliyokwenda kufanyakazi ya maendeleo kwenye kilimo ilipelekwa shilingi bilioni mbili peke yake, lakini mwaka 2017/2018 tulitenga fedha hapa shilingi bilioni 150 fedha iliyokwenda kufanyakazi ya kilimo ilipelekwa shilingi bilioni 16 peke yake, lakini mwaka jana tumetenga pia fedha imekwenda kupelekwa karibuni shilingi bilioni 46 peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo nashangaa na nasema kwamba jambo hili halihitaji hata kuwa profesa wala halihitaji kuwa daktari. Nazungumza hivi kwa sababu Watanzania asilimia 65 mpaka 75 tafsiri yake ni kwamba ndiyo wanunuzi wakubwa katika Taifa hili na ndiyo walipa kodi wakubwa. Ukitaka kujua kwa nini biashara zime- stuck katika mwaka 2018/2019 ni kwa sababu wakulima na wafanyabiashara wa mazao walishindwa kuuza mazao yao baada ya kukosa soko na ndiyo maana biashara zote zilisimama. Kwa hiyo, unapozungumzia biashara lazima uzungumzie kundi la watu asilimia 75 la wakulima, wafugaji na wavuvi. Usipozungumzia kundi hili ujue kabisa wanunuzi hawatakuwepo katika nchi hii kwa sababu wakikosa kipato hata wafanyabiashara wa maduka wanaofanya biashara za viwandani hawataweza kuuza kwa sababu watu wanaotegemewa sana ni wakulima, wafugaji na wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie mchango wa sekta ya kilimo katika nchi hii ni mkubwa sana. Ukienda kuangalia kwenye suala la ajira karibuni asilimia 65 ya Watanzania wote wanajiajiri katika kilimo, ufugaji na uvuvi, lakini ukienda kwenye chakula karibuni asilimia 100 tunapata chakula kutokana na hao wakulima ambao ni wananchi waliojiajiri kwenye kilimo. Lakini ukienda pia kwenye pato la Taifa inachangia karibu asilimia 28 mpaka 30 lakini bado uwekezaji kwenye kilimo kwenye Serikali ya Awamu ya Tano iko chini ya asilimia mbili, sasa tusitegemee viwanda kwa sababu asilimia 65 ya malighafi ya viwandani yanategemea kilimo na kama yanategemea mazao ya kilimo tafsiri yake ni kwamba kama hatutawekeza kwenye kilimo tusitegemee kupata viwanda katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mnasema kwamba hii ni Serikali ya viwanda halafu hamuwekezi kwenye viwanda mnapeleka kwenda kununua ndege, mnakwenda kujenga Stiegler’s Gorge, mnakwenda kujenga standard gauge na manatumbia kwamba hii ni Serikali ya viwanda, hivyo viwanda vitakuja kwa namna gani? Kwa hiyo ni lazima tuhakikishe kwamba tunainua kilimo na ninataka kutoa mfano, kwamba Serikali hii kwa kweli imeshindwa kabisa kuhakikisha wkamba inawasaidia Watanzania wanyonge ambao ni wakulima, wafugaji na wavuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2004/2005 katika bajeti ya kipindi hicho yaani uwekezaji ulikuwa ni asilimia 4.7 ya bajeti yote; mwaka 2005/2006 ilikuwa aislimia 5.8 ya bajeti yote; mwaka 2006/2007 ilikuwa aislimia 5.8 na pia mwaka 2009/2010 ilikuwa asilimia 8.6 na walitenga fedha karibu shilingi bilioni 666.9; leo mnatenga shilingi bilioni 208 miaka mingapi imepita mnatenga shilingi bilioni 208 mnasema mnakwenda kuinua kilimo na mtapata viwanda katika Taifa hili, mnajidanganya. Ni lazima tufanye mageuzi ya kilimo kwanza ndiyo tutakwenda kwenye viwanda na kama mnaota viwanda wakati hamjafanya mageuzi ya kilimo mnajidanganya na Serikali yenu itakuwa ni Serikali ambayo inazungumza uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi utaona kabisa walikuwa wamekubalina kwamba ni lazima wawekeze kwenye kilimo, watainua kilimo kwa asilimia nane ndani ya miaka mitano, lakini leo kilimo hakijainuka na kilimo hapa kimekua kwa asilimia 5.3 peke yake. Sasa kwa hiyo mmewadanganya wananchi ambao mlikwenda kuuza Ilani yenu iili mchaguliwe na mwongoze Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye Ilani yenu katika kifungu cha 27(n) mlisema kwamba mtanunua meli tano za uvuvi ili kuhakikisha kwamba mnawainua wavuvi lakini pia mnahakikisha kwamba kinachangia pato la Taifa kwenye upande wa uvuvi. Lakini nakwambia mpaka sasa hakuna meli hata moja wala boti iliyonunuliwa kwenye bahari ya Hindi kwa ajili ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ilikuwa ni kwamba mnatengeneza na kwenda kuuza sera zenu kwa wananchi lakini hazitekelezeki. Kwa hiyo, sisi tunasema kwamba tunawakumbusha Watanzania waelewe kwamba yanayozungumzwa kwenye majukwaa, yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi hayatekelezeki.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu ukweli Watanzania sio watu wajinga, leo wakulima wako kijijini wanalima kule, wanakosa masoko na hata wakipata masoko wanatafuta masoko yao tunakwenda kuzuia mipaka mnasema wasiondoke. Juzi Salum Sumri kule Sumbawanga aliamua kuacha mabasi akasema ngoja ajikite kwenye kilimo akagharamia vitu vingi sana kwa ajili ya kilimo, lakini cha kushangaza baada ya kugharamia haya amekwenda kulima amepata karibuni tani 47,000 lakini ameshindwa kuuza hayo mahindi yake yako ndani mpaka sasa hivi alipata soko Congo mkazuia mkasema asiende kuuza mkasema mtakula mahindi yote haya mnakulaje mahindi tani 40 na ngapi wakati fedha hamna za kununulia mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naona...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)