Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kwa kupata nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Serikali.

Kwanza nianze kwa kumpongeza kaka yangu Dkt. Mpango pamoja na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote wa wizara hii. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti naona ni namna gani taarifa hii ya Mheshimiwa Waziri ilivyozingatia maoni mbalimbali ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti. Mheshimiwa Waziri hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie hali halisi ya reli ya kati; sote tunafahamu kwamba reli ya kati ni reli ambayo inasaidia sana wafayabiashara wanaopeleka mizigo Congo, Burundi na Zambia. Lakini leo hii kuna tatizo kubwa la upungufu wa mabehewa kwenye Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja wameonesha kwamba wanajipanga kununua mabehewa mapya na wanajipanga kununua vichwa vya treni.

Mimi naomba tu niiishauri Serikali hebu tuharakishe haraka kununua mabehewa, kwa nini nasema hivi; juzi tu hapa mimi ni mdau katika kufanya biashara kidogo tumelipa shilingi 54,195,000 kwa ajili ya mabehewa 13 kusafirisha tani 520 kwenda Kalemi. Kwa bahati mbaya tunaambiwa kwamba mmelipa hizi pesa, lakini mabehewa mtayapata baada ya miezi mitatu au miezi sita. Sasa wafanyabiashara wanashindwa kuendelea kufanya biashara na Wakongo kwa sababu unachukua tender kwa Wakongo, unawaahidi kwamba ndani ya wiki tatu au mwezi utakuwa umewafikishia mizigo yao Kigoma ili waweze kupakia kwenye meli kupeleka Kalemi au kupeleka Burundi matokeo yake wenzetu wa TRL hawana mabehewa ya kutosha kwa ajili ya kubeba mizigo.

Kwa hiyo, mimi niliomba nijikite kwenye hili ili Mheshimiwa Waziri kwa sababu mmeonesha kwenye bajeti ya Wizara ya Miundombinu kwamba wana bajeti yao ya kununua mabehewa mapya na vichwa mimi naomba pesa ile ipelekwe ili waweze kununua mabehewa mapya, wafanyabiashara waweze kubeba mizigo kupeleka Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili reli inakwenda na bandari. Mheshimiwa Waziri unafahamu kwamba Bandari ya Kigoma mnaendelea kidogo kidogo kuiboresha. Tunaomba kasi ile ya kuboresha iongezeke zaidi, lakini huku tukiboresha bandari nimeona katika mpango na katika bajeti ya mwaka 2019/2020 mmeonesha kwamba kuna ununuzi wa meli mpya kwa ajili ya mizigo kwenye Ziwa Tanganyika, lakini kuna ununuzi wa meli mpya kwa ajili ya abiria. Mimi niombe Mheshimiwa Waziri utusaidie meli hiyo iweze kununuliwa kwenye mwaka wa fedha ujao kama ambavyo mlivyopanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie SGR; nimeona kwenye Kamati ya Bajeti hapa ule mtandao wa ujenzi wa SGR kwa maana ya kutoka Dar es Salaam mpaka Isaka; Isaka - Mwanza halafu ndio iende Tabora - Kigoma; Kigoma - Kalema, na hatimaye Uvinza huko Songati mpaka Kigali. Mimi niiombe Serikali natambua kwa sasa hivi tumejipanga ku-concentrate na huu mtandao wa kutoka Dar es Salaam mpaka Isaka; Isaka - Mwanza lakini wakati tunakwenda Mwanza tuangalie nah ii route ya kwenda Tabora; Tabora - Kigoma tukifanya hivyo tutawezesha sasa kupokea mizigo inayokwenda Kongo lakini pia mizigo inayotoka Kongo inayoingia Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa nilizonazo Rais Mstaafu Kabila wa DRC ameshasimamia kule Kalemi bandari imekamilika, wamekamilisha na meli kubwa ya kubeba mizigo na target yao ni nini? Target yao ni kuchukua yale madini ya kolta kuyatoa Kalemi na kuyaleta Dar es Salaam na tayari wameona kwamba Mheshimiwa Rais wetu ameanzisha masoko ya madini kitu ambacho Wakongomani kimewafurahisha sana. Sasa wanajipanga kuwa wanatoa dhahabu, wanatoa yale madini ya kolta kutoka kule kuyaleta Dar es Salaam. Sasa tukuombe Mheshimiwa Waziri hivi katika huu mtandao wa SGR tuweke mkazo na kutoka Isaka - Tabora - Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili nizungumzie kiwanja cha ndege cha Kigoma. Hivi karibuni tulimpokea Spika wa Bunge la Burundi pamoja na Wabunge walisafiri kutoka Burundi kwa magari mpaka Kigoma, wakapanda ndege pale mpaka Dar es Salaam, Dar es Salaam ndio wakapanda tena ndege kuja Dodoma, lakini wanachosikitika wao ni kwamba hakuna yaani ile airport pale ikiboreshwa wao wanaweza wakawa wanasafiri kwenda nje ya nchi kwa kutumia kiwanja kile kile ili mradi tu connection ziweze kuimarishwa vizuri. Sasa kile kiwanja cha Kigoma tulishawalipa fidia wananchi, wananchi hawadai tena fidia.

Sasa najiuliza swali kigugumizi ni nini katika kuendeleza kile kiwanja cha Kigoma? Tukiendeleze kiwanja cha Kigoma ili tuwe na route ya kwenda Kalemi tuwe sasa hivi tuna route ya kwenda Bujumbura tunataka sasa tuwe na route ya kwenda Kalemi, tuwe na route ya kwenda Lubumbashi, tufungue mipaka zaidi ya kibiashara, wafanyabiashara kutoka nchi hizi jirani waweze kuingia Kigoma wafanye biashara zao na hatimaye warudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo sasa nizungumzie masuala ya jimboni kwangu. Tunafahamu kwamba vyanzo vingi vya Halmashauri vimechukuliwa na Serikali kuu na sasa hivi hali ya Halmashauri zetu Wakurugenzi wanashindwa kuwalipa Waheshimiwa Madiwani hata posho za vikao. Sasa nilifikiri katika hii Finance Bill labda vile vyanzo tulivyovichukua vya Halmashauri ilikuwa sasa ni wakati muafaka kuvirejesha kwenye Halmashauri zetu. Kwa nini nasema hivyo; tuone kwenye makusanyo ya majengo, kodi ya majengo tulimuuliza DG wa TRA kwamba ninyi target yenu mlikuwa ni kukusanya kiasi gani wanasema ilikuwa ni kukusanya Halmashauri zote 180; lakini mmekusanya kiasi gani? Tumekusanya kwenye Halmashauri 30 tu.

Sasa unajiuliza tuna Halmashauri 180 TRA wameweza kukusanya Halmashauri 30 peke yake; kwa nini hivi vyanzo sasa kama vimeshindikana Serikali Kuu tusivirudishe kule halmashauri ili Wakurugenzi waendelee kusimamia. Nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hali za Halmashauri zetu ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie miradi ya maendeleo. Tunayo miradi ya maji, imekuwa ni hadithi. Tuna miraji ya maji ambayo inashindwa kukamilika zaidi ya miaka 15 tangu awamu ya Mheshimiwa Mkapa, awamu ya Mheshimiwa Jakaya na sasa tuko awamu ya Mheshimiwa Magufuli tunayo miradi ya maji ambayo haikamiliki. Mfano peke yake mimi jimboni kwangu nina mradi mkubwa kule Rukoma na mradi mkubwa pale Kandaga...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hasna sekunde 30 malizia sentensi muda wako umeisha.

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru niombe tu Serikali labda tufunge macho, tujaribu kumaliza miradi yote ile ya maji iliyokuwa huko nyuma halafu ndio tuendelee na miradi mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naomba kuunga mkono na nampongeza sana kaka yangu Mpango. (Makofi)