Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti asubuhi ya leo na mimi nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutupa nafasi ya kujadili bajeti ya nchi yetu katika mwaka wa fedha huu tunaoanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naungana na waliotangulia kuipongeza Wizara kwa ujumla wake na Serikali kwa juhudi ambazo wameendelea kuzifanya katika kusaidia uchumi wa Taifa letu. Lakini nianze kwa maneno machache ya wachangiaji wa asubuhi wanasema Serikali yetu, Rais wetu amekosa washauri wazuri ndiyo maana uchumi wetu hauendi vizuri na maneno mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi kwamba katika muda wa miaka karibu miwili Bunge hili limekuwa likiishauri Serikali mambo mengi ya msingi na Serikali imeyasikia na imeyafanyia kazi. Serikali hii ina wataalamu na washauri wazuri ndiyo maana leo tunajivunia gawio la Airtel kwa historia ya nchi yetu na kupata hisa hiyo ambayo Serikali imepata. Hao ndiyo washauri, Rais hafanyi kazi peke yake Serikali hii ndiyo ushauri wao ndiyo umesababisha sasa hivi Serikali inapokea gawio katika mashirika ya Serikali ambayo yalikuwa yakijiendesha kwa hasara. Kwa nini tusitambue michango ya watumishi wetu wanaosaidia nchi.

Mheshimiwa Spika, Rais kazi yake ni kusimamia, lakini wako watumishi wetu wanaofanyakazi kumshauri Rais na mambo mengi yamefanyika kwa kipindi hiki ndiyo maana tunajenga reli ndiyo maana tumefufua Shirika la Ndege ambalo limekufa kwa zaidi ya miaka 20. Ukisema hakuna washauri wazuri nadhani hatuitendei haki nchi yetu ndiyo maana hata kodi ambazo tulikuwa tumezilalamikia zimefutwa na Serikali hii kwasababu ya ushauri wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baya zaidi wako wanaohoji kwa nini Rais amekutana na watumishi sijui watu gani wafanyabiashara, Rais huyu ni Rais wa Watanzania wanyonge wa Taifa hili, anayo haki na wajibu wa kufanya alichokifanya na wote tumpongeze ni historia katika nchi Rais kuja kuongea na watu wachache na wa chini kabisa huyu Rais ni wa mfano ndiyo maana yeye anachojali ni watu wake, amepigiwa kura kama Wabunge hapa lazima akutane na wapiga kura wake wakati wote tumpongeze Rais ambaye ameona Ikulu ni sehemu ya Watanzania na siyo sehemu yake peke yake, halafu watu mnakuja hapa mnahoji eti kwa nini Rais amekutana na wafanyabiashara, huyu ni Rais wa mfano, ni Rais wa wanyonge, ni Rais anayeonesha kwa vitendo kwamba anajali maslahi ya Watanzania bila kujali hadhi yao ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii lazima tujifunze kujifunza kwake ni Wabunge wangapi wanakutana hata na wapiga kura wakitongoji, Rais huyu amekutana na wafanyabiashara wa kila Wilaya historia hiyo, amekutana na Makatibu Tarafa historia hiyo na wafanyabiashara wa madini historia hiyo ndiyo Rais tunayemtafsiri kama Rais wa wanyonge wa Taifa hili tumpongeze, tumtie moyo na anafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba niseme maeneo machache kushauri katika bajeti tunazungumza habari katika kitabu cha Waziri ukurasa wa 31; Waziri anasema hivi; katika kuendeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda katika mwaka 2019/2020 Serikali itajikita kuvutia uwekezaji zaidi kwenye viwanda vilivyotumia malighafi zinazopatikana nchini kama vile mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini.

Mheshimiwa Spika, nataka nimuulize Waziri kiasi gani mmetenga? Kwa sababu kuzungumza ni jambo moja na lakini kuwekeza katika maeneo hayo ni jambo lingine na Mheshimiwa Waziri lazima tujifunze kwamba Serikali haiwezi kuwapa wananchi mmoja mmoja fedha kwa ajili ya kujenga kilimo, kwa ajili ya kuwekeza katika mifugo, lakini lazima Serikali itengeneze miundombinu na mazingira wezeshi ili Watanzania wanaoweza kuwekeza wawekeze katika maeneo hayo. Ni kweli mnazungumza maneno ya kuwezesha kilimo lakini kiasi gani ambayo Serikali imetenga kwa ajili ya mazingira wezeshi katika sekta ya kilimo, katika mazao yale ya kibiashara ikiwepo pamba na mazao mengine kama chai, kahawa na mengine kama hayo, kama hatuwekezi katika maeneo hayo hatuwezi kwenda.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nishauri Serikali katika eneo hili, moja ya tatizo kubwa linaloikabili sekta ya kilimo kwenye nchi yetu ni mambo makubwa matatu; moja upatikanaji wa mvua ya uhakika ambayo imekuwa shida, tunataka Serikali na Wizara ituambie tunafanya nini kuhakikisha kwamba maji tunayapoteza ukiwa unaenda Dar es Salaam wakati wa masika haipitiki barabara yetu kwa sababu ya mvua na maji mengi, Serikali ingefanya mchakato wa kukusanya yale maji ili kujenga bonde hilo ikawa ni zone ya umwagiliaji na tukawa na kilimo chenye tija kwa ajili ya maslahi ya Watanzania kuliko kupoteza haya maji bure mengi ambayo kwa kweli wakati mwingine yanatuletea maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine upatikanaji wa pembejeo kwenye nchi yetu imekuwa donda sugu. Naomba Serikali na hili katika hili Bunge tukubaliane tunataka Serikali wakati wa majumuisho mtuambie mnafanya nini kuhakikisha pembejeo za hakika zinapatikana kwa wakulima. Kila mwaka tunaletewa pembejeo fake lakini Serikali haiwachukulii hatua wale wanaotusababishia pembejeo hizo na Serikali imeondoa ruzuku katika pembejeo tunapata wapi pembejeo ili wakulima walime kwa haki na kwa ustawi wa Taifa hili. Serikali haiwezi kulima lakini itutengenezee mazingira rafiki ili tuweze kulima kwa tija, wakulima hawajui wanapata wapi pembejeo, Serikali mnafahamu nini mikakati ya kwenu kuhakikisha kwamba pembejeo tunazipata kwa gharama zetu wenyewe wakulima siyo kwa gharama zenu, lakini hatuzipati. Kila mwaka mnasema mnawashughulikia waliotuletea fake halafu mwaka huo nani anatufidia sisi wakulima kwamba tumepata hasara na Serikali hiyo ambayo wako kule chini wanaosimamia hizo pembejeo kwanini hawachukuliwi hatua.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho mimi naomba kwa niaba ya wafugaji wa nchi hii tumeona tozo nyingi mmefuta tunawapongeza sana, lakini tozo mlizofuta ni za wafanyabiashara wa viwandani, sisi wafugaji wa chini tunatozo mnayotutoza kila ng’ombe shilingi 30,000 tunavyopeleka ng’ombe Kenya au kutoa nje ya nchi na huku hakuna masoko, mtuhurumie katika eneo hilo tumehangaika na Wizara sasa tumeleta kilimo chetu Mheshimiwa Waziri wa Fedha msipotusikiliza tutaenda kwa Rais na Rais atafuta hiyo tozo. Kwa nini m-charge mfugaji wa kawaida ng’ombe zake anaenda kuuza Kenya mnamwambia kila ng’ombe alipe shilingi 30,000 huyo ng’ombe tumefuga pamoja? Huyo ng’ombe tumelisha pamoja? Hapana tunagawanaje faida shilingi 30,000 ni mgao gani nchi hii ambao mna-charge shilingi 30,000 ng’ombe peke yake 30,000 kichwa cha ng’ombe mmoja kupeleka Kenya hii si sawa mtuondolee tozo hiyo tugawane nusu mchukue 15,000.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani shilingi 30,000 kila ng’ombe mmoja kupeleka Kenya unalipa shilingi 30,000 kwa nini? Mbona hamna utaratibu halafu huku kwenye Halmashauri unalipia shilingi 2,700, umelipia sijui shilingi 5,000 nyingi ya kutosha hii tozo naomba Serikali ipunguze bei. Naunga mkono hoja. (Makofi)