Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia jioni hii. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu kwa wingi wa neema na rehema zake ambazo anatujalia kila iitwapo leo.

Kwa namna ya pekee kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango - Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake - Mheshimiwa Dkt. Kijaji wakisaidiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kuandaa vizuri sana mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa weledi mkubwa na niseme tu kwamba bajeti hii au mapendekezo haya yamezingatia maslahi ya Taifa na imegusa maslahi ya makundi mbalimbali hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nianze kuchangia kwa kuzungumzia suala la maji kwa Mkoa wa Mtwara kwa bahati nzuri nimepata taarifa kwamba Mheshimiwa Prosfesa Mbarawa alikuwepo Mtwara wiki iliyopita na amefanya kazi nzuri ya kukagua utekelezaji wa miradi katika mkoa wa Mtwara ukiwepo Mradi wa Makonde ambao unagharimu kiasi cha dola milioni 70. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mbarawa lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hii ahadi yake aliyoitoa wakati alipotembelea Mkoa wa Mtwara mwezi wa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee tena naomba niishukuru Serikali kwa upandea wa afya mkoa wetu wa Mtwara umeweze kupatiwa shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya 13 pamoja na hospitali za Wilaya tatu. Lakini napenda niifahamishe sasa Serikali kwamba baadhi ya vituo vya afya vimekamilika. Lakini havijaanza kutumika kutokana na ukosefu wa vifaa tiba pamoja na wataalamu wa kuhudumia vile vifaa. Kwa hiyo, naomba nitoe ombi langu kwa Serikali iweeze kututekelezea au kututimizia haya mahitaji ili kusudi vituo hivi viweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande huo huo wa afya naomba nizungumzie kwa uchache kabisa suala la vifo vya uzazi. Ukingalia takwimu za kitaifa utaona kwamba kuna vifo kwa wastani wa 500 kati ya vizazi hai 100,000 kwa kitaifa. Lakini nilipokwenda Mkoa wa Mtwara kuangalia takwimu nimepata kwamba vifo ni kuanzia mwaka 2015 ni 168; mwaka 2016 ni 146; mwaka 2017 ni 148 na mwaka 2018 ni 245 na hii kati ya vizazi hai 100,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukiangalia utaona kwamba hii iko chini ya wastani wa kitaifa jambo ambalo ni jema. Lakini sasa hii trend ukiangalia vizuri utaona haipo reliable na wala haipo predictable.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya Afya iende kufanya utafiti kwa undani kwamba ni maeneo gani ya nchi yetu yanapekea vifo hivi au hizi takwimu za kitaifa kuwa juu kufikia 500 au zaidi. Lakini pia iangalie na sababu zinazopelekea vifo hivi kufikia juu, nitoe mfano tu mwaka 2015 katika Hospitali ya Wilaya Mkomaindu waliweza kunipa sababu ya vifo vingi katika Hospitali hiyo ya Rufaa ukilinganisha na Kituo cha Afya cha Nanyumbu kwa wakati ule Nanyumbu ilikuwa ni kituo cha afya kabla haijapandishwa hadhi. Walisema kwamba vifo hivi vinachangiwa kwanza umbali wa kutoka kituo cha afya na ni kwa sababu kwamba wakina mama wengi wanapata rufaa kutoka Nanyumbu na wanapekwa pale wakiwa katika hali ambayo si nzuri, wanakuwa na complications fulani, kwa hiyo ndio maana wanakuwa na vifo vingi ukilinganisha na Kituo cha Afya cha Nanyumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwaka jana 2018 pia niliweza kufuatilia Hospitali ya Ligula na Likombe. Data zao zilionesha kwamba katika Hospitali ya Ligula vifo vya akina mama vilikuwa ni vingi ukilinganisha na Kituo cha Afya cha Likombe. Kwa hiyo, niombe tu kwa sababu pale sikupata sababu nini niombe sasa Serikali ingalie maeneo kama haya ili iweze kupanga mkakati madhubuti wa kukabiliana na haya matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamalizi mchango wangu ningependa kuishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuweza kuleta mageuzi ya kiuchumi katika halmashauri zetu na kwa wananchi kwa ujumla. Niseme kwa mfano kuna upanuzi wa bandari ambao unaendelea kule Mtwara, lakini vilevile kuna ujenzi au ukarabati wa uwanja ndege huko huko Mtwara. Niseme tu kwamba shughuli hizi ambazo zinafanywa zitaweza kuzisaidia Halmashauri zetu na Mkoa wetu kwa ujumla kuongeza njia mbalada za kuongeza kipato badala ya kutegemea zao la korosho pekee.

Kwa hiyo, nishukuru sana Serikali lakini hapo niongezee tu kwamba kuna mwenzetu mmoja hapa alikuwa akisema kwamba wananchi wawezeshwe kuanzisha viwanda wa ngozi na kadhalika na kadhalika. Lakini sasa tukirudi nyuma tujiulize kwamba kati ya kuku na yai kinaanza kitu gani. Sasa ni lazima kwanza yawekwe mazingira wezeshi, ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa umeme ambao unaaminika na wa gharama nafuu ni vitu vya muhimu sana kuwepo ili wananchi waweze kuvitumia kwa ajili ya kuzalisha kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema kwamba Mkoa wa Mtwara una vivutio vingi sana ambavyo mazingira haya wezeshi yanaweza yakasaidia katika kukuza utalii kwa mfano ukienda unakuta kuna Shimo la Mungu kule Newala, kuna Mji Mkongwe wa Mikindani, kuna Makonde Plateau, lakini pia kuna beach nzuri sana, kuna mmoja amezungumzia hapa utalii wa pwani. Kwa hiyo, utalii unaweza ukasaidia kuwa kama ndio njia mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuiomba Serikali hasa Waziri wa Elimu kwamba mambo ni mengi ambayo yamefanyika katika nchi yetu, makubwa sana katika awamu hii ya tano, sasa tusiishie kusifia nakupongeza lakini Waziri wa Elimu nimuombe akae na timu yake ya watalam ili waone ni namna gani wanaweza wakayaweka masuala haya yote makubwa na ya kihistoria katika system yetu ya elimu ili kusudi tuweze kurithisha vizazi vijavyo ambao nao wanaweza wakajengewa uzalendo kutokana na mamba haya haya wakawa wazalendo wa kweli, vilevile wakawa majasiri, lakini wakajenga uthubutu kupitia masuala haya muhimu na makubwa ya kihistoria ambayo yameweza kufanyika. Nadhani hakuna haja ya kuyataja sote tunayafahamu ni mambo mazuri nadhani tuanze sasa ili kusudi tuweze kujenga kizazi kijacho ambacho kinaweza kikayatumia masuala haya kuleta maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamalizia niombe kukumbushia Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba walituahidi wataleta sheria ambayo itasaidia kutenga fedha katika Halmashauri kwa ajili ya lishe ya watoto wa chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)