Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia na mimi nafasi hii jioni hii ya leo katika mwaka huu 2019/2020 na mimi nichangie hii bajeti inayokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu ni kilekile lakini kabla ya yote ninapenda kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo imesomwa leo asubuhi na, Mheshimiwa Silinde, Mbunge wa Momba. Hiyo ni hotuba ya Kambi na tunaiunga mkono kwa asilimia mia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kawaida ni yaleyale yanajirudia; mwaka 2016/2017 mwezi Aprili, bajeti ya maendeleo ilikuwa wamefikisha asilimia 57 ya bajeti yote na tukaja tena Bungeni tukawa tunajadili ili tupitishe bajeti ya mwaka unaokuja; mwaka 2017/2018 tulitekeleza kwa asilimia 60; mwaka huu wa fedha 2018/2019 mpaka mwezi Aprili imetekelezwa kwa asilimia 45. Sasa tunasonga mbele au tunarudi nyuma?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati bajeti hii imetekelezwa kwa asilimia 45 mpaka mwezi Aprili, lakini inaonekana makusanyo wamekusanya kwa asilimia 65. Sasa mimi nataka kuhoji Serikali, je, hii bajeti kama mmeitekeleza kwa asilimia 45; kwa hiyo, ina maana asilimia 65 mliyokusanya na sasa hivi imebaki miezi miwili tu/mwezi mmoja au tuseme miezi miwili, mtawezaje kufikia kukusanya hiyo hela ili mtekeleze hiyo miradi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kusikitisha sana; mimi niko kwenye Kamati ya Miundobinu, Kamati hii kwenye Bajeti yote ya Serikali tunakwenda kupitisha hapa tunapewa asilimia 40 ya bajeti yote na tunaposema miundomibu tunaangalia na vipaumbele. Sasa vipaumbele vya hii Serikali ni nini? Kwa hiyo, kilimo haipo kwenye kipaumbele, maji haiko kipaumbele, afya haiko kipaumbele, elimu haiko kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sasa kipaumbele chetu kipo kwenye miundombinu, lakini tukisema kwenye miundombinu hii asilimia 40 inakwenda kufanya nini? Sana sana asilimia kubwa inakwenda kununua ndege kwa hela cash inayokusanywa kutoka kwa Mtanzania maskini, inayokusanywa tunakwenda kununua ndege. Hivi wananchi wa Mlimba leo nikiwaambia jamani hela zinazokusanywa huku zinakwenda kununua ndege hivi ninyi mnadhani watanielewa kule? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sasa hivi barabara haipitiki, watu wanalima kule mpunga sasa hivi wanavuna mpunga, wanavuna ufuta, bei zinazidi kuporomoka kwa sababu barabara ni mbovu, mashimo tupu. Mafuta kule yamepanda bei, nenda piga simu watu wa EWURA Mlimba hakuna mafuta ya dizeli wala ya petroli yaani mpaka natikisika moyo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini hakuna, siyo kwamba kuna ukame wa mafuta bali hakuna gari kubwa inakwenda Mlimba leo. Sasa hivi watu wananunua kule mafuta ya kupima kwenye vigaloni petroli na dizeli, wananunua kwa magendo. Hivi sisi tunajihesabu tuko nchi hii au tuko nchi nyingine? Lakini Mbunge niko hapa napitisha bajeti; bajeti ya nani, inamhusu nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Wizara ya Fedha na Mipango inaniambia uchumi umekua; umekua kwa nani?

Labda kwao wenyewe na makaratasi yao. Lakini kwa Mtanzania wa kawiada kule kijijini uchumi haujakua, hali ni mbaya. Kama leo mtu ananunua lita ya mafuta ya petroli haizidi lita moja unapima kwenye chupa, kwa shilingi 5,000, unamwambiaje mtu huyu kwamba uchumi wake umekuwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ajira za walimu, watoto wa kimaskini katika nchi hii ndio walikuwa wanakimbilia katika mambo ya ualimu. Tangu iingie Serikali hii madarakani walimu wanaoajiriwa kiduchu, tena wameanza mwaka huu wa fedha, leo kundi kubwa la watu wenye ma-degree yao wako barabarani hawana kazi, watoto wa maskini, leo mnasema uchumi umekua, umekua kwa nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tunapoongelea tuangalie sasa kwenye bajeti ya kilimo ambako ninachozungumzia kilimo ndiyo huko kwetu leo bajeti ya kilimo kwenye maendeleo wametoa asilimia moja ya bajeti leo mnasema eti mnaweka kipaumbele kwenye kilimo na asilimia 75 ya wanawake ndiyo wakulima kule vijijini, leo mnaupeleka wapi nchi hii? Msifanye hivyo mnawaumiza hawa wanyonge mnaowasema, hali ni mbaya. Kwa hiyo mnapotengeneza bajeti mlinganishe bajeti ya vitu na bajeti ya moja kwa moja kwa wananchi katika matumizi yao. Kwa hiyo bajeti hii ni ya vitu siyo ya wananchi. Kwa sababu leo mwananchi wa Mlimba hawezi kupanda ndege, hawezi kutumia huo umeme sijui wa Stiegler’s sijui miaka 10 ijayo huko tutakuwa wengine tumeshakufa wengi tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliaminishwa hapa umeme wa gesi, gesi ndiyo mkombozi nchi mimi nilikuwa Bungeni bahati nzuri wengine hapa hamkuwepo, lakini wenzenu ile awamu ya nne tuliaminishwa hapa gesi ndiyo mkombozi wa nchi hii, gesi ndiyo kila kitu leo gesi iko wapi mmerukia kwenye Stiegler’s ninyi vipi? Na mikopo ndiyo tutalipa vipi? Mwisho wachina watakuja kuchukua kila kitu kwetu. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo; mimi ni mkulima lakini mimi kuna wafugaji leo mnasema Stiegler’s sawa mmechukua, Bonde la Kilombero mmechukua ardhi yote imebaki chache kule kuna wafugaji wale wafugaji wanatangatanga, hawana mahali pa kwenda, je, bajeti hii huyu mfugaji au mvuvi inamsaidiaje kwenye hii bajeti uje hapa uwaambie wenzio wanakusikiliza huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema hapa kwenye swali langu la nyongeza pori hili hapa tunalopita kwenda Morogoro hapa NARCO sijui mnaita limekaa tu, halina chochote, halina ng’ombe, sana sana kuna nguchiro tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini katika mpango wenu mahsusi mkasema sasa tunachukua wafugaji wanaohangaika, tunaotesha majani mazuri, tunaleta wataalam, kila mfugaji apewe eneo lake aoteshe majani, anenepeshe ng’ombe, tujenge kiwanda cha ngozi, tujenge kiwanda cha maziwa, tujenge kiwanda nyama ili hivi ninyi mkoje? Uchumi tunao tunaukalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Marehemu Nyerere aliwahi kusema uchumi mnao mnaukalia, kwa nini mnapenda kukalia kalia vitu? Kwa nini mnafanya vitu vikubwa ambavyo Watanzania wengi hawana faida navyo, mnasema ooh tutakuja kupata maendeleo baada ya hivi vitu vyote kuisha ndege, sijui reli sijui nini ninyi vipi ninyi? Mbona reli ya TAZARA mmeisahau? Reli ya TAZARA ilikuwa kila siku kwenye vitabu vyenu mnasema reli ya TAZARA, leo nimepigiwa simu, jana usiku watu wametoka kule Masagati Mlimba wamepeleka tena wametoka usukumani huko wamenunua mchele tani 30, ufuta tani 30 wameweka pale TAZARA na hela wameshalipa tangu tarehe 7 mpaka leo hawajasafirishiwa mzigo wao pale TAZARA. Hivi utendaji gani kwa nini mnawatia watu umasikini? Na bei ya ufuta inazidi kuporomoka Dar es Salaam, yule mkulima kule si anapata hasara? Sasa hapa unasema uchumi umekua, umekua kwa nani wakati yule mtu amekopa benki, atalipa huyo mkopo acheni mambo yetu haya bwana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji; maji bado ni tatizo kubwa, leo mnasema nchi hii ya viwanda, kwetu Mlimba sisi hakuna maji, kuna miradi ambao Serikali imeingia mkataba wameruhusu, lakini hela hawapeleki, kwa nini mnatufanyia hivi?

Suala la kilimo bado narudi kwenye kilimo kwa sababu mimi ni mtoto wa mkulima, leo hiki kilimo mnakipeleka wapi, mmenyang’anya mashamba yameingia huku Stiegler’s tunatunza hifadhi/mazingira, lakini hamjaweka miundombinu ya mabwawa ili ile ardhi ndogo tuliyobaki nayo tupate kumwagilia ili tupate chakula. Hivi mnatuendeshaje sisi watu wa kawaida? Hivi mnatuona kama mataahira? Sisi watu wa kuwapigia kura tu wakati nyingine mnapora tu hamna lolote. Haki ya Mungu, kwa bajeti hii hakuna Mtanzania kule kwa hiari yake mwenyewe akaenda kupiga kura. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Mkoa wa Morogoro mmekuja mmehutubia pale Jamhuri mmewabeba watu kwenye malori kama ng’ombe, lakini sisi CHADEMA tunaenda kufanya mkutano mnatukatalia, hivi hii nini mnafanya mambo gani hapa nchini? Hii nchi mali yenupeke yenu? Acheni haya mambo uvumilivu huu utafika mwisho tunaweza tukavuruga uchumi....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)