Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika,asante sana. Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama. Naomba nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti yake ya Serikali, ni bajeti yenye mwelekeo chanya kabisa kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania, hongera sana Mheshimiwa Mpango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee mradi wa Rufiji Hydro Power ambao umeanza kutekelezwa tarehe 15 Juni, 2019 baada ya utekelezaji wa mambo yote ya msingi ambayo yataiwezesha kufanya shughuli vizuri katika mradi huo. Na mambo ya msingi hayo ambayo yameweza kutekelezwa ni pamoja na barabara, madaraja, kambi za wafanyakazi, maji, umeme, afya na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa utekelezaji wa mradi huu utaleta mafanikio chanya hasa ukizingatia tunaelekea kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda. Tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda, tunahitaji umeme wenye uhakika na umeme wenye uhakika hautapatikana katika maeneo mengine bali utapatikana kutokana na mradi huu wa Rufiji ambao mradi huu ukikamilika utazalisha megawati 2,115 na ili tuweze kuendesha viwanda vyetu hapa nchini ni lazima uwe na umeme wenye uhakika. Kwa hiyo, mradi huu umekuja wakati muafaka kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali ni kuhakikisha mambo haya ya msingi yanafanyika. Ushiriki wa Watanzania katika ujenzi wa mradi huu, huu mradi ni mkubwa na wa kitaifa lakini pamoja na ushiriki huo, mradi huu kuna eneo maalum unatokea na eneo hilo si eneo jingine bali ni Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Kibiti pamoja na Rufiji. Hata kama watapewa ajira watu wengi, lakini kipaumbele nacho kizingatiwe kwa watu ambao wanatoka kwenye maeneo hayo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu ya pili, katika mradi huu ni lazima tuhakikishe kwamba tunahifadhi mazingira; mazingira yakihifadhiwa ndipo tutakapoweza kupata maji ya kutosha katika Mto Rufiji na ili tuhifadhi mazingira na kupata maji ya kutosha ni lazima tuweke kipaumbele katika kuhifadhi mazingira kutoka kwenye mito ifuatayo; Mto wa Kilombero, Mto wa Ruaha Mkuu pamoja na Mto wa Ruegu ambao unamwaga maji kwenye Mto Rufiji hatimaye kuelekea kwenye Bahari Kuu ya Hindi, hayo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi ambalo nataka nilizungumzie ni nishati ya umeme maeneo ya Visiwa vya Delta. Delta ina visiwa visivyopungua 16, kwa hiyo, utakapotekelezwa mradi huu, ni lazima kuweka kipaumbele katika visiwa vile vya Delta ambavyo kuna Simbaulanga, Msufini, Sarai, Saninga na visiwa vingine vingi ambavyo vinapatikana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie suala la gesi; nakuja kwenye LNG ambayo inapatikana kule Likong’o katika Mkoa wa Lindi na huu ni mradi mkubwa wa kitaifa. Katika bajeti iliyopita, Waziri wa Nishati alituita tukaenda Lindi kwenye suala zima la kupata semina juu ya jambo hili, lakini amezungumza kule tulielezwa mambo mazuri, tukaelezwa mradi huu utakuwepo, tukaelezwa kwamba watu watalipwa, maeneo yale hayafanywi shughuli zozote za maendeleo hatima yake kwenye vipaumbele vya Serikali hakuna sehemu yoyote ambayo imeainishwa juu ya mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mpango, utakapokuja kufanya majumuisho, tunaomba utuambie mmefikia hatua gani juu ya mradi huu wa LNG ambao ni mradi mkubwa kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo, nataka nizungumzie suala la umeme wa majumbani. Suala la umeme wa majumbani kutokana na gesi asili, tunahitaji umeme huu usambazwe kwa haraka sana katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi kwa sababu umeme huu bei yake ni tofauti na umeme wa Gridi ya Taifa. Tunaomba hilo lifanyike na lipewe umuhimu wa kipekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda na tunajenga reli. Sasa reli ile inategemea chuma na hiki chuma si chuma kingine bali ni chuma cha Liganga na Mchuchuma. Hatuwezi kuelekea kwenye uchumi wa kati wakati huo tuna maliasili zilizojaa chungu nzima katika Taifa letu. Mradi wa Liganga na Mchuchuma haujapewa kabisa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba mtakapokuja vilevile mtueleze juu ya jambo hili, tumefikia hatua gani? Ni lazima ile miradi ya kimkakati iendelezwe, siyo miradi ya kimkakati inafikia hatua inawekwa pembeni, tunamwekea nani pembeni wakati tuliipitisha sisi wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la elimu; elimu bure imeleta manufaa sana kwa Taifa hili na kwenye elimu bure tumeona kwamba wanafunzi wameongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Sasa tunachohitaji, rai yetu; wakati wanafunzi hawa wameongezeka ni lazima waende sambamba na ongezeko la madarasa, waende sambamba na ongezeko la kuwatafuta walimu, waende sambamba na ongezeko la kuwatengenezea walimu mazingira bora zaidi. Na mazingira bora zaidi ni pamoja na kuangalia maslahi yao, kulipwa madeni yao ambayo yamerundikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama walimu tunasema ualimu ni wito, lakini itafikia hatua – tena wengine sasa hivi wanasema ualimu kazi tu, ualimu si wito na ukimwambia, kwa mfano ukienda shuleni na nina uzoefu kama mwalimu, ukienda shuleni ukawaambia wanafunzi naomba wanafunzi nani anataka kuwa daktari utaona wananyoosha wengi sana; nani anataka kuwa engineer, wanayoosha; nani wanataka kuwa kitu gani, watanyoosha; nani wanataka kuwa walimu, huoni mtoto anayenyoosha mkono kwa sababu ya mazingira yaliyopo. Kila siku anamuona mwalimu alivyovaa, anamuona kama ni mtu dhaifu kwa vile alivyovyaa kumbe mwalimu siyo mtu dhaifu, mwalimu ndiyo anayejenga watu hawa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukisikia kuna madaktari, wamejengwa na mwalimu; ukisikia kuna engineer, mwalimu amefanya kazi, ukisikia kuna wanadiplomasia mwalimu amefanya kazi, ukisikia kuna wanasheria, walimu wamefanya kazi; walimu ndiyo kila kitu katika taifa hili. Kwa hiyo tunachoomba mtakapokuja hapa mtuambie mmejipangaje kuhakikisha kwamba walimu wanapata maslahi yao kwa wakati mwafaka. Ni muhimu sana katika kumjengea uwezo na yeye kujiona kwamba ni part ya wafanyakazi waliopo katika nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba tu nimalizie kwa kusema kwamba tumepewa kipaumbele kwenye kilimo, kweli kwa sababu tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda kilimo ni muhimu sana. Lakini kilimo hiki ni kilimo cha namna gani; kisiwe kilimo cha kutegemea mvua, ni lazima kiwe kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliaji ndicho kitakachotutoa katika mazingira yetu haya na kuelekea uchumi huo wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ikiwezekana mia moja na zaidi. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)