Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii na mimi kumpongeza kwa kweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu kwa bajeti hii ya mwaka huu ambayo ni nzuri sana, ni bajeti ambayo imezingatia maoni ya wadau mbalimbali. Maoni ya Waheshimiwa Wabunge, maoni ya wasomi, maoni ya watu wote wafanyabiashara na ni bajeti ambayo imeepukana na bajeti za mazoea ya kupandisha bei ya sigara, bei ya bia na bei ya soda. Ni bajeti ambayo imekwenda kihalisia, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha Mpango hiki hapa ambacho alisoma asubuhi Mheshimiwa Waziri, Serikali imesema inapanga kuendelea kuboresha na kukarabati shule za msingi na shule za sekondari, ni jambo jema sana hili.

Mimi nimewahi kutembelea Sekondari ya Pugu ninaiona ilivyokarabatiwa inafurahisha sana. Mwanafunzi anaposoma kwenye mazingira, kwenye miundombinu ambayo ni rafiki anasoma vizuri na anaelimika vizuri. Mimi naipongeza sana Serikali kwa jambo hili, naiomba sasa Serikali ikishakarabati shule zote za msingi na sekondari sasa ikarabati walimu, iwakarabati walimu vizuri na kuwapa motisha ili wafanye kazi vizuri kwenye miundombinu ambayo imekarabatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili mimi naomba niiombe Serikali, Chuo cha Ualimu cha Mkwawa ilikuwa sekondari, naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu unisikilize; Chuo cha Elimu cha Mkwawa ilikuwa ni sekondari ilikuwa inaitwa Mkwawa High School, ilikuwa na maabara ya fisikia sita, maabara ya kemia sita, maabara ya biolojia saba. Ilikuwa mkienda Chuo Kikuu cha Dar es Salaama one third ya wanafunzi wanaosoma sayansi wametoka Mkwawa High School. Sasa kulikuwa na umuhimu wa kuwa na walimu wengi ndio maana wakaibadilisha iwe Chuo cha Ualimu. Sasa hivi tuna walimu wa ziada naomba Mkwawa High School irudishwe ya zamani ili tuweze kutengeneza wanafunzi wa sayansi pale, naiomba sana Serikali ifanye katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya hilo Serikali inatoa ruzuku vizuri sana kwenye sekta ya afya inatoa madaktari, inatoa walimu, inatoa madaktari walimu na madawa. Ruzuku kwenye sekta ya afya naiomba Serikali ikimaliza huko igeukie kwenye elimu, itoe ruzuku vilevile kwenye elimu, huwezi kuwa na maendeleo bila kuelimika. Kwa hiyo naiomba Serikali itoe ruzuku kwenye vyuo au shule za watu binafsi ili tuweze kuelimisha jamii ya Watanzania vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mpango huu hapa Serikali inasema inanedelea kuboresha na kukarabati reli ya kati na reli ya TAZARA wakati huo ikijenga standard gauge, ni jambo zuri sana. Tunatumia uchumi wetu wa jiografia vizuri, tunaitumia hali ambayo Mwenyezi Mungu alituweka vizuri. Lakini reli ya TAZARA inasuasua kwa sababu ni reli ya kati ya nchi mbili ndio maana mimi naiomba Serikali ikiwezekana sheria iliyounda reli ya TAZARA irudishwe tena hapa Bungeni tuweze ukikarabati vizuri ili kila nchi ishughulikie sehemu yake ya reli, ile reli ya TAZARA ambayo ilikuwa reli ya uhuru wakati huo sasa hivi ni reli ya biashara ili Tanzania tunufaike na reli hiyo na uchumi wa jiografia ambao Mwenyezi Mungu ametupa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipotembelea Malawi hivi karibuni suala kuu kati ya yeye na kiongozi mwenzie ilikuwa ni reli ya TAZARA, ilikuwa ni Malawi Cargo Centers ambazo zimekufa, ndio sasa naiomba Serikali ifuatilie sana tufufue Malawi Cargo Centers ambazo ziko Dar es Salaam na Mbeya tuifufue vizuri sana reli hii lakini vilevile tujenga bandari kavu Inyala ili mizigo ya Malawi iishie pale Iny’ara pamoja na Malawi Cargo Centers, ikitoka hapo naishauri Serikali ijenga reli kutoka hapo Inyala kwenda mpaka Itungi Port ili tupunguze mizigo ambayo inapita barabarani na kuzifanya barabara zetu ziishi muda mrefu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka kwenye reli nije kwenye barabara, Mheshimiwa Rais alipokuwa ziarani Mbeya tumshukuru sana Mheshimiwa Rais amekaa Mbeya siku tisa bila kutegemea, tunamshukuru sana ahsante sana Mheshimiwa Rais. Aliiongelea barabara ya Tanzam High Way hasa hasa kipande cha pale Mbeya ambayo kuna conjunction kubwa sana, Mheshimiwa Rais akasema Serikali itatoa fedha ya kujenga bypass ya kutoka Mlima Nyoka kwenda mpaka Songwe. Naomba katika bajeti hii Serikali ilifikirie hilo la kujenga bypass ya kutoka Mlima Nyoka kwenda mpaka Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niishukuru Serikali kwa barabara ya Mbeya - Chunya ambayo sasa hivi imeisha Mheshimiwa Rais aliifungua akiwa ziarani, namshukuru sana. Lakini kwetu sisi wana Chunya barabara hii ni mboni ya jicho letu, tunataka kuilinda kwa kila hali, kwa hiyo, naomba Serikali iweke mobile bridges za kuweza kuilinda barabara hiyo na mizigo ambayo ya lumbesa ambayo inaharibu barabara. (Makofi)

Vilevile Mheshimiwa Rais alifungua aliweka jiwe barabara ya kutoka Chunya kwenda Makongorosi, naomba Serikali isimamie kwa karibu barabara hiyo ili kama ilivyo kwenye mkataba barabara hii ujenzi wake uishe mwezi Februari, 2020 ili tukienda kwenye uchaguzi tuwe na mambo ya kusemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisome ukurasa wa 91 wa kitabu cha bajeti; malengo ya bajeti hii amesema Mheshimiwa Waziri makubwa yapo manne nalisema lengo la tatu ambalo linasema kuimarisha kilimo (uzalishaji wenye tija na masoko ya mazao, ufugaji, uvuvi na misitu) kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa sekta hii katika uchumi wa Taifa (chakula, ajira, kipato cha wananchi, michango katika fedha za kigeni na muunganiko wa sekta hii na maendeleo ya viwanda). Katika hili niongelee tu zao moja tu ambalo tunalima Nyanda za Juu Kusini tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku nchi ya Malawi ilikuja kuchukua mbegu Chunya mwaka 1966, leo nchi ya Malawi inatengeneza kilo milioni 200 kwa mwaka za tumbaku wanauza nje, sisi mwaka 2010 tulifika kilo milioni 120 mwaka huu projections ni kilo milioni 54 tunashuka. Naomba Wizara ya Kilimo ijiulize kuna nini kwa nini production zinashuka naomba tutumie Chuo Kikuu cha SUA watafiti wako pale wazuri sana kwa nini kilimo chetu kinashuka, kwa nini hatupati masoko ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali, Wizara ya Kilimo tujiulize mazao mengi mwenzangu alisema asubuhi hapa tumbaku, pamba, korosho inashuka production badala ya kuongezeka kuna tatizo gani? Naomba Serikali ilifikirie sana hilo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi katika hilo zao la tumbaku mwaka huu kuna kampuni nne ambazo zinanunua tumbaku. Kampuni moja imekataa kutoa makisio, kwa hiyo, ina maana kuna wananchi wa sehemu za Tabora, Chunya, Mpanda na Ruvuma, kwa hiyo, wananchi na vyama vya msingi vitakosa kulima na kuuza tumbaku yao. Naiomba Serikali ilichukue jambo hili kwa muhimu sana ili wananchi wa sehemu hizi wapate kulima na kuuza tumbaku na kuinua hali zao za maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme la mwisho, Mheshimiwa Rais alipokwenda Afrika Kusini, nchi ya Afrika Kusini imesema inaanza kufundisha Kiswahili, nchi nyingi, hata nchi ya Kongo nayo imesema wataanza kufundisha Kiswahili, ina maana Tanzania itaanza ku-export kama zao Kiswahili, lakini vijana wetu tulionao hawajaiva kama tulivyoiva baba zao wa zamani ambao tulikuwa tunapitia JKT na tuna maadili ya kutosha. Naomba hawa vijana watakuwa ni mabalozi wetu huko wanakoenda kwa hiyo, naomba Wizara, Serikali, mnapowachagua vijana hawa wa kwenda kufundisha Kiswahili nje ya nchi, iwe ni Afrika Kusini, iwe ni Kongo, iwe Zambia, kwanza tuwafundishe itifaki, tuwafundishe ubalozi kwa hiyo, wasije wakaenda kule wakaenda kututia aibu Tanzania ambayo ni nchi ambayo inasifika duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)