Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii, lakini tu niseme kwamba naunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali kwa asilimia 100 na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni bajeti nzuri sana, na mimi niliyekaa muda mrefu kidogo humu ndani naifananisha bajeti hii na bajeti ya mwaka kama 2005/2006 kama siyo 2004 iliyokuwa chini ya Awamu ya Mzee Mkapa, ilifuta kero zote ambazo zilikuwa zinatatiza kwa nchi yetu na hii imetokea, nikushukuru sana Dkt. Mpango kwa usikivu, nikushukuru sana pamoja na Wataalam wako, naomba tuendelee hivi, kwa sababu kwanza kwa kitendo cha kuondoa hizi ada na tozo 54 ni jambo la kujivunia, ni jambo la kimapinduzi, litainua uchumi na hiyo ni kwa sababu utakuwa umewajali wananchi wa Tanzania, naipongeza sana Serikali na nina ushauri mmoja au miwili katika mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wataalam wako hebu tujaribu kuangalia, mimi bado huwa najiuliza kwa nini huu Mpango wa PPP, hatuutumii, una tatizo gani? Hebu tukae tujifikirie mara mbili mbili, tukiutumia na sheria tumeshatunga. Tukiutumia una matatizo gani? Tukae tujipange vizuri, lakini ushauri mwingine, nikushauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Serikali inaweza ikaongeza vyanzo vingine kupitia dhamana ya Serikali za Mitaa, municipal bond nafikiri nikisema hivyo unanielewa. Hiyo itasaidia kuongeza vyanzo, mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana iliyofanya mimi kama mwananchi, Mbunge wa Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza nikisimama mbele yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha Serikali yangu ambayo ninayoiamini sana, naulizwa sawa, mmeondoa tozo na ada 54 mimi mkulima wa zao la pamba nafaidika nini na tozo hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Kwimba lakini na Wilaya zingine zinazolima zao la pamba, wakulima hawa wanahangaika kama watoto wa bata, zao la pamba sijui lina mkosi gani? Pamba yao wanahangaika hawajui wapi waipeleke, wapi wauze leo msimu wa pamba ulianza tarehe 2 Mei na hili tunalisema, tunalisema, tunalisema. Tarehe 2 Mei mpaka leo hakuna kinachoendelea, zao la pamba hili limekuwa kama vile adhabu kwa mkulima, Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe unajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mazao haya matano haya, major crops yanakuongezea uchumi kwenye hela za kigeni, lakini wananchi hawa wanajiongezea kipato. Sasa leo mazao haya mojawapo zao la pamba, leo tumelitelekeza wananchi wanahangaika bei leo tena kwa bahati nzuri Waziri wa Kilimo hayupo, lakini wameenda huko wameona hali halisi, leo mimi Mbunge message nilizonazo na simu ninazopigiwa zaidi ya mia moja wanauliza Mheshimiwa Mbunge pamba yetu tutaiuza wapi? Tupeleke wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali naomba hili tuchukue hatua za haraka, kwa sasabu wananchi hawa kama watauza pamba yao, watakwenda dukani watanunua simenti, mabati, mbao na pesa itaingia kwenye circulation, hawa wanaouza vifaa vyao pesa zao watalipa kodi, lakini kama leo pesa zao, pamba yao imekaa nyumbani, imerundikana kwenye maghala, hamna mnunuzi, muathirika namba moja atakuwa ni mkulima, lakini na Serikali itakosa kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu mimi niombe sana ikiwezekana Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Waziri mwenye dhamana na Viwanda tuache kufanya siasa kwenye kilimo cha pamba, naona tunafanya siasa, kinachotokea sasa kuna mawakala wako kule ambao wanasema sisi tunazo pesa, tunanunua kwa kilo shilingi 1,200 lakini wanawapa watoe pesa wanakwenda kununua kwa shilingi 500/600/700 lakini huku wanasema tunanunua kwa shilingi 1,200 na hawa ni wafanyabiashara wanunuzi wapo na bahati nzuri Serikali inafahamu tunawachezea wakulima, tunawanyanyasa wakulima wa zao la pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali ya chama changu najua ni sikivu sana kwenye zao la Pamba na imekuwa kila msimu, misimu yote, mara tunapotaka kuanza msimu wa Pamba utasikia mara bei imepanda, mara imeshuka, mara imepanda, mara imeshuka niiombe sana, lakini ukienda kwa umbali zaidi bei ya Pamba unakuta wanauza mpaka shilingi 1,500/ shilingi 1,400 lakini ukija huku, kwa mfano hata leo kama nilivyosema mawakala hawa ambao ndiyo wanunuzi, nafikiri kuna kamgomo baridi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iingilie kati huu mgomo baridi uliopo iutatue, hii siyo bure wanataka wawapandie wakulima wa zao la pamba ili kusudi wawaibie zaidi, kwa kufanya hivyo hata cess ya Halmashauri kwa zile bilioni zako mia saba themanini na ngapi sijui? Huwezi kuzipata kwa sababu sisi Mwanza tunategemea pamba, lakini ili pamba iuzwe na kwa kuona lazima ipitie kwenye Vyama vya Ushirika na kadhalika, sasa kwa kufanya hivyo ile pesa yako Mheshimiwa huwezi kuipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimeona kwenye Finance Act, nikushukuru sana, safari hii hujagusa suala la gaming board kwa sababu kama ulikuwa unagusa na kuna watu wanapitapita na wameshapita na umeshawasikia wanataka kuondoa ile VAT ya 18% kwenye winning tax.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa tafadhali, tafadhali sana usikubali, kwa sababu pale kuna mapato ya kila mwezi unapata bilioni tatu, shilingi bilioni tatu mara kumi na mbili zaidi ya bilioni thelathini na sita usikubali hata kidogo, fumba macho, nenda hivyo hivyo kama mlivyoanza zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini niiombe sana suala la pamba Serikali, Serikali pamba, pamba, pamba burobaa burobaa, pamba naomba sana, sana Serikali iingie kati, naunga mkono hoja. (Makofi)