Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ambayo tumeipata kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia hoja ya Wizara hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuniacha katika Wizara hii kuendelea kumsaidia katika majukumu ya utawala wa ardhi na shughuli nyingine zinazohusiana na ardhi. Nimshukuru Waziri wangu kwa maongozi yake mazuri, ni mentor mzuri kwa kweli anaweza kusimamia watendaji walioko chini yake na kuweza kuelekeza mambo yakafanyika vizuri na kweli tunafanya vizuri. Nimshukuru Katibu Mkuu pamoja na timu nzima yote ya Wizara pamoja na taasisi zilizoko chini ya Wizara, wanafanya kazi vizuri na tunashirikiana na ndio maana pongezi hizi zinakuja kwa sababu ya ushirikiano na namna ambavyo Wizara inasimamiwa.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Tumepokea michango kwa maandishi kutoka kwa Waheshimiwa Waheshimiwa Wabunge 21 na Wabunge 17 wamechangia; kwa hiyo jumla ni 38; kwa hiyo tunawashukuru sana na pongezi zenu tumezipokea kwa sababu kazi kubwa tuliyoifanya tumeiona.

Mheshimiwa Spika, nisiwe mchoyo wa fadhila, niendelee kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Ilemela walioniamini na kunipa fursa hii. Nishukuru na watendaji wanaosimamia sekta hii wakiongozwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza ambaye leo anashuhudia hapa, yuko na maafisa kutoka Manispaa ya Ilemela pamoja na jiji kwa namna ambavyo wanafanya kazi nzuri na ndiyo maana pia mkoa unaonekana umefanya kazi vizuri kwa sababu ya usimamizi.

Mheshimiwa Spika, niishukuru familia yangu nikimshukuru na binti yangu mpendwa, Diana, leo amekuja kushuhudia; nashukuru sana kwa hayo.

Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru Kamati, kwa kweli ushauri walioutoa tumeuzingatia na tutaufanyia kazi. Kama ambavyo Wizara siku zote imekuwa sikivu. Kila wanapotupa ushauri ambao tunaona unajenga zaidi Wizara tunauchukua na tunaufanyia kazi; na kwa kweli kamati imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kutoa ushauri pale ambapo tunaona kwamba tunahitaji oengine kuboresha zaidi, na wamekuwa wakifanya hivyo; na hata hotuba yao wameitoa ilikuwa pia, ina ushauri mzuri. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na kamati yake.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Waziri Kivuli kwa hotuba yake nzuri, naye ametoa changamoto kadhaa na kuweza kutoa ushauri. tutayapitia yale yote ambayo ameyazungumza tuweze kuona namna bora ya kuweza kuyatumia yale yanayojenga; lakini nishukuru tu kwamba mmetambua kazi inayofanywa na Wizara na mpaka mkapongeza pia kwenye taarifa yenu. Kwa hiyo tunashukuru kwamba tunafanya kazi kwa pamoja, kwa sababu tunapojenga taifa moja tunahitaji kushikamana na kuhakikisha tunakwenda vizuri. Ardhi ni mali, ardhi ni mtaji; tusiposimamia vizuri kila mmoja atapata shida; si mpinzani si CCM si yeyote. Kwa hiyo tunashukuru sana pale ambapo tunakuwa tunazungumza lugha moja na inayoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wachangiaji wamechangia mambo mengi, lakini kwenye upande wa mipango miji zaidi ya Wabunge 10 wamechangia na wote wakiongelea habari nzima ya namna ya kuweza kujizatiti katika kupanga makazi yetu yaliyo bora. Wengi wamezungumza, Mheshimiwa Kubenea amesema, Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mheshimiwa Aida Khenan, Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mheshimiwa Mahmoud Jumaa, Mheshimiwa Charles Mwijage, Mheshimiwa Lwakatare, Mheshimiwa Mzava, Mheshimiwa Kamili, Mheshimiwa Selasini, wote wamechangia upande wa mipango miji.

Mheshimiwa Spika, napenda tu niseme kwamba, Wizara siku zote inajizatiti kuhakikisha kwamba miji yetu inapangwa vizuri. Ndiyo maana kama mlisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tunayo miji zaidi ya 30 ambayo Master Plan zake zipo zimekamilika, kama Halmashauri 12 hivi, na nyingine ziko kwenye hatua nzuri ambayo tunakwenda; lengo ni kuhakikisha miji yetu inapangwa.

Mheshimiwa Spika, tatizo tunalokumbananalo tu ni kwamba staff tuliyonayo bado haitoshelezi kuweza kufanya kazi ile, na utaalam pia wa mipango miji unahitaji kuwa na timu ya wataalam inayoweza kufanya kazi ile kwa kasi kubwa na kuweza kufanya kazi inayokusudiwa; lakini lengo na dhamira ya Wizara ni kuhakikisha miji yetu imepangwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Stanslaus Mabula alizungumzia habari ya watu walioko milimani; na kama unavyojua Mji wa Mwanza una milima na kama ilivyo maeneo mengine kuna milima:-

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo ambayo yalikuwa yameachwa kwenye suala zima la urasimishaji katika kupanga ile miji yetu. sasa lile eneo lilikuwa limeachwa kwa sababu jiji lenyewe lilikuwa na mipango ambayo walisema kwamba wao ndio wanatarajia mipango hiyo. Hata hivyo kwa hoja aliyoizungumza, ya kwamba tunahitaji pia kuwawezesha wale wananchi ili waweze kuwa na nguvu kiuchumi kwa kutumia rasilimali yao. Kwa sababu Halmashauri ya Jiji ina mpango wake leseni za makazi haziwezi kuzuia ule mpango kuwepo. Kwa hiyo, kwa hoja aliyoitoa kama Wizara tumeichukua, tutaona namna ya kuifanyia kazi vizuri ili wale wananchi ambao hawakupimiwa kipindi kile waweze kupimiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Selasini amezungumzia habari ya kukopesha halmashauri zetu ili ziweze kupima na kupanga. Niseme tu, ni juzi tu hapa tumetoa mikopo ya bilioni 6.2 hivi kwenda kwenda kwenye Halmashauri 24; na Halmashauri hizo zimepewa mkopo na masharti waliyopewa ni kwamba wahakikishe wanafanya upimaji vizuri, wanauza viwanja vyao na wanarejesha. Wakirejesha vizuri tunawapa tena; kadiri unavyokopa na kurejesha vizuri tunawapa kwa sababu tunajua hili suala la upangaji ni suala endelevu. Kwa hiyo, hiyo inafanyika na Wizara imeshalichukulia hatua vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika suala zima la upangaji tunapokuwa tunaendelea kupima kuna maeneo ambayo halmashauri zetu pia zinazungumza na wananchi kama kawaida, pale ambapo miji inakuwa imetangazwa kuwa iko chini ya mipango miji. Kuna namna wanavyokubaliana kiasilimia, utakuta Chemba wanakubaliana 60 kwa 40, ukienda kule Mkinga nao wamekubaliana; lile nalo linaharakisha zoezi la kupima kwa sababu unakuwa umeshawashirikisha moja kwa moja. Sasa kwa sababu hawana ile pesa ya kutoa moja kwa moja wanaridhia kutoa sehemu ya ardhi yao ili iwe ni pesa ya mchango kwao kwako wewe kuweza kuwapimia na kuweka miundombinu; na hili linafanika bila tatizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niseme tu, tutoe rai kwa halmashauri zetu waendelee kutumia mpango huu ambao tunaweza kusema ni barter trade, kwa sababu hela huna lakini ardhi unayo. Kwa hiyo unatoa kwa asilimia wanayokubaliana, wengine wana 70 kwa 30, wengine 60 kwa 40; lakini lengo letu ni kuhakikisha kuwa imepimwa. Wizara inachosema tu ni kwamba, haturuhusu kuchukua ardhi ya mwananchi bila kumlipa fidia, haturuhusu kuchukua ardhi ya mwananchi bila ridhaa na haturuhusu kuchuku ardhi ya mwananchi hlafu ukakaanayo bila kuiendeleza. Kwa hiyo hayo ndiyo maelekezo ya Wizara ambayo tunasema lazima yazingatiwe.

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia suala la sera; kwa kweli ni jukumu la Wizara na tunakiri kwamba usimamizi wa sera na sheria katika Wizara ni jukumu letu la msingi katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na sera ambazo katika utendaji zinatuongoza.

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema, ni kweli Sera Nyumba, kama alivyoiongelea, kwamba inahitaji kuwepo; ni kweli na sisi tunaliona hilo lakini tayari mchakato ulikwishaanza, draft za mwanzo zilishafanyika na tulishaanza pia kupokea maoni. Kwa hiyo bado iko kwenye mchakato, itakapokuwa tayari tutaitoa kwa sababu tunaona ni pengo lililopo kweli, pasipokuwa na hiyo tunasema tunaposema tunataka kuwa na makazi bora, tunataka kuwa na nyumba bora, kama huna sera ambayo ipo itakuwa ni shida. Tunayo Sera ya Makazi ya 2000 lakini inahitaji maboresho fulani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anazungumzia ameongea kwa kina sana kuhisiana na hizi sera na mpaka aliongelea masuala ya real estate; ya kwamba tunahitaji pia kuwa na hiyo sera ambayo inasaidia sana katika kuhakikisha kwamba hawa waendelezaji milki hawajifanyii tu mambo yao jinsi wanavyojua. Ndiyo maana tunaona wengi wanajenga halafu na gharama na nini zinakuwa pia ni kubwa sana kulingana na hali halisi kwa sababu tu hicho chombo hakijawepo na kuweza kuwasimamia. Kwa hiyo hili kama Wizara tumelichukua na tunaendelea kulifanyia kazi kwa sababu tayari liko kwenye mchakato wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia migogoro ya matumizi ya ardhi. Mheshimiwa Yussuf ameongea vizuri na ni Mjumbe wa Kamati, Mheshimiwa Abdala Mtolea amezungumza, Mheshimiwa Mndolwa ameongea katika haya katika masuala ambayo yanahusiana na migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kumekuwepo na migogoro ya ardhi katika maeneo mengi lakini tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa busara zake ambazo alizo nazo. Migogoro imekua ni mingi katika sekta mbalimbali, lakini Wizara zote za kisekta zimewekwa katika timu moja ambayo imepitia; na wakati Mheshimiwa Waziri anatoa hotuba yake pale alionesha kitabu kimoja kikubwa sana, kina migogoro ya kila aina mle ndani kulingana na sekta. Iko ya matatizo ya kwenye vyanzo vya maji, iko ya Jeshi la Wananchi na wananchi wenyewe, iko ya ardhi kwa wafugaji na wa kilimo, yaani iko ya aina nyingi. Kwa hiyo wamepitia mgogoro mmoja baada ya mwingine.

Mheshimiwa Spika, na hata kama hawakufika kwenye eneo lako, maana kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliongea kwamba hawajafikiwa kwenye maeneo yao; lakini hatua iliyochukuliwa imegusa maeneo hayo, hata kama hawakufika unaweza ukakuta kwenye kitabu kipo kwa sababu wamehusishwa Wabunge. Ninyi wenyewe mlitoa migogoro pale ndani Mheshimiwa Waziri akawa anaipokea. Wakuu wa Mikoa walishakaa nao kila mkuu wa mkoa alipewa nafasi ya kuzungumzia wakatoa ile migogoro waliyonayo; lakini pia bado wananchi kwenye programu ya FUNGUKA NA WAZIRI wametoa. Kwa hiyo yale yote ambayo wameyakusanya sasa tunaangalia namna ya kuyapatia ufumbuzi kwa sababu ni jambo ambalo ni kubwa na linaingiza sekta nyingi. Kwa hiyo niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge tujaribu kuvumiliana katika hili ili tuweze kuona ni jinsi gani ambavyo tutaweza kulimaliza.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea suala la hati kutotoka. Kuna Mbunge mmoja amechangia kwa maandishi anasema hati hazitolewi. Kwa kweli, mimi nitashangaa kama tatizo hilo lipo kwa sababu Mheshimiwa Waziri hapa wakati anatoa hotuba yake ameonesha pia hata katika picha; zaidi ya hati 6,000 ziko kwa Dar-es-Salaam peke yake. Ukienda Mwanza kuna zaidi ya 2,000; nilikwenda pia Bagamoyo kule nikakuta kuna hati ziko pale zaidi ya 100, ziko tayari na watu hwachukui, zimeshalipiwa na hazidai. Hata hivyo kuna wengine ambao wameshapimiwa hawataki kuchukua hati kwa sababu wanaogopa watadaiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu hili Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia Julai 1, kama tunavyosema, yeyote ambaye amepimiwa ardhi yake, amelipia upimaji halafu hataki kuchukua hati kwa sababu tu atadaiwa kodi ya ardhi, maadam tayari ukishapanga na kupima umeshaingia kwenye system ambayo tayari tunajua kodi yako ni kiasi kadhaa na invoice unayopewa inaonesha kodi yako; tutaanza kuwadai wote, watalipa kodi ya ardhi uwe una hati hauna hati, maadam umepimiwa na tunajua wewe eneo lako ni hilo basi tutajua kwamba tutakudai. Tuwaombe sana ndugu zetu, kwa sababu tunasema ukikaa bila kuwa na hati ile ardhi yako haikusaidii. Huwezi kufanya shughuli zozote za kimaendeleo ambazo unaweza ukasema pengine uende benki upate mkopo ufanyie shughuli za kuweka dhamana mahali, hauwezi. Mimi nitoe rai tu kwa wananchi wote kwamba wafanye hiyo kazi ya kuhakikisha unakamilisha hatua nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Mheshimiwa mmoja amezungumzia habari ya upimaji kwenye urasimishaji kwamba watu wanalipa halafu hawapewi hati. Pia hapa kuna mambo mawili, kuna watu wanalipia upimaji halafu wanasahau kwamba hati inakuja kwa hesabu yake tofauti. Ile ya upimaji ni tofauti na ile unayolipia kwa hati. Kwa hiyo mimi niseme tunaendelea kuwaelimisha wananchi ili kwamba unapokuwa umelipia upimaji haina maana kwamba sasa unamilikishwa lazima pia gharama za kumilikishwa utapewa kwa sababu gharama za umilikishaji zinategemeana na ukubwa wa eneo, eneo mahali lilipo na matumizi ya eneo. Kwa hiyo haziwezi kuwa sawa, haziwezi kuwa flat rate kama hizi ambazo tunasema ni za upimaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wakalalamikia kwamba, gharama za upimaji ni kubwa. Gharama za upimaji zinaweza kushuka kutoka hata hapo 150,000 ilipo kutegemeana tu na idadi ya viwanja na makubaliano. Tumekwenda nadhani Chemba wanadai kama 90,000/= nadhani, halafu Mkinga wana 60,000/=; kwa nini wengine wana-charge 60 wengine 150,000/=?

Mheshimiwa Spika, 150,000/= iliwekwa kama bench mark, kwamba haitakiwi izidi hapo, lakini inaweza ikashuka na kushukla kwake kunategemea pia na ile scope ya kazi anayokwenda kufanya. Kwa hiyo mimi niseme kuwa hayo yanawezekana; lakini pia halmashauri zinahimizwa kutumia vifaa vya ofisi ambavyo vipo vya upimaji, vinatolewa bure na hivi vinaongeza kasi, na watumishi walioko kwenye kanda wanayo nafasi ya kuja kwenye halmashauri zetu kuhakikisha kwamba wanasaidia katika zoezi la upimaji. Tukitumia fursa hiyo tuliyonayo hatutakuwa na tatizo katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia habari ya matatizo kwenye mabaraza ya ardhi na utendaji wa watumishi usioridhisha; na hii si kwenye mabaraza ya ardhi tu na katika ofisi nyingine za umma ambazo zimezungumziwa kwamba, usimamizi na utumishi wa sekta lazima uimarishwe kwa sababu, kuna watu wanakwenda ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba, ikama ya watumishi kunzia Wizarani mpaka na taasisi zake bado iko chini. Wizarani tulitakiwa kuwa na watumishi 1,692 lakini tulionao ni 945 tu, maana yake tuna upungufu wa 747. Ukiena kwenye mabaraza tunao 173, lakini wanahitajika 844, tuna upungufu wa 671. Halmashauri 1,546 na walitakiwa kuwa 2,957 hivyo wana upungufu wa 1,411.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema kwenye hotuba yake, tunafanya upangaji upya wa watumishi katika Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba tunawapanga kulingana na mahitaji, tunawapanga kulingana na taaluma zao katika maeneo ambayo wanayo. Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba tuwe na subira haya yanafanyiwa kazi na tutaendelea kushirikiana pale ambapo tunahitaji kuboresha kutokana na michango mnayotupa.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naendelea kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)