Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia kidogo kwa hizi dakika tano na nitazitumia vizuri. Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina ubora wake, lakini pia kuna matatizo mengine madogo ambayo yapo, kwa hiyo naomba nichangie kwenye matatizo madogo ambayo yapo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuna matatizo ambayo yako kwenye Wizara hii. Sisi Wilaya ya Hanang tulihitaji ardhi ile ambayo imerejeshwa kwa wananchi shamba la Gawal na shamba la Wareet kufuta hatimiliki ya awali ili wananchi waweze kugawiwa maeneo yao waweze kupata hatimiliki, lakini ofisini kwa Mheshimiwa Waziri naona kuna ugumu sana wa kuweza kufuta hiyo hatimiiki na tunaomba alifanyie kazi hilo kwa sababu ni muhimu sana, wananchi wanahitaji hatimiliki lakini hawawezi kupata mikopo kutokana na ugumu uliotokana na Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine la pili, napenda kuzungumzia suala la migogoro; sisi Wilaya ya Hanang tuna mashamba ya NAFCO ambayo kwao yamebinafsishwa kwa wawekezaji na tuna mgogoro sana na mwekezaji mmoja ambaye ni Ngano Limited au kwa jina lingine analitumia Rai Group, yeye ni wa Kenya, alibinafsishiwa mashamba matatu. Cha kushangaza huyu mwekezaji analima asilimia 30 tu tangu amepewa yale mashamba. Sasa Mheshimiwa Waziri nimesikia akinyang’anya mashamba ya watu wengine ambao hawajayaendeleza, sasa huku Hanang kwa nini ameshindwa kufika na wakati anafika hata Babati.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afike Hanang akatembelee hayo mashamba ambayo yanaitwa Ngano Limited ayaone yakoje, lakini kwa taarifa fupi napenda kumweleza kwamba Halmashauri ya Hanang inategemea cess kutokana na mazao. Sasa hivi tumekosa hiyo cess kwenye mashamba hayo matatu, tulikuwa matajiri kutokana na kupata hiyo cess, lakini mashamba hayalimwi hata kidogo na wao wenzetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimweleze kwa kifupi Mheshimiwa Waziri aelewe kwamba shamba la Gidagamowd lina hekari 16,330 ambazo amebinafsishiwa huyo Ngano Limited. Yeye analima hekari 5000 tu, hekari 11,330 hajalima, hii ni miaka yote tangu amepewa hayo mashamba, yanakaa hivi hivi ni mgogoro.

Mheshimiwa Spika, shamba lingine ni shamba la Murjanda alilobinafsishiwa huyo bwana ambalo lina ekari 13,400, kwa hiyo anayolima yeye ni ekari 6000, ekari 7,400 halimi.

Mheshimiwa Spika, angalia tena shamba lingine la tatu ambalo amepewa huyo mwekezaji ni shamba la Setchet, shamba hili lina hekari 16,300, analima hekari 3,500 tu, hekari 12,800 halimi. Mheshimiwa Waziri hebu aangalie kati ya hekari hizo zote hekari 34,000 mwekezaji huyo halimi, je angeyaachia yale mashamba kwa wananchi si yangelimwa yote na tungepata cess sisi Wilaya ya Hanang? Sasa hatupati cess, wewe pia kwenye Serikali hupati kodi yoyote kwa sababu ya tatizo alilonalo. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa undani na kwa huruma kwamba Wanahanang sisi tunategemea kilimo, sasa kama halimi ya nini? Yarejeshwe kwa wananchi ili waendelee kuyalima, hatuna sababu ya kuwa na wawekezaji ambao hawafanya au hawatekelezi wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la tatu napenda kuzungumzia suala la kupima viwanja. Tuna tatizo la mpango wa upimaji shirikishi, kwa sababu matatizo haya yanatokea kwa Wilaya ya Hanang kutokana na kutokuwa na majalada na headed paper kwa sababu inabidi Wilaya ya Hanang wakachapishe kwenye government printers na ni ghali. Matokeo yake upimaji unakuwa wa gharama ya juu, tunaomba Wazri atusaidie tunafanyaje ili gharama ziwe chini na Wizara yake ndio inaweza hilo. Sasa kama hawataweza kuwawezesha Wataalam wetu walioko wilayani au wale ambao ni wataalam ambao sijui ni wa upimaji shirikishi uliopatikana siku hizi, basi wawawezeshe ili gharama ziwe za chini na wananchi waweze kumudu.

Mheshimiwa Spika, ya kwangu ni hayo, sina mengi ya kuongea zaidi ya kutaka Mheshimiwa Waziri afike Wilaya ya Hanang kutatua hiyo migogoro. Haya mashamba hata sisi tuna uwezo wa kulima. Ahsante sana. (Makofi)