Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika Wizara hii. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo inayobeba maisha yetu sisi wananchi wote tuliomo ndani ya Tanzania na Wizara hii inajukumu kubwa sana. Kwa hiyo, nitachangia kwa kadiri ya uwezo Mungu aliyonipa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kijukuu changu, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa namna ambavyo wanafanya kazi na sisi Kamati wanatushirikisha katika utendaji wa kazi yao. Pongezi hizi ziendane sambamba na utendaji ambao umetukuka ambao wanao Mungu awajalie waende mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ardhi haiongezeki, lakini idadi ya watanzania inaongezeka, idadi ya mifugo inaongezeka, shughuli za kibinadamu zinaongezeka, mahitaji ya vitu vilivyopo juu ya ardhi na chini ya ardhi yanaongezeka lakini ardhi yetu inabaki pale pale. Sasa ni lazima tuishauri Serikali iangalie namna bora ya kupanga matumizi bora ya ardhi kwa haraka ili tuwe na kilimo cha kisasa, tuwe na ufugaji wa kisasa lakini pia tutumie maliasili zetu kama misitu na maeneo yaliyohifadhiwa vizuri kwa sababu hayo yatabaki hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, hebu tujenge picha ya miaka 50 ijayo, watanzania ambapo wanaweza kufikia idadi ya milioni 100 hali itakuwaje na ardhi yetu ni ile ile. Ama inazidi kupungua kwa sababu ya erosion na mambo mengine ya mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, ni lazima Wizara iwezeshwe kupewa fedha kwa ajili ya kupanga matumizi bora ya ardhi ili tuweze kukabiliana na changamoto ilinayokuja hapo mbele ya ongezeko la idadi ya watu, idadi ya wanyama, idadi ya matumizi yale tuweze kuendana na hali halisi ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia miaka mitano tu au kumi tusipoangalia zaidi ya hapo tutakuja kukuta tunaachia vizazi vyetu matatizo makubwa sana ya ardhi. Kwa hiyo, tuiombe Serikali kwa heshima kubwa na taadhima kubwa na mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, itoe fedha kumuwezesha Waziri wa Ardhi na Watendaji wake waweze kupima ardhi na kupanga matumizi ya ardhi na yasimamiwe kwa faida yetu na maisha yetu na kizazi kijacho. Vinginevyo tutajikuta katika hasara kubwa sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la migogoro ya ardhi. Hili litaendelea kuwepo lakini inaumiza kichwa kuona bado kuna migogoro ya ardhi ya wilaya na wilaya, kuna migogoro ya ardhi baina ya kata na kata, kuna migogoro ya ardhi baina ya kijiji na kijiji. Kwanini, wakati yote hayo yanasimamiwa na taasisi moja, au vitu vyote hivyo viko chini ya Serikali. Ninavyoona na ninavyojifunza tukiwa kwenye Kamati tunapokwenda huko ni kwamba, suala la ardhi, sera na mambo mengine yako chini ya Wizara. Huko chini mmiliki wa ardhi ni halmashauri, ni kijiji, wao ndiyo wenye maamuzi, sasa hapa kutakuwa na mvutano. Waziri anasema sera inasema hivi, lakini mwenye ardhi ambaye ni kijiji au ni halmashari yeye anataka hivi. Kwa hiyo, huu mvutano tuiombe Serikali ikae pamoja ione namna bora ambavyo masuala ya ardhi yatakuwa katika sehemu moja na yataweza kufanyiwa kazi kulingana na ardhi yetu ilivyo.

Mheshimiwa Spika, lingine niombe, migogoro yote inasababishwa na kutopangwa kwa matumizi ya ardhi, ardhi kutokupimwa. Haijulikani maeneo ya mifugo, haijulikani maeneo ya kilimo, haijulikani maeneo ya hifadhi, maana yake hifadhi nazo zimevamiwa, wananchi wanagombea maeneo ya hifadhi, wananchi wanagombea maeneo ya misitu. Yatakapopimwa na hili ndiyo suala ambalo litaleta msukumo mkubwa sana wa kutatua matatizo hayo. Kwa hiyo, haya yatakapopimwa yote na matumizi yakapangiwa na hali halisi ikaenda kama ilivyopangwa, basi haya yatatatuka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali, namshukuru Mheshimiwa Rais ameunda Kamati ile ya Wizara nane; Mawaziri nane, wamepita wamekwenda kuangalia hizo changamoto zilizopo huko, sasa waje hapa na hiyo taarifa baada ya kuipeleka kwa Mheshimiwa Rais ili na sisi kama kuna mvutano wa sheria na upo, kwa sababu tunaona sheria zinavyovutana. Sheria ya ardhi haioani na Sheria ya wanyamapori, kwa hiyo migongano ya sheria hizi ili tuzifanyie marekebisho kwa haraka ziweze kuendana na wakati na tuone sasa ardhi hii badala ya kuwa neema kwetu inakuwa balaa ili tatizo hili liondoke. Leo watu wanauana, watu wanapigana kwa sababu ya ardhi. Haiwezekani katika nchi ambayo watu tuko na amani na tunaweza tukakaa, tukazungumza na tukarekebisha sheria zetu kulingana na mahitaji na matumizi ya ardhi tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nataka nikizungumze ambacho binafsi hakinipi raha ni kuona kwamba kuna baadhi ya watu wanamiliki ardhi kubwa sana na hawaitumii. Kuna baadhi ya watu wanamiliki viwanja kumi na tano, ishirini, thelathini, wakati watu wengine hawana. Sasa haya maadam yanajulikana, ni miongoni mwa haya matatizo ambayo yanasababisha watu kwa watu kupigana. Kwa hiyo, tuiombe Serikali sasa kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri ili kila mtu aliyepewa ardhi aweze kuitumia, na kama haitumii basi tutumie taratibu za kisheria kuona kwamba kama ardhi huitumii basi wapewe wanaoweza kutumia ili kuondoa hii migogoro ambayo inasababisha siku hadi siku kuleta hatari katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie kidogo kuhusu National Housing. National Housing ilikuwa inakwenda vizuri sana na mpaka sasa Shirika hili lilikuwa linatoa picha kwamba ni shirika moja zuri ambalo linatuletea tija lakini katika kipindi cha mwaka mmoja takriban sasa au zaidi kidoho shirika hili linasua sua. Tunaomba kabisa…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, dakika moja tu nimalizie sentensi yangu. Tunaomba kabisa Serikali iruhusu ile mikopo waliyokuwa wanachukua shirika hili ili waweze kuchukua mkopo wamalizie yale majengo waliyonayo lisipate hasara. Nakushukuru sana.