Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika sekta yangu ya nishati na nikushukuru sana kwa kunipa hii fursa nikiwa msemaji wa karibu na mwisho.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia ningependa nitoe shukrani kwanza kabisa kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na miongozo thabiti katika kutekeleza shughuli za Wizara yetu, hakika tunamwombea kila la heri katika usimamizi wa shughuli zake za kuliongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anavyotuelekeza kusimamia miradi hii na sughuli mbalimbali za Wizara yetu na niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake thabiti, sisi kama Mawaziri kutusimamia kutekeleza majukumu ya Serikali. Niendelee kumshukuru sana Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kusimamia vyema Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe mwenyewe kwa miongozo mahiri sana katika shughuli za Bunge. Nadhani kila mtu ni shahidi, hongera sana Mheshimiwa Spika. Namshukuru sana Mhshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote katika michango yetu tuliyopata, ushauri na maoni mbalimbali. Nikiri kwamba yote tutakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Naibu Waziri wangu, Mheshimiwa Subira Mgallu jinsi anavyonisaidia katika shughuli mbalimbali katika Wizara lakini katika kufuatilia mambo ya utekelezaji wa Wizara yetu. Niendelee kuwashukuru sana watendaji wa Wizara yetu na taasisi zake pamoja na bodi zake zikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara yetu Dkt. Mwinyimvua.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Chato napenda popote walipo niwashukuru sana kwanza kwa kunifikisha hapa, lakini pia kwa kuniombea kutekeleza majukumu ya Serikali huku na shughuli ya jimbo naendelea nayo. Hongereni sana wananchi wa Chato, tuko pamoja na ninyi, tembeeni kifua mbele.

Mheshimiwa Spika, niipongeze na kuishukuru familia yangu ikiongozwa na mke wangu Violeth Kalemani ambaye ananiwezesha, kuniandaa vyema kusimama mbele ya Bunge lakini hata katika utekelezaji wa majukumu ya Kiserikali, mama Vaileth na watoto wako, watoto wangu pia, hongereni sana na Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba sasa nirudi kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge. Kwanza tumekiri kupokea mawazo na ushauri juu ya hoja mbalimbali za maandishi takriban 58 na michango mingine ya kuzungumza 52, kwa hiyo tuna jumla ya michango 110, lakini tunatambua bado michango mingine itaendelea kuja na sisi tunasema m bele ya Bunge lako Tukufu tuko tayari kuipokea na kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo machache, naomba nijielekeze kwa jumla jumla haitakuwa rahisi kujibu hoja moja baada ya nyingine. Nitaanza na kuchangia katika mradi muhimu wa kipaumbele katika Taifa letu wa kuzalisha umeme kutokana na maporomoko ya Mto Rufiji, megawatt 2,115.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, hoja hii imejadiliwa sana na bila shaka hakuna Mtanzania hadi sasa asiyejua umuhimu wa mradi huu. Kilichobaki Waheshimiwa Wabunge na Watanzania hebu tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wetu, tuutekeleze mradi huu, tufike tunakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili nina mambo matatu makubwa, la kwanza ni la ufahamu tu, hivi mradi huu unachukua eneo gani linalosemwa kwamba likiharibika ustawi wa jamii utakosekana? Hifadhi ya Selous ina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000, eneo linalochukuliwa na mradi kwa ujumla wake kwa maana ya miundombinu yote ni kilometa za mradi 914.2 sawa na asilimia 1.8 ya eneo lote, hilo ni jambo la kwanza, ni muhimu sana Watanzania tukaelewa. La pili, katika hilo, tuta litakapojengwa eneo lile ni eneo dogo zaidi ukilinganisha na eneo lote la Selous ambalo ni kilometa za mraba 0.025 sawa na asilimia 0.025, eneo dogo sana.

Mheshimiwa Spika, sina sababu ya kuelezea sana katika hilo. La pili, mradi huu utakapokamilika utatupatia megawatts 2,115, uwezo wetu wa sasa wa umeme tulionao tuna jumla ya megawatts 1601.92 haufikii hata umeme tutakaopata kutokana na mradi huu. Kwa hiyo hapa naeleza manufaa ya haraka ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, la pili, suala la uharibifu wa mazingira limetajwa sana. Ni suala la kujiuliza wala halihitaji elimu ya juu sana. Leo hii tunapoongea wananchi wa Dar es Salaam wanatumia mkaa kwa mwezi magunia 5 00,000 ambapo kila gunia lina kilo 100, hapo ni Dar es Salaam peke yake. Wananchi wa miji mingine matumizi yao katika masuala ya nyumbani ni asilimia 68 lakini wananchi wa vijijini matumizi yao ya mkaa ni asilimia 27, lakini matumizi ya kuni ni asilimia 73, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, ukijumlisha mkaa unaotumika Dar es Salaam na maeneo mengine, ukajumlisha mkaa unaotumika vijijini na maeneo mengine pamoja na kuni zinazotumika vijijini pamoja na mengine ni sawa na tani moja ya futi za ujazo ya mkaa pamoja na kuni zinazotumika ambayo inaweza ikavunwa katika eneo la hekta za ukubwa wa futi za ujazo 10 mpaka 12. Maana yake ukataji wa mkaa na kuni ni mkubwa zaidi tukiachia kutekeleza mradi huu kwa sababu Watanzania wengi wataendelea kutumia kuni na mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa hoja ya bure ni hii, hivi tukiacha kutekeleza mradi huu, tukaendelea kukata kuni na mkaa kwa hali hii hivi nani anaharibu mazingira. Tukiutekeleza mradi huu utatuwezesha kusambaza umeme mpaka vijijini. Kusambaza umeme mpaka kwenye miji, kusambazia umeme Jiji la Dar es Salaam linalotumia mkaa mwingi na hivyo kuokoa uharibifu wa mazingira. Kwa hiyo summary yangu katika hilo suala la mazingira, kuutekeleza mradi huu ni kutunza mazingira zaidi kuliko kuacha kuutekeleza mradi huu. Hii ni hoja ya msingi sana, ya bure kabisa na niwaombe Watanzania watusikilize, watufuate, tuutekeleze mradi huu. Tuepuke kuharibu mazingira yetu. Hiyo ni hoja ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, gharama za mradi; ili uzalishe megawatt moja ya mradi huu, upate unit moja ya umeme utatumia shilingi 36 tu basi. Kwenye vyanzo vingine hali ikoje? Kwenye gesi nianzie hapo na haina maana kwamna naiponda gesi, nitaizungumza vizuri na yenyewe, kwenye gesi tunatumia shilingi 147 kwa unit, moja kwenye solar tunatumia shilingi 103 kwa unit moja, kwenye upepo tunatumia shilingi 103.2 kwa unit moja, kwenye makaa ya mawe shilingi 118 kwa unit moja. Ukienda kwenye nuclear ambayo bado ni 65 ambayo ndiyo inafuatia kwa wepesi pamoja na jotoardhi. Sasa tujiulize tunataka umeme wa ghali au mwepesi, tunataka tuzalishe umeme wa gharama nafuu ili Watanzania wa Maneromango kule waununue wa bei ya chini, hilo ndilo lengo la Serikali. Kwa hiyo gharama ya utengenezaji na uzalishaji wa mradi huu bado ni mwepesi ukilinganisha na miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu, umeme mchanganyiko; Waheshimiwa Wabunge na Watanzania naomba niseme kutekelezwa kwa Mradi wa Rufiji hakumaanishi hata kidogo (kamwe) kutotekeleza kutumia gesi, kutotumia solar na miradi mingine. Tunakwenda na umeme mchanganyiko, Waingereza wanasema energy mix na ndiyo maana leo umeme mkubwa tunaotumia hapa nchini kwa sasa ni umeme wa gesi asilia ambao katika jumla ya megawatts 1601.92 t unatumia gesi yenye umeme wa sasa megawatts 884 sawa na asilimia takriban 60 ya umeme tunaozalisha. Maana yake bado tuna kipaumbele cha kuzalisha umeme kwa kutumia rasilimali ya gesi. Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, matumizi ya gesi sio kuzalisha umeme tu, yako matumizi zaidi ya mara tano ya matumizi ya kuzalisha hiyo. Mpango wetu, tumegawanya mpango wa matumizi sahihi na endelevu ya rasilimali ya gesi kwa miaka 30 ijayo ambayo iko subject to review na yenyewe. Kwa sasa tumetenga takriban 8.8 kuzalisha umeme peke yake, lakini bado kwenye gesi hiyo hiyo tuna futi za ujazo 4.3 kwa ajili ya viwanda vitakavyokuja. Tunataka tujenge viwanda vya mbolea na petrochemicals na ni gesi hii hii tutaitumia. Hayo ni matumizi mengine.

Mheshimiwa Spika, pia tunataka tuwasambazie Watanzania gesi hii ili itumike kwenye viwanda vidogo vidogo na viwanda vingine ambapo napo tumetenga takriban futi za ujazo 3.65 ili ziweze kujenga viwanda. Vile vile tunategemea Watanzania baadaye wasiendelee kukata kuni na kutumia mkaa itumike gesi hii kwa matumizi ya nyumbani ambako nako tumetenga futi za ujazi 1.2 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na katika magari.

Mheshimiwa Spika, leo nimeleta gari linalotumia gesi. Kama ingewezekana kukanyaga ukumbini, ningependa sana likanyage mkaliona lakini kwa Waheshimiwa ya Wabunge na kwa ruhusa yako mara baada ya Bunge hili liko pale nje, Wabunge mnaruhusiwa kutazama muangalie miundombinu kwenye gari inavyotumia gesi. Lipo gari tumelileta kama mfano muone yanavyotumia gesi ambapo kwa sasa tuna magari zaidi ya 200 yanayotumia gesi kutoka magari 80 mwaka juzi, napo tunasonga mbele. Najaribu kuonesha matumizi ya rasilimali ya gesi ambayo wengi wanadhani inasahaulika, hata kidogo! Tunakwenda kuitumia kwa usahihi na usawa ule ule.

Mheshimiwa Spika, matumizi mengine katika gesi naendelea kupambanua kidogo kwa ruhusa yako. Gesi hii tunataka tuwe na viwanda vya vyuma, tutakuwa na ujenzi mwingi sana kwenye ujenzi vya uchumi wa viwanda ambavyo tumetenga futi za ujazo trilioni 1.1 kwa ajili ya viwanda special vya vyuma na bado sasa tunataka kujenga LNG. LNG Waheshimiwa Wabunge itatumia gesi kwenye mpango wetu, kila mwaka tumetenga gesi tani milioni 10 kila mwezi kwa ajili ya LNG tunayotaka kuijenga na LNG itahitaji gesi nyingi sana. Maana yake Waheshimiwa Wabunge, matumizi ya gesi bado yako pale pale hayajasahaulika kwenye umeme na kwenye masuala mengine.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye umeme, bomba la Madimba, bomba hili linaendelea kutumia gesi hii. Limesemwa kwamba uwezo wa bomba ni mkubwa kuliko mahitaji kwa sasa lakini suala jepesi la kujiuliza hata unapotaka kujenga kiwanja cha ndege, hivi unaogopa kujenga kiwanja kikubwa kwa sababu una ndege moja? Ni afadhali ujenge kiwanja kikubwa utakaponunua ndege 100 zitatua pale. Nataka nilieleze Bunge lako Tukufu, bomba hili kwa sasa hivi na nimshukuru Mheshimiwa CAG wakati anakagua mwaka jana alisema matumizi yake ni asilimia sita ya gesi lakini mpaka sasa nataka niwaambie Waheshimiwa kupitia Bunge lako Tukufu mpaka sasa hivi matumizi ya gesi wala sio asilimia sita, imeshavuka! Imeshafika asilimia 16 na bado tunakwenda na hapa tumefungua tu mradi wa Kinyerezi namba II mwaka jana wenye megawatts 248.

Mheshimiwa Spika, tutaongeza megawatts 185 mwezi Agosti mwaka huu tutakapokamilisha Kinyerezi Na.I extension. Tutaongeza gesi nyingine kwenye kutumia, kwa sasa hivi gesi tunayotumia kwa siku ni milioni 120 milioni futi za ujazo kwa siku. Kwa hiyo gesi inaendelea kuingia kwenye kuzalisha umeme. Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba pamoja na kutumia Mradi huu wa Mto Rufiji, bado matumizi ya umeme mchanganyiko ikiwemo gesi tunaendelea kuitumia.

Mheshimiwa Spika, tuna miradi mitatu mikubwa ya kuzalisha gesi katika umeme ikiwemo Kinyerezi I, Kinyerezi III yenye jumla ya megawatts 600 lakini tutaanza kwa awamu na megawatts 300 kwa phase one na phase two. Tuna Mradi wa Mtwara ambao tunaanza kuutekeleza mwakani nao wa megawatts 300 wa gesi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na ndugu Watanzania, matumizi ya gesi bado yapo pale pale. Nilikuwa najaribu kuwaondoa wasiwasi Watanzania kwamba kutumia maji katika kuzalisha umeme kwamba tunasahau matumizi ya gesi, la hasha hata kidogo, Mheshimiwa Rais yuko makini, Watanzania tuko makini, Waziri anayeongea yuko makini na Wabunge wako makini, tunaomba mtuamini. Hiyo ni hoja ya kwanza ambayo ningependa nichangie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, umeme wa upepo. Imeelezwa hapa kwamba katika Mabunge yaliyopita tulieleza nia yetu ya kuzalisha umeme wa upepo kwa haraka haraka, lakini nataka niwaeleze wachangiaji, nimeeleza gharama za kuzalisha umeme kwa upepo, solar na kadhalika lakini katika miradi ambayo tulitaka tuitekeleze ukiwemo Mradi wa Singida na Same kupitia Geo Wind na Wind East Africa wazalishaji hawa walitaka tununue umeme kutoka kwao kwa senti za Marekani 13 kwa unit, jambo ambalo tungefanya hivyo tungeingiza mzigo mkubwa sana kwa Watanzania kupitia TANESCO kwa kununua umeme huo.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa niaba ya Watanzania ni afadhali tuchelewe lakini tuhakikishe safari yetu tutafika salama kuliko kuwahi ukaenda kuishia korongoni. Tungetekeleza miradi hiyo tulikuwa tunakwenda kuwaangamiza Watanzania. Tulichofanya kwanza ni kuanza kupitia upya hizo bei za Watanzania kutakiwa TANESCO kununua, EWURA wamekamilisha, tunakwenda sasa kuzalisha umeme huo kwa bei pungufu ili kusudi TANESCO wakiununua Watanzania wanunuaji wasibebeshwe mzigo.

Mheshimiwa Spika, baada ya mapitio hayo ndiyo maana imetuchukua muda, kwa sasa hivi tutakwenda kama mzalishaji yuko tayari ndiyo maana tumetangaza Novemba mwaka uliopita kwamba kama kuna mzalishaji binafsi na tunawataka sana wazalishaji binafsi tunachotaka ni umakini wa masharti aje badala ya kuendelea na kujadiliana, majadiliano yasiyoisha muda wake. Tumeweka viwango kwamba mzalishaji wa umeme wa upepo kama yuko tayari kutuuzia unit moja kwa senti saba za Marekani na kushuka chini, huyo aje! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa makaa ya mawe, kama yuko tayari kutuuzia kwa dola senti sita huyo aje. Kwa solar kama anataka kutuuzia kwa dola senti tano huyo aje ili TANESCO wakiununua umeme huo atakuuzia wewe mlaji kwa bei ya chini. Tungenunua kwa bei ya senti 13 kama baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanashabikia tukimbilie tulikuwa tunakwenda kuishia korongoni. Kwa niaba ya Watanzania, kama Waziri niliyepewa dhamana, tutakuwa makini katika hili ili kutowabebesha mzigo Watanzania ambao ni wapiga kura wetu.

Mheshimiwa Spika, nimelieleza vya kutosha kwa nini hatukukimbia kuutekeleza, lakini tunakwenda kuutekeleza lakini tunakwenda kutekeleza kwa utekelezaji makini kwani Serikali iko makini, tutaifanya hivyo kwa niaba ya manufaa ya Tanzania. Hapo nimejibu suala la upepo kwa nini hatukutaka kufanya hivyo kwa sababu kuna watu walitaka tutoe maelezo.

Mheshimiwa Spika, hasara kwa TANESCO, hivi hasara ni kitu gani? Kwanza TANESCO imepata mizigo mikubwa sana huko nyuma. Kama ni hasara ziko sababu zilizochangia hasara kwa TANESCO. Sababu ya kwanza kubwa tulikuwa na miradi mikubwa ya kukodi mitambo, mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme wa mafuta mazito na ninyi wengi tunaifahamu Waheshimiwa Wabunge. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, Mabunge yaliyopita na Serikali zilizopita kwa kupiga kelele ili Serikali iachane na ununuzi wa mafuta mazito kuzalisha umeme ikiwemo mtambo wa IPTL, Aggreko, Symbion na mitambo mingine, kwa nini nasema hivyo? Tulikuwa tunalipa capacity charges kila mwaka, zaidi ya shilingi bilioni 635 kwa kampuni moja kuilipa kwenye mtambo mmoja. Hili lilikuwa ni zigo kwa TANESCO, hilo tumeachana nalo tangu mwaka juzi, kwa hiyo, hasara zinakwenda zinapungua.

Mheshimiwa Spika, la pili, viko vituo vingi, ukienda Madaba tulikuwa tunatumia mafuta, Ludewa mafuta, Songea mafuta, Mbinga mafuta, Kigoma mafuta, Loliondo mafuta, Mwanza Nyakato mafuta; na mafuta hayo, natoa mfano, Ludewa tu ulikuwa unaweza kununua mafuta ya shilingi bilioni 703, lakini ukiuza umeme unachovuna ni bilioni 331, hiyo ni hasara.

Mheshimiwa Spika, tulichofanya ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme mkubwa, ili nchi nzima tuiunganishe kwenye gridi ya taifa tuachana na hiyo mitambo.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, mwezi juzi alizindua mradi mkubwa sana wa Makambako-Songea, ambao umetuokolea takribani shilingi bilioni 9.8 tulizokuwa tunanunua mafuta kwa ajili ya kuzalisha umemem na kuwasambazia Watanzania. Hizi zilikuwa ni hasara kwa TANESCO ndugu zangu, sasa tumeachana nazo. kwa hiyo zilikuwepo na mkakati ndiyo hiyo ninayoisema (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine ndugu zangu, TANESCO ilikuwa inaleta nguzo kutoka South Africa, ilikuwa inanunua luku za mita kutoka China, turansformar kutoka India, nyaya kutoka nje. Mwaka jana tumepambana na hili, tumesema lazima tujenge viwanda vya ndani, na njia pekee kwa vile vifaa vinavyopatikana nchini ni kusitisha uingizwaji wa vifaa hivi na kuliokolea gharama shirika letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge mliounga mkono jambo hili, wapo lililowaumiza, nafahamu, lakini tunasonga mbele kwa kuokoa gharama na hasara kwa shirika letu. Maana yake nini, tulikuwa tunaweza kununua nguzo moja mpaka kwa shilingi laki nne kwa fedha ya Tanzania. Nguzo kuitoa South Africa na inawezakana hiyo hiyo inazunguka inarudi, bado unatakiwa ui-clear bandarini. Suala siyo gharama tu, hata muda. Sasa hivi unaweza ukakimbia hapa Mafinga ukanunua nguzo moja kwa shilingi 80, ni kiasi gani shirika linaokoa gharama hiyo? Hizo zote zilikuwa ni hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa summary yake, mpaka mwaka juzi shirika lilikuwa na hasara ya shilingi bilioni 349, mwaka jana zimepungua, zimekuwabilioni 122, mwaka huu zinakwisha na kupata faida ya bilioni tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge nataka kusema, nini faida ya sitisho hilo? Kwanza tumeokoa jumla ya shilingi bilioni 162.34 ambazo tumenunua vifaa hivyo, lakini pili tumetengeneza ajira kwa watanzania zaidi ya 3520 kwa ajili ya viwanda hivyo. Kwa hiyo, tulikuwa tuna viwanda vitatu vya nguzo, sasa hivi tuna viwanda tisa, tulikuwa tuna kiwanda kimoja tu cha transformer, tuna viwanda takribani vitano. Tulikuwa tuna kiwanda kimoja cha waya, tuna viwanda sita, tulikuwa hatuna kiwanda hata kimoja cha luku, sasa hivi tuna viwanda vitatu vya luku, ndugu Watanzania naomba tuelewe hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mahitaji yetu ya ndani ya vifaa vyote kwa ujumla wake ni nusu ya uwezo wa viwanda vya ndani kwa sasa vilivyojengwa ndani ya miezi saba hadi sasa, hayo ni mafanikio makubwa, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Suala la Madeni ya TANESCO. Mwezi januari mwaka 2018, ni kweli TANESCO ilikuwa na madeni takribani bilioni 990, lakini sasa hivi inavyolipa yamepungua sana, na inaedelea kuyapunguza, na mkakati wa kumaliza madeni yote kwa shirika hili ni ifikapo mwaka 2026, madeni yote TANSECO itakuwa imeyamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, madeni yake yanapungua limefikia bilioni 957, lakini tumemuomba mhakiki wa Serikali ayahakiki madeni haya. Yako madeni mengine yanabishaniwa na yako madeni mengine wala si halali; ni matumaini yetu yatapungua sana. Katika madeni hayo TPDC kimsingi, ambaye ndiye anayeuza gesi kwa kiasi kikubwa kwa TANESCO ndiye aliyekuwa na madeni makubwa, 480, lakini sasa yameshuka mpaka 340. Kwa sababu sasa hivi TANESCO ina uwezo wa kulipa, badala ya kulipa bilioni saba kwa wiki sasa hivi ina uwezo wa kulipa bilioni tisa kwa wiki, katika madeni ya TPDC.

Nalielezea Shirika la TANESCOkwa ujumla wake jinsi ambavyo sasa hivi limejipambanua. Silitetei kama shirika la umma lakini kwa kwa sababu sasa hivi lina uwezo wa kuwahudumia Watanzania. Zipo changamoto, lakini lina uwezo wa kuwahudumia Watanzania, na tunakokwenda lita- improve zaidi. kwa hiyo nimeona niseme hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa kuhusiana na madeni, kwa vile TANESCO ina uwezo wa kulipa madeni na kwa vile sasa hivi TANESCO haipati ruzuku kutoka Serikalini, tumemwomba Mheshimiwa Rais na ametuelekeza, shirika hili ni kubwa halina haja ya kuombaomba, shida ilikuwa ni usimamizi na sisi tunalisimamia. Kwa hiyo tangu mwaka juzi shirika hili halipati ruzuku kutoka Serikalini, linajiendesha lenyewe. Zaidi ya hapo linapata faida ya ongezeko ya asilimia 1.5 mwaka juzi na mwaka jana ni 7.6. Kama nilivyosema, ni matumaini yetu, kuanzia mwaka huu na miaka inayokuja, shirika la TANESCO litaanza kutoa gawio Serikalini. Hayo ni mafanikio, nilitaka kueleza kwamba pamoja na madeni hayo, lakini jitihada za kuyalipa ni kubwa na ni matumaini yetu yatakwisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme moja katika suala la umeme vijijini. Ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri; mwaka 2008 tulikuwana vijiji 506 vilivyokuwana umeme, 506, mwaka 2015 tulikuwa na vijiji 2018 vilivyokuwa na umeme. Leo hii tunapoongea umeme vijijini tumeunganisha vijiji 7127, tunapoongea hapa. Mradi unapotekelezwa tunajua kunakuwa na changamoto nyingi sana. Mradi huu utakwisha mwezi juni mwakani, ni matumaini yetu utakapokamilika mwezi juni mwakani, utafikisha vijiji 10,128 vyenye umeme, sawa na asilimia 84 na tutabakiza vijiji 1990 katika ya vijiji 12,268. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Watanzania, sisi kwa sasa ndiyo vinara, ndio tunaoongoza kwa nchi ya Afrika Mashariki kutandaza umeme vijijini kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wakenya pamoja na kuwa na umeme wa MW 2,003, lakini wana asilimia chini ya 43 kupeleka umeme vijijini. Waganda, mpaka wametuomba tupeleke vijiji sita vya mfano nchini kwao ili nao waone umeme vijijini, na tumewapelekea vijiji vya mpakani, vikiwemo Nangoma pamoja na Umurushenya, tutaendelea kuwapelekea. Huu ni mfano kwa nchi yetu inavyopiga hatua.

Mheshimiwa Spika, lakini zipo changamoto katika suala hili; moja ya changamoto katika maeneo haya kwanza ni uelewa, kwamba hauwezi ukawa wa pamoja kwa wakati mfupi. Kazi yetu ni kuendelea kuwaelewesha wananchi na washirika wengine ili kusudi tuutekeleze mradi huu kama ilivyodhamiliwa.

Mheshimiwa Spika, lakini niwapongeze Waheshimiwa Wabunge, mnatupa ushirikiano mkubwa sana katika kupeleka umeme vijijini, nawapongeza sana sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi napenda niseme shukrani mlizotupa katika kupiga hatua kwenye umeme vijijini naomba ziwarudie Waheshimiwa Wabunge, mmefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tutaendelea kutoa ushirikiano ili tupeleke umeme katika vijiji vyote. Lipo jambo lilizungumzwa hapa, kwamba viko vijiji 55 kwamba vilikuwa hewa. Nataka niseme, kwenye miradi hii mikubwa changamoto zipo; lakini kubwa, hata Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, unaweza ukakuta kijiji kina vitongozi saba, lakini kati ya vitongoji saba ni kitongoji kimoja ndicho kimepelekewa umeme. Swali la kujiuliza, vitongoji vingine tuviache kwa sababu tulishapeleka kitongoji kimoja cha kijiji kile? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini unapopelekea umeme, hukiiti kitongoji, unaita kwa jina la kijiji. Kwa hiyo mnakuta majina mengine yamerudiwa hata zaidi ya 100, lakini tunapokwenda kule la kwanza ni kufanya survey ili kuona ni sehemu gani ya kijiji kilichopelekewa umeme, hakina, ndipo eneo hilo lipelekewe umeme. Nimeona nitoe ufafanuzi katika jambo hilo na kama kuna mahala ambapo kuna kuwa na oversight lazima tufanye replacement na tunafanya hivyo kwa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nichukue nafasi hii kusema kwamba utekelezaji wa miradi hii tutaendelea kufanya usanifu ili kuwa na usahihi wa kutosha. Hata hivyo, tuko tayari kupokea mawazo na ushauri wa Wheshimiwa Wabunge ili tuweze kufanya marekebisho ya kuimarisha kazi hii.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, ningependa sana niseme, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania; ni kweli tunapopeleka umeme vijijini maeneo ya taasisi yanasahaulika sana, na ni changamoto si tu kwa shirika na kwa mkandarasi hata wasimamizi wa taasisi hizo. Nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge watusaidie kupitia wenyeviti wa halamshauri na wakurugenzi, maeneo yote ya taasisi ambayo yako kwenye vijiji vyenye umeme, niombe sana yalipiwe ili taasisi zote za umeme ziendelee kuunganishiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, iko changamoto ya Waheshimiwa Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri kuilalamikia Serikali, kwamba Kituo changu cha Afya hakina umeme, Zahanati haina umeme, shule haina umeme, lakini sababu haijalipiwa. Niwaombe sasa tutumie nafasi hii tulalamike tukiwa tumeshafanya malipo. Nami nitumie nafasi hii kuelekeza Shirika la Umeme TANESCO pamoja na wakandarasi popote watakapoona taasisi ya umma, iwe kilomita 100, iwe kilomita tano, ipelekeeni umeme, ili mradi pamelipiwa. Waheshimiwa Wabunge nimeeleza kwa msisitizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie, nitoe maelekezo kwa wakandarasi, Shirika la Umeme TANESCO na wadauwengine wanaosambaza umeme, kwa niaba ya Serikali, popote pale, taasisi ya umme itakapokuwa, kutoka kwenye kijiji chenye umeme au eneo lenye umeme, iwe kilomita 100, iwe kilomita 20, iwe kilomita mbili, pelekeni umeme kwenye taasisi hiyo ili mradi imelipiwa gharama zake, nadhani limekaa sawa, elfu ishirini na saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali ya awamu ya tano, na mimi nilisema niliposimama kwenye Bunge lako Tukufu, awamu iliyopita mwaka uliopita, nilieleza kwamba tutapeleka umeme mpaka kwenye nyumba za matembe. Watu walikuwa wanadhani tunatania, mpaka kwenye nyumba za makuti, walikuwa wanadhani tunatania, tuko seriousna jambo hili. Nyumba yoyoye ya mtanzania, mtanzania anamuishi, ndimo humo humo tutampelekea umeme, humo humo tutampelekea umeme. Atakapohama nasi tutapeleka umeme atakakoelekea,tunajali maisha ya watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elfu 27 lengo lake ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata umeme. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa maelekezo mazuri, kwa kujali Watanzania wa maisha ya kawaida. Tumefanya maamuzi, kupitia Bodi ya Shirika letu la TANESCO, kwamba umeme unaopelekwa vijijini, uwe wa REA, uwe unaopelekwa na TANESCO, ili mradi unapelekwa vijijini, kuanzia Mei mosi mwaka huu kuunganishwa umeme ni elfu 27 tu, basi. Iwe TANESCO, iwe REA, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, tukatoe elimu hii na mimi nimesimama hapa kupitia Bunge lako Tukufu, Watanzania wote wanisikie, wandarasi wote wanisikie, TANESCO wanisikie, Wabunge mnisikie, na mimi najisikia hivyo, gharama ni elfu ishirini na saba (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala secular lilishatoka na Waheshimiwa Wabunge mtapewa.

SPIKA: Hebu liweke vizuri, Mheshimiwa Waziri, hapo kwenye 27 hebu irudia tenaili Wabunge waondoke nayo vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba nirudie kwa ruhusa yako. Kuanzia tarehe moja, Mei mwaka huu kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), bodi imepitisha na secular ilishatoka na imeshaanza kufanya kazi, gharama ya kuunganisha umeme katika maeneo yote ya vijijini; iwe unapelekwa na REA, iwe unapelekwa na TANESCO, au yeyote aliyepewa kazi na Serikali, gharama ni elfu ishirini na saba tu basi. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwa heshima ya Bunge lako, nitoe maelekezo kwa mameneja wote wa kanda, mikoa, wilaya, wa TANESCO na Makao Makuu, walisimamie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Niendelee, Kukatika kwa Umeme. Katika maeneo ambayo pia tumeimarisha sana ni pamoja na eneo hili. Pamoja na kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo, Serikali inachukua hatua za maksudi sana kuhakikisha kwamba jambo hili halijitokezi sana. Katika maeneo ya Dar es Salaam, nitoe taarifa kwa wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania, shida inayotokea sasa hivi tulipata break-down ya engine moja, lakini Serikalikupitia kwa Mheshimiwa Rais wetu, tumeleta mashine ya MW 240 ambayo inafungwa sasa hivi kwa Dar es Salaam, ambayo ni matumaini yetu, ndani ya mwezi mmoja itakamilika. Kwa hiyo, maeneo yote ya Dar es Salaam na watanzani kwa sababu inajengwa kwenye gridi ya taifa, umeme utakuwa ni wa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Watanzania waendelee kuvumilia, kwa sababu ziko changamoto nyingi, lakini matumaini yetu umeme utakwenda kuimarika na kukatika itapungua sana.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu LNG. Mradi wa LNG umeelezwa sana, na mimi ningependa kurudia. Dhamira ya kutekeleza mradi huu iko palepale. Mradi waLNG utatekelezwa, nimetaja gesi tuliyotenga na hatua tuliyofikia sasa hivi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Nape na Wabunge wengine wa Lindi, tuliokuwa nao hivi juzi katika semina tuliyoifanya. Tumekutana na wadau, tumekutana na wawekezaji pamoja na Serikali, tumekubaliana, majadiliano yataongeza speed. Ni matumaini yetu watamaliza mapema, ikiwezekana mwakani, ili utekelezaji uanze kufanyika na ujenzi utaanza miaka mitano ijayo na huu mradi utachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumetenga mpaka fedha kwa ajili ya kufidia wananchi ambao wataathirika na mradi huu. Hii ni kuonyesha commitment ya Serikali kwa lengo la kuutekeleza mradi huu. Niseme tu kwamba ndugu zangu wananchi wa Lindi na Watanzania wote mradi hu ni mkubwa, tumeupa kipaumbele na utatekelezwa bila kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala kurudiwa mikataba hapa, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza. Iko mikataba ya rasilimali ya gesi, nikopongeze Mheshimiwa Spika, mwaka jana uliunda Tume Maalumu, kwa ajili ya kufuatilia na kukagua umuhimu, dosari na changamoto za mikataba hiyo. Nitoe shukurani sana kwako na kamati iliyofanya kazi hiyo; lakini nirudie kusema, Serikali inachukua hatua madhubuti sana.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameshanza zoezi hili, ni matumaini yetu litakamilika. Lakini lengo letu kubwa, maama liko jambo limezungumzwa, la kutotoa leseni; lengo letu kubwa, ipo hatari ya kutoa leseni kwenye masharti ambayo ni hasi kwa Watanzania. Tunataka tujiridhishe, kuondoa wasiwasi, kwamba masharti yatakayoingiwa yatakuwa ni sahihi na bora kwa Watanzania baada ya mikataba hii kupitiwa vizuri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, chukua muda kwa umakini, fanya kazi kwa umakini, toa kitu cha makini, tufanye kazi ambayo itakuwa na tija kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Usambazaji wa Gesi Majumbani. Tumeeleza katika taarifa yetu. Bila shaka katika eneo hili, kati ya maeneo ambayo watanzania watakumbuka sana utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ni pamoja na kutekeleza miradi ya kusambaza gesi majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisirudie hasara ya mkaa pamoja na mambo mengine yanavyofanyika, lakini ni kubebesha mzigo kwa Watanzania. Watanzania wengi kwa sasa hivi, wengine unaweza kukuta wanakula mlo mmoja kwa sababu ya kuogopa gharama ya matumizi ya kupikia. Mradi huu utaokoa gharama kwa kiasi kikubwa. Mradi huu tumeanza kuutekeleza maeneo ya Dar es Salaam, tumeshaunga wateja zaidi ya 200 na yako maeneo mengi kwa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na mikondo minne, mkondo wa kwanza wa kupeleka gesi ni ule unaotoka Ubungo, kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam- Mlalakua mpaka Tegeta; mkondo wa pili unakwenda mpaka Mikocheni, mkondo wa tatu unakwenda mpaka Keko na mkondo wa nne unakwenda mpaka maeneo ya Chanika. Kwa hiyo ni matumaini yetu baada ya kusambaza vizuri gesi hii Watanzania, hasa wananchi wa Dar es Salaam watatumia gesi hii kupunguza ukakasi wa maisha.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili muhimu, tulichoanza kufanya, gesi kwa sasa hivi, ambayo tumeanza kuisambaza, ina punguzo la asilimia 40 ya gharama ya matumizi ya kawaida ya sasa hivi ya gesi asilia. Kwa sababu mitungi inayokuja kwa sasa wananchi wanalipa zaidi ya shilingi 50 na 57,000, lakini kwa matumizi ya gesi hii wanayounganishiwa, gharama yake itakuwa ni chini kwa asilimia 40 ya bei na gharama hiyo ya mitungi ya sasa.

Mheshimiwa Spika, vilevile wananchi wanatumia mkaa, nimetaja hasa mkaa wa kilo 100, utakuwa na punguzo si chini ya asilimia 35 mpaka 45. Kwa hiyo, utawapunguzia ugumu na ukakasi wa masiha wananchi kwa ajili ya kutumia rasilimali hii.

Mheshimiwa Spika, Umeme wa Grid Kigoma na Katavi. Yako maeneo tunakubali, kwamba Serikali bado inayafanyia kazi. Tumeanza kutekeleza, tuna miradi miwili, mradi wa kwanza ni wa kupeleka umeme mkubwa wa kV 400, kutoka Iringa kupita Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga. Utekelezaji wa mradi huu umeshaanza, umbali wa kilometa 624. Pia tuna eneo la kutoka Sumbawanga - Mpanda - Kigoma hadi Nyakanazi. Utekelezaji wa eneo hili sehemu yake bado na tunaendelea na majadiliano kupata wawekezaji ili tuanze kuutekeleza. Tumeona tuanze kupeleka umeme mwingine kutoka Nyakanazi kupita Kigoma hadi Geita, utekelezaji wake umeanza.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kunusuru Kigoma kwa sasa kwa haraka, ni huu mradi wa kuusafirisha umeme wa kV 132 kuutoa Tabora kupitia Urambo kwenda Nguruka hadi Kidahwe, umbali wa kilometa 391, utekelezaji umeanza na matumaini yetu kwamba tunaweza kukamilisha ifikapo juni mwakani. Kwa hiyo, wananchi wa Kigoma, katika eneo hili wawe na matumaini kwamba nao wataacha kutumia mafuta mazito na kuwapunguzia gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Katavi, tutachukua umeme kutoka Tabora vilevile utapita Ipole kwenda Inyonga mpaka Nsimbo umbali wa kilometa 383. Utekelezaji unaenda sambamba na Mradi wa Kigoma. Miradi yote miwili itagharibu takribani dola za Marekani milioni 92.8. Utekelezaji wa miradi hii ni muhimu sana kuutaja ili pembe zote nne za nchi yetu ziweze kupata umeme wa gridi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Rukwa ni kweli yako maeneo ambayo hayana gridi kwa sasa tunachukua gridi kutoka Zambia takribani megawati nane lakini yako maeneo tutatoa umeme kutoka maeneo ya Kigoma kupeleka Katavi hadi Rukwa wakati tunakamilisha Mradi mkubwa wa Sumbawanga hadi Nyakanazi.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge pamoja na kueleza maeneo hayo, lakini ningependa pia nizungumzie huu Mradi wa Bomba la Mafuta. Hivi sasa tumeanza kutekeleza Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda, tunafahamu kwamba imechukua hatua kufikia hadi sasa, lakini napenda kutoa taarifa tu katika Bunge lako Tukufu kwamba, mradi huu tunaendelea vizuri. Hivi sasa tuko katika hatua za mwisho kabisa za kumaliza majadiliano na majadiliano yakikamilika hatua inayofuata ni kuanza ujenzi. Nimpongeze sana Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi wiki iliyopita ameshafanya semina kwa ajili ya tathmini ya wananchi watakaopisha miradi wakati wa ujenzi.

Mheshimiwa Spika, wakati tunafanya majadiliano hatua za awali za ujenzi zimeshaanza, kwa sasa tunachofanya ni kufanya maandalizi ya kupata ardhi kwa ajili ya ujenzi wa bomba, maandalizi ya kulipa fidia na kwa ajili ya kujenga vituo 16 vitakavyopitiwa na mradi huu. Hatua hii ni kubwa, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huu na ningependa nitoe taarifa kwamba utekelezaji wa mradi huu bado uko pale pale na tumepanga utakamilika ifikapo mwaka 2023, kwa sababu kwa sasa umechelewa kidogo, lakini muda wa kuutekeleza ni uleule, miezi 36.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza hapa, nilizungumza suala la IFAD watekeleze wataalam wetu, Huyo IFAD alikuwa ni Mkandarasi ambaye ni Consultant ambaye alikuwa anasimamia miradi ya ujenzi wa backbone, ilikuwa kuna hoja kwamba amefanyiwa malipo ya ziada ya milioni 97. Napenda kulieza Bunge Tukufu jambo hilo kwanza lishakuwa close na Mheshimiwa CAG na wala siyo jambo la kujadili kwa sababu alishalipa kulingana na makato ambayo yalifanywa kulingana na mkataba wake. Kwa hiyo jambo hili napenda tu nimweleze Mheshimiwa Mbunge aliyekuwa anataka kujua usahihi wa jambo hili kuwa usahihi wenyewe uko katika hali hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza kwa sasa ambalo ni vema sana niwaambie Watanzania ni makusanyo na mapato ya shirika letu. Si kwamba narudia naeleza eneo dogo na sehemu niliyokwishaeleza kwa sasa Shirika la Umeme (TANESCO) wako wananchi na baadhi ya watu wanasema ligawanywe, ningependa kuchukua nafasi hii kuwaeleza Watanzania kwamba jamani umeme ni usalama, umeme ni biashara, umeme ni uchumi, sipingani na wanaosema shirika ligawanywe, lakini ningependa sana tuwe makini katika kuchukua hatua za kulimega shirika hili kabla hatujafanya hivyo. Kwa nini nasema hivyo? Ukisema uzalishaji ufanywe na mtu binafsi na amiliki mitambo ya kuzalisha maana yake atakuwa na mamlaka ya kusema leo nazima umeme nakarabati nchi nzima, matokeo yake nchi mnaweza mkaingia gizani, hilo ni jambo mahususi Watanzania tulielewe tunaweza tukaligawa lakini lazima tuwe makini katika kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, katika usambazaji, ni matumaini yangu kama tutaipatia shirika na bahati mbaya ikiwa ni shirika binafsi lisambaze umeme mpaka vijijini ni mashirika machache na wengi wameshajaribu na kushindwa, yatakayoweza kufanya hivyo, matokeo yake watapenda kupata faida kubwa na Watanzania wengi uwezo wao ni mdogo jambo la msingi hapa kitakachokuwa Watanzania watashindwa kumudu na hivyo azma ya Serikali ya kupeleka umeme nchi nzima itashindikana. Ningependa kutoa wito Watanzania tutoe maoni namna bora ya kulifanya shirika letu liimarike zaidi badala ya kuligawa vipande vipande. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru ulipokuwa unazungumza umeme mchanganyiko, mtu akasema kuna umeme solar muhimu sana kuweko kwenye gridi ya Taifa, ulimjibu mpaka nikasema kumbe Mheshimiwa Spika ni mwanasayansi. Unaweza ukatumia ukaweka umeme wa upepo kwenye gridi ya Taifa megawati 1,000, umeme wa upepo megawati 1,000, lakini umeme wa solar unategemea jua.

Kwa hiyo siku jua limeshuka utakosa megawati 1,000, siku jua limeshuka na inategemea na mpango mkakati, hili jambo lazima lielezwe kwa sayansi sana, namwona sana Mheshimiwa Heche anataka kuamka lakini ajiandae na ufafanuzi wa kisayansi.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema hapa katika gridi ya Taifa standard katika kataifa yote umeme wa renewable kwenye absorption ya umeme haitakiwi azidi asilimia 15, kwa sababu ya kuogopa risk. Kwa hiyo kama tuna megawati 1,600 tunatakiwa tuingize umeme wa renewable walau asilimia tano mpaka 15 ikizidi hapo unaiweka nchi katika hatari ya kukosa umeme itakapotokea dharura hiyo. Napenda niseme na kupongeza kwa argument hiyo, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, umeme wa upepo kulingana na stadi tulizonazo speed maana potential tuliyonayo kwenye umeme wa upepo ni speed ya upepo, speed ya upepo tuliyonayo kwa sasa hivi ni speed ya kuanzia 4.5 meter per second mpaka meter 9.0 per second. Kwa hiyo ikipungua speed maana yake unakosa umeme wa upepo vilevile, haya ni masuala ya kisayansi sana, lakini napenda niyaseme kwa maana ya uelewa Waheshimiwa Wabunge. Kubwa unapokuwa na umeme mchanganyiko na hasa unapokuwa na umeme mwingi wa maji gharama yako itakwenda kupungua. Wenzetu wa Misri ambao wana umeme zaidi ya megawati 4,000 wa maji ndiyo maana bei yao iko chini ya dola 4.6 dola za Marekani, sisi yetu iko juu kwa sababu tumetumia pia gharama kubwa kwenye ku- compute gharama za umeme na kwa sababu hatujazalisha umeme mwingi wa maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo napenda kutumia nafasi hii kurudia tu kusema kutumia umeme wa maji, kutumia umeme wa gesi, kutumia umeme wa makaa ya mawe ni muhimu sana, lakini yako mambo mawili ya kuzingatia kwanza gharama ya kuijenga mtambo huo na ya pili gharama ya kuwauzia wateja walaji wa mwisho utakapokamilika mradi huo. Ndiyo maana tunasema mara baada ya miradi hii kukamilika na masuala mengine yanayoendelea, ni matumaini yetu kwa Serikali yetu makini inakwenda kutazama upya bei kwa gharama za umeme ili kuwapunguzia mzigo Watanzania ambao tunatumia kodi yao kuzalisha umeme huu kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliyotaka kueleza ya msingi nimeyaeleza, sasa ningependa nitumie nafasi hii kwa niaba yako na Waheshimiwa Wabunge nishukuru kwa michango yao, kuna mengi ya kusema mengine tutaendelea kuyaeleza na kwa sababu hiyo mengine tutayaeleza kwa maandishi tutaleta ufafanuzi kwenye Bunge lako tukufu na mengi tumeomba yaiingie kwenye Hansard.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.