Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili kwa mara ya pili ili niweze kuchangia hoja ya Wizara yetu ya Nishati na nianze kusema naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, pia napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ya pekee kwa miongozo yake na kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika sekta hii ya Nishati. Namshukuru pia Makama wa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mheshimiwa Chief Whip wetu kwa maelekezo mbalimbali anayoyatoa ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, nikushuruku wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge pamoja na Kamati yetu ya Nishati na Madini kwa miongozo mbalimbali mnayotoa katika sekta yetu ya nishati. Kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa namna ambavyo anaongoza Wizara yetu na kazi nzuri anayoifanya nchi nzima kwa weledi, uaminifu na kipaji ambacho alicho nacho na nimtakie kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru familia yangu, mume wangu Juma Mtemvu, wazazi wangu, watoto wangu na familia yote Vilevile nikishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi pamoja na Wajumbe wa UWT, Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wetu wa Serikali katika mkoa huu na wanachama kwa namna ambavyo wananipa ushirikiano katika majukumu yangu ya Unaibu Waziri lakini pia ya Kibunge ndani ya Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Wabunge wa Bunge hili kwa namna ambavyo wamechangia hoja yetu na mashirikiano wanayotupa siku zote, kwa ushauri wao na maelekezo ya mara kwa mara; kwa kweli wameitendea haki hoja yetu. Takribani Wabunge 100 wamechangia, 50 wamechangia kwa maandishi na wengine 50 wamechangia kwa kuzungumza.

Mheshimiwa Spika, umenipa dakika 15 lakini nataka niseme yote yaliyojadiliwa ndani ya Bunge lako tukufu tumeyapokea, na kwa kuwa majibu yatakuwa ya kimaandishi kwa kila mmoja hoja yake aliyochangia itoshe tu nichangie kwa ujumla wake na kama nilivyotanguliza kusema kwamba nimewashukuru sana. Mjadala wetu huu leo ulijielekeza kwenye suala zima la masuala ya Nishati na hususan asilimia 80 ya waliochangia walijielekeza kwenye mradi wa REA. Mradi wa REA awamu ya tatu ambao umelenga kufikisha vijiji vyote umeme takribani 12,268 ifikapo 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, tumesikia changamoto, tumesikia mlivyotuelekeza, tumesikia namna gani Watanzania wanahitaji nishati hii ifike vijijini. Tumepokea pongenzi; lakini siku zote nasema anayekupongeza anahitaji zaidi. Pongezi mlizozitoa leo mnahitaji tufanye kazi zaidi tuyafikie maeneo mbalimbali, tufikie vijiji vyote 12,068 ili kuweza kuleta tija na tuwaunganishie vijiji vyote. Ila nataka niseme moja, kwamba mradi huu kwa kweli wa REA awamu ya tatu pamoja na hoja kwamba umechelewa. Tumeshawa-categorize wakandarasi, tunatambua wakandarasi ambao wanafanya vizuri na tunatambua wakandarasi ambao bado kasi yao haijawa nzuri. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu, kwamba tunavyopima mradi huu wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na miradi mingine inayoendelea tupime baada ya kuwafungulia letter of credit, ambayo ilikuwa mwezi wa sita mwaka jana 2018.

Mheshimiwa Spika, kwa miezi 24 wa mradi huu, matarijio yetu mradi huu utakamilika Juni, 2020. Kwa kuwa ndani ya Bunge hili na asilimia kubwa ya maswali ninayoyajibu pamoja na Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani yanahusu masuala ya nishati vijijini. Tumeweza kuwahamasisha na kuwasimamia wakandarasi, na hii tunawaahidi wakamilishe mradi ifikapo Desemba, 2019 ili miezi sita inayosalia iwe miezi ya kuunganisha wateja na ya kurekebisha mapungufu mbalimbali. Kwa hiyo niwatoe hofu Wabunge wote waliochangia hoja hii, kwamba pamoja na Watendaji wetu ambao wanafanya kazi vizuri wakiongozwa na Dkt. Khamis Mwinyimvua na Wenyeviti wetu wote wa Bodi zetu hizi. Kwa kweli jambo hili litawezekana na tuahidi tu kwamba itawezekana.

Mheshimiwa Spika, la pili, tumesikiliza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hotuba hii ilionesha kwamba hakuna jambo lolote ambalo limefanyika; tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani hakuna mradi wowote uliokamilika. Pamoja na kuchangia kwangu, nitaomba mwongozo wako ni nini kifanyike inapotokea hotuba yenye nia ya kupotosha na kulipotosha Bunge lako. Kwanini nasema hivyo, tumesema kwenye taarifa yetu tangu Serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani kwanza kiwango cha uzalishaji wa umeme kimeongezeka. Sasa hivi tuna Mega Watt takribani 1,604 kutoka Mega Watt 1,200 za mwaka 2015. Vilevile tumesema mradi wa Kinyerezi II Extension ulioanza awamu hii ambao umezalisha Mega Watt zaidi ya 244 umekamilika. (Mkofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, mradi wa Makambako - Songea wa KV 220 umezinduliwa, umekamilika. Kana kwamba haitoshi mradi wa kusafirisha umeme wa Iringa – Shinyanga KV 400 umezinduliwa umekamilika. Pamoja na miradi mbalimbali ambayo tumeisema na tumesema, kwamba sasa tunakuwa na Megawatt 300 za ziada tofauti na upungufu wa Mega Watt 100 mwaka 2015. Kwa hiyo ni wazi kabisa Serikali ya Awamu ya Tano imetenda katika kipindi hiki kifupi cha miaka hii mitatu.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa pia utolee mwongozo wako ni suala zima la Taarifa ya Kambi ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuonesha kwamba Serikali inaikwamisha sekta ya nishati na tathmini na namna ambavyo amekuwa amefanya analysis, inashangaza. Nimshauri Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Waziri Kivuli pengine wakati anaandaa taarifa yake ahusishe na watu wa fani nyingine. Kwa sababu utaona namna ambavyo amekuwa anafanya analysis hususan ya fedha zilizopelekwa kwenye Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amelipotosha Bunge lako Tukufu. Utaona katika analysis yake aliyoifanya kwa mfano ya mwaka 2015/2016 ameishia Desemba, 2015. Wote tunafahamu mwaka wa fedha wa Serikali unaishia tarehe 30 Juni, hii inafahamika. Unapofanya tathmini ya kuonesha Desemba 2015 unakuwa na hoja binafsi na si hoja ya kulipa uelewa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nataka niitaarifu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa mwaka 2015/2016 Wakala wa Nishati Vijijini ilipokea bilioni mia mbili tisini na tano na arobaini ikiwa ni asilimia 81 ya fedha zilizotengwa. 2016/ 2017 ilipokea bilioni arobaini mia tano tisini na tano ikiwa ni asilimia 75 iliyotengwa. 2017/2018 ilipokea bilioni mia tatu sabini na nne ponti tano ikiwa ni asilimia 80. Mwaka tunaouzungumza 2018/2019 mpaka sasa na hata taarifa ya Kamati yenyewe ambayo Naibu Waziri Kivuli ni Mjumbe wa Kamati hiyo mpaka sasa REA imepokea asilimia 81. Kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haiiwezeshi REA, isingewezekana kwa kipindi kifupi cha miezi 36 vijiji takribani 5,019 kupelekewa umeme. Kwa hiyo ni wazi kabisa Bunge lako limepotoshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kana kwamba haitishi, Bunge lako pia limepotoshwa kwenye taarifa ya hasara za Shirika la TANESCO. Tumepokea changamoto zote zilizoelewa, lakini hasara za Shirika la TANESCO zimekuwa zikipungua. 2015/ 2016 zilikuwa bilioni 949, 2016/2017 zimekuwa bilioni 265, 2017/ 2018 TANESCO ilipata hasara ya bilioni 112. Kuliaminisha Bunge lako, na kwa kuwa taarifa hii inaingia kwenye hansard, kwamba hasara za TANESCO zikiwa zimeongezeka hususan awamu ya tano, tutaomba mwongozo wako vinginevyo taarifa ambazo za upotoshaji ziondolewe kwenye hansard ya Bunge ili kupata taarifa sahihi. Niko tayari ku-submit audited report za TANESCO kuthibitisha hoja yangu ninayojenga sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hasara hizo lakini TANESCO imekuwa ikiwekeza kwenye fedha zake za ndani, kwenye miradi ya uzalishaji na miradi ya distribution. Mwaka 2015/2016 TANESCO iliwekeza bilioni 205, mwaka 2016/2017 TANESCO iliwekeza bilioni 220, mwaka 2017/2018 TANESCO imewekeza bilioni 233. Tunaona miradi yote hiyo, ujenzi wa sub-stations line ya Mtwara, kituo cha Maumbika ni fedha za ndani ya TANESCO. Ujenzi wa Sub-station maeneo mbalimbali, uunganishaji wa grid ya taifa kwenye maeneo mbalimbali ni fedha za TANESCO.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa suala zima la LNG. Ni kweli, natambua concern za Wabunge kwamba mazungumzo yamechelewa, lakini nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu mazungumzo haya yalikwama baada ya wabia wa mradi huu kutofautiana. Isingewezekana Serikali ikaendelea na mazungumzo ilhali wabia hawa wametofautiana. Hata hivyo pale kila mbia alipotaka tuzungumze pamoja na Serikali ikatoa baraka zake mazungumzo haya yameanza kwa kasi na yanataraji kukamilika Septemba, 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie dakika chache kueleza uzoefu wa mazungumzo. Mfano Canada ilipojenga LNG yao, mazungumzo yalichukua miaka saba (7), Papua New Guinea ilipojenga LNG yao mazungumzo yalichukua miaka minne (4). Sambamba na hilo hata Msumbiji hapa walichukua mazungumzo mwaka mmoja na nusu lakini pamoja na kwamba mazungumzo haya hayakuingiliana kwenye masuala ya mkataba mkataba. Timu yetu hii tumeshaipeleka nje nchi za Indonesia, tumeipeleka Msumbiji, Papua Guinea, Trinidadi and Tobago na Qatar kwa ajili ya kuona namna gani nchi hizi zilifanikiwa wakati wa haya mazungumzo ya LNG. Kama ambavyo Wabunge wa Mkoa wa Lindi wamesema kwa kuwa mazungumzo yameshaanza na kwamba wawekezaji wanaendelea vizuri ni imani yangu mradi huu mkubwa ambao utatumia takribani trilioni 69, utatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuzungumzia mradi wa Rufiji Hydropower, na kwa kuwa natoka Mkoa wa Pwani ni mdau wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imetolewa takwimu hapa, bei ya umeme unaozalishwa na maji ni shilingi 36, bei ya gharama ya umeme unaozalishwa na gesi ni shilingi 147. Mheshimiwa Silinde alitolea mfano kwamba mradi wa Kinyerezi One Extension, bilioni 60 iliyotajwa kwenye kitabu ni fedha za kumalizia. Mradi huu umegharimu Dola za Kimarekani milioni 188 ambapo ni kama bilioni 454. Kutaka kutuaminisha bilioni 60 inaweza kuzalisha Megawatt 150 ni kulipotosha Bunge lako. Hata taarifa yetu ambayo Mheshimiwa Waziri ameisoma, ukurasa wa 34 ilieleza kinaga ubaga kiasi cha fedha iliyotumika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge pamoja na michango yenu mizuri ninaomba michango hiyo ijielekeze kwenye takwimu zinazotolewa, isiwe na nia ya kupotesha, tunajenga nyumba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli tunategemea kufika uchumi wa kati 2025, tunahitaji umeme mwingi zaidi. Mmetaja miradi mbalimbali lakini gesi hiyo katika taarifa yetu hatujaiacha, uko mradi mpya wa kuzalisha Megawatt 300 katika Mkoa wa Mtwara kwa kutumia gesi. Uko mradi pia Kinyerezi IV na VI ambayo inaandaliwa, inaonesha kwamba gesi hatujaiacha na bado tunaimba huo wimbo kwa sababu gesi inatarajiwa kutumika kwenye viwanda, gesi inatarajiwa kutumika kwenye viwanda vya mbolea, gesi inatarajiwa kutumika kwenye kuendesha magari. Kwa hiyo kusema kwamba sasa hivi wimbo hatuimbi, tunaimba wimbo wa umeme wa bei nafuu kwa ajili ya viwanda na kwa ajili ya kushusha bei ya watumiaji wa umeme wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi binafsi namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ujasiri wake. Ndani ya Wizara ya Nishata hatutarudi nyumba, tunatambua umeme ukiwa mwingi tumeshaanza kujenga miundombinu ya kusafirisha, ya kuuziana na nchi za jirani. Leo tunajenga Singida – Namanga kwa ajili ya ku-connect nchi ya Kenya, tuna mpango wa kujenga Masaka Mwanza kwa ajili ya kuunganisha na nchi ya Uganda. Zipo nchi zinahitaji umeme mwingi; umeme ni biashara. Mradi huu ukishakamilika una uwezo wa kuzalisha trilioni 9 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Serikali. Kwa hiyo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge pamoja na maneno yote hatutarudi nyuma, mwendo mdundo katika mradi huu wa Rufiji Hydropower. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wakazi wa Mkoa wa Pwani hususan Kibiti na Rufiji tunatambua mradi huu, bwawa hili litatusaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunatambua fursa za ajira lakini tunatambua vijiji 37 vitakavyounganishiwa umeme katika maeneo ya Morogoro na maeneo ya Mkoa wa Pwani. Si hivyo tu, tunatambua kwamba nia ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka bei ya umeme ipungue kutoka senti 11 USD ya sasa na kadri itakavyowezekana. Haya yote yatawezekana baada ya energy mix ya kutosha hususan ya kuongeza umeme wa maji. Tunatambua, na tumepokea maoni ya kutumia nishati ya jadidifu na ndiyo maana tumetangaza tender kuwaalika wawekezaji binafsi Megawatt 950 kwenye upepo, kwenye maji na kwenye makaa ya mawe; na kana kwamba haitoshi, joto ardhi pia.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge, niwashukuru wote ambao mmechangia hoja yetu na tutaendelea kufanya kazi. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)