Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii na kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Dkt. Mendrad Kalemani na dada yangu Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi kubwa wanayoifanya, hakika Taifa linaona na wananchi wetu wanaona na naamini wako kwenye mikono salama sana kwa hiyo waendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii kwa maneno mafupi sana. La kwanza ni kuhusu mradi wetu wa Rufiji Hydro Power Project. Nimesema wiki iliyopita wakati nachangia hapa nikasema Serikali yetu imejiandaa vizuri hatuna wasiwasi na malipo yoyote kuhusu Mradi huu wa Rufiji Hydro Power Project na ndio maana tumeshalipa shilingi bilioni 723, sio kwamba tumefanya makosa, hapana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa inafahamu kabisa kwamba bajeti uliyotupitishia hapa na Bunge lako Tukufu ilikuwa ni shilingi bilioni 700 kamili lakini mpaka sasa tumelipa bilioni 723.598 ni kwa sababu ya umuhimu wa mradi huu na Waheshimiwa Wabunge wamehoji kwamba zimetoka wapi pesa nyingine, hizi bilioni 23.

Mheshimiwa Spika, naomba kulikumbusha Bunge lako Tukufu kwamba mamlaka ya kufanya uhamisho wa Mafungu kutoka Fungu moja kwenda Fungu lingine ni mamlaka ya Waziri wa Fedha na Mipango. Kunapokuwa na jukumu muhimu, jukumu la msingi ambalo halitakiwi kusubiri mamlaka hiyo Bunge lako Tukufu kupitia Sheria ya Bajeti na kanuni zake alipewa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, anafanya uhamisho wa fedha kutoka Fungu moja kwenda Fungu lingine. Hii bilioni 23.598 Mheshimiwa Waziri amehamisha kutoka Fungu 21 - Hazina kwenda Fungu 58 ili mradi huu uweze kutekelezwa na Taifa letu liweze kupata faida iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, asubuhi wakati najibu swali hapa niliona kulikuwa na mshangao na mshangao wenyewe ni kwamba kodi haichangii kwenye bei ya bidhaa yoyote inayozalishwa. Kwa Tanzania kwa sasa hivi gharama kubwa kwenye viwanda vyetu ni umeme, umeme wetu ni wa bei ya juu na ndio maana Mheshimiwa Rais wetu alipobeba Ilani ya Chama cha Mapinduzi aliahidi ndani ya miaka mitano, bei ya umeme itashuka na haiwezi kushuka, hakuna miujiza ya kushuka kama hatutotekeleza Rufiji Hydro Power Project, naye Mheshimiwa Rais kwa sababu aliahidi ni mtekelezaji na sasa tunatekeleza. Naomba nimwambie Mheshimiwa Spika na Bunge lako Tukufu tuko tayari Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza mradi huu bila kuchelewa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulisemea ni kuhusu deni la TPDC na Waheshimiwa Wabunge wamesema kwamba Serikali imeiachia TPDC kulipa deni hili. Uhakika wa suala hili na ukweli wake ni kwamba deni hili kwa sasa linalipwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi siyo TPDC, ni Serikali kuu ndio inayolipa deni hili na deni lenyewe ni deni la mkopo kwa ajili ya kujenga Bomba la gesi na kuna deni kwa ajili ya mkopo wa Mnazibay. Madeni haya yalichukuliwa kutoka katika Benki ya Exim Bank China na yote haya tumeanza kuyalipa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, cha msingi tu tunachotakiwa kufahamu, mkopo huu ulikopwa na Serikali kupitia TPDC kwa makubaliano kwamba miradi hii itakapotekelezwa TPDC itairejeshea Serikali fedha hizi. Hii kwa sababu ni mradi wa maendeleo ambao lazima ulete faida ndani ya Taifa letu, ndio maana Serikali ikasema kwa sababu miradi hii haijaanza kuzalisha vizuri Serikali inalipa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)