Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kwenye sekta hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu kiuchumi na usalama. Tumeshuhudia shughuli nyingi za maendeleo zikikwama kwa ajili ya ukosefu wa nishati. Akina mama wajawazito wanapoteza maisha pale wanapojifungulia kwenye zahanati/vituo vya afya ambavyo havina umeme na wanatumia torch kuzalishiwa. Kwenye hospitali kubwa ambazo hazina generator ikiwa mgonjwa anafanyiwa operation na umeme ukakatika basi kuna vifo vya mama na watoto hutokea ikiwa ni pamoja na wagonjwa wengine wenye kufanyiwa operation.

Mheshimiwa Spika, umeme unasaidia uchumi wa nchi yetu kwani wananchi wetu wataweza kujishughulisha na uchakataji wa mazao ghafi, viwanda mbalimbali vikubwa na vidogo vitaanzishwa, wafanyabiashara wa chini, kati na juu wote watafaidika. Lakini muhimu kuliko yote ni usalama kwa raia, maana mwanga, hasa vijijini utasaidia sana kupunguza uhalifu.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huu naomba Waziri na Naibu Waziri ambao wamekuwa mara kadhaa wakizunguka kufuatilia utekelezaji wa miradi, hasa ule wa REA, lakini maeneo mengi ya Mji wa Tarime hayana umeme. Mji wa Tarime una kata nane, lakini umeme ni chini ya asilimia 40. Umeme upo Kata ya Bomani kwa asilimia zaidi ya 90, Kata ya Nyamisangura ina umeme kwa asilimia 50 tu, Kata ya Nyandoto ni kwa asilimia 20, Kata ya Kenyamanyori ni chini ya asilimia 20. Maeneo ya Kogete, Tagotha, Mubali, Kenyamanyori Cnetre, Lobasa, Kebaga Mining, Makao, Nyamitende, havina umeme. Kata ya Katare nayo ina umeme chini ya asilimia 30, maeneo ya Nkongore yenye zahanati, shule ya msingi na sekondari havina umeme. Kata ya Nkende nayo haina umeme kwa zaidi ya asilimia 70 za wakazi wake, maeneo ya Magena yenye Kituo cha Afya na shule ya msingi, Katare, Itebe, Nyamihito, Nyamitende, Kata ya Nyandoto, maeneo ya Kewoje, Nyagisesa wanapojenga Mji Mpya na nyumba za Askari Polisi na Kanda Maalum Tarime/Rorya.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mji wa Tarime ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Tarime, ni mji wa kimkakati maana upo mpakani. Wenzetu upande wa Kenya umeme unawaka vyema na kutoa mandhari nzuri wakati wa usiku ilhali upande wa Tanzania Mji wa Tarime ni giza totoro. Ni vyema Serikali ikatoa kipaumbele kwenye miji kama Tarime iliyokaa kimkakati. Nitaomba commitment ya Serikali maana REA inapita kwenye baadhi ya maeneo tu kwenye kijiji na kata na si wakazi wote. Hii inaleta mtafaruku mkubwa na wananchi wanahisi kubaguliwa. Ni rai yangu Serikali kuhakikisha Mji wa Tarime kata zote nane za Nkende, Nyandoto, Katare, Turwa, maeneo ya Buguti, Nyamisangura, Bomani, Kenyamanyori na Sabasaba wapatiwe either umeme wa REA, hasa kata za pembezoni, densification, na umeme wa TANESCO.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, lakini ya umuhimu naomba kuwasilisha, lakini bila kusahau mradi wa Kinyerezi ambao kwa kweli Serikali ikiwekeza vyema itasaidia sana kupunguza kero ya umeme. Ila nishauri Serikali kupeleka wataalam nje ili waweze kuwa na ujuzi kwenye uendeshaji wa mradi wa Kinyerezi, na pia utengenezaji wa mitambo inapoharibika au kui-service kuliko sasa kuipeleka mitambo Marekani kwa ajili ya service.