Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nachangia kwa maandishi Wizara ya Nishati kama ifuatavyo na naomba Waziri anipe majibu stahiki:-

Mheshimiwa Spika, bei ya umeme wa REA Mtwara Mjini, hotuba ya Waziri imesema ataweka utaratibu vijijini kote bei ya REA iwe 27,000/=, lakini Mtwara Mjini hii program ilikuwepo lakini ikaondolewa. Sababu za msingi hakuna, naomba Waziri atupe majibu kwa nini bei hii imeondolewa Vijiji vya Mtwara Mjini ambavyo wamebatiza jina la mitaa.

Mheshimiwa Spika, mkuza wa gesi Mtwara-Lindi; ilisemwa mote mlimopita bomba la gesi mngepelekewa umeme kwa gharama ya REA yaani 27,000/=tu, lakini Mtwara Mjini kata takribani nane bomba hili la gesi limepita. Cha ajabu wananchi wa kata hizi watozwa laki tatu mpaka tano kwa ajili ya kuunganisha umeme wakati sera inasema shilingi 27,000 tu kwenye huu mkuza wa gesi. Waziri kwa nini anatukandamiza Wanamtwara Mjini?

Mheshimiwa Spika, usambazaji wa umeme vijijini/ mitaa ya pembezoni mwa Mtwara Mjini; kila siku Waziri nikimuuliza anasema maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Mtwara yatapelekewa umeme kwa mfumo wa ujazilizo. Mpaka leo Waziri amepeleka sehemu moja tu ya Mbawala Chini kwenda kulambisha kidogo tu. Maeneo ninayoyalalamikia kila siku ni: Mbae-Mkangala; Lwelu- Dimbuzi na Mkangala - Mkunjanguo mpaka Mwenge na Mtawanya- Namayanga.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya ya pembezoni ya Mji wa Mtwara yanaitwa mitaa lakini Wizara haitaki kupeleka umeme kabisa. Waziri atuambie kwa nini anatunyanyasa wana Mtwara Mjini kwa kukataa bila sababu kupeleka umeme mitaa hii wakati umeme wote kusini unatoka Mtwara Mjini? Maeneo haya kila moja haizidi kilomita tatu kutoka vyanzo vya umeme lakini Serikali haitaki kupeleka mtandao wakati gharama ni nafuu sana.

Mheshimiwa Spika, gesi majumbani Mtwara Mjini; imepelekwa majumbani Masaki, Dar es Salaam kwa miaka miwili sasa lakini pale inapotoka hii gesi Wanamtwara tupo tayari kununua hii gesi lakini Serikali haitaki kutuletea. Anachofanya Waziri ni danganya toto tu na kuahidi kuwa mradi wa Mtwara utaanza, lakini hata mimi Mbunge wa Jimbo sina taarifa hata moja juu ya utaratibu wa hiyo gesi majumbani. Nimemuuliza Mheshimiwa Waziri anasema utaratibu bado lakini Masaki anakoishi yeye kapeleka gesi anatumia gesi kupikia, pale Mtwara inapotoka gesi anasema mchakato unaendelea. Hali hii ni uonevu mkubwa na ukandamizaji wa Wanamtwara ambao tumekuwa tunalalamikia kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 90 wa hotuba ya Waziri amesema mchakato wa kupeleka gesi Uganda unakamilika. Haiingii akilini hata kidogo gesi iende nje kutumiwa majumbani wakati pale inapotoka Mtwara ni nyumba 300 tu wakati kila nyumba Mtwara inahitaji hii gesi nafuu ya Serikali. Haikubaliki.