Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya usiku na mchana, kwa kweli wanafanya kazi. Naomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwalinda ili muendelee kufanya kazi zaidi kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Nishati ndiyo sekta wezeshi kwa maana ya viwanda nchini na nchi yoyote ambayo imeendelea kiviwanda ni lazima iwe na umeme wa kutosha. Kwa hiyo, naamini kwamba mipango iliyopo ya Wizara na miradi hiyo ambayo inakwenda kuanzishwa itasababisha nchi yetu iwe na viwanda vya kutosha na hatimaye kuongeza uchumi wa wananchi lakini pia nchi yetu kukua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie juu ya usambazaji wa umeme, hasa kasi ya wakandarasi. Kasi ya wakandarasi wa umeme kwenye maeneo mengi siyo nzuri, hairidhishi. Kwa mfano kwenye jimbo langu mpaka sasa hivi kuna kata tatu hazina umeme kabisa lakini pia mkandarasi aliyepo kwenye eneo langu alianza kazi toka mwaka jana lakini mpaka leo hii ameweza kupeleka umeme kwenye vijiji viwili na katika vijiji hivyo viwili amepeleka kitongoji kimoja kimoja; amepeleka umeme Kijij cha Hang’ana kitongoji kimoja, lakini poa Kijiji cha Iyembela kitongoji kimoja, lakini bado kwenye maeneo mengi hajapeleka umeme. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri tusaidie ili kasi ya mkandarasi iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya maeneo wananchi wameshajituma tayari kuanza, wameitikia agizo la Mheshimiwa Rais la Tanzania ya viwanda tu. Kwa mfano Kijiji cha Ndinga wana kiwanda cha sembe wamenunua toka mwaka 2016 lakini mpaka leo hakifanyi kazi kwa sababu wanasubiri umeme uweze kufika katika kijiji hicho.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna Kijiji cha Madeke, wana kiwanda cha kuchakata mananasi, bado hakifanyi kazi kwa sababu umeme haupo. Wamejaribu kutumia nishati ya dizeli, dizeli ni gharama; lakini pia wametumia solar, haina uwezo mkubwa wa kuweza kustahimili kwa sababu kule eneo la Lupembe ni eneo la mvua nyingi kwa hiyo muda mwingi ni mvua kwa hiyo haiwezi kustahimili kuweza kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukuombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo haya ya uzalishaji kwenye maeneo ya vijiji hivi, kasi iweze kuongezeka ili wananchi wa Jimbo hili la Lupembe waweze kupata umeme na hatimaye kuweza kuanzisha viwanda kwa sababu ni wakulima wa matunda, ni wakulima wa mananasi, ni wakulima wa miti, kwa maana ya mbao, wanataka viwanda ili kuweza kuongeza thamani ya mazao yao.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni juu ya umeme ambao unapelekwa kwenye viwanda. Eneo letu la Lupembe ni eneo la mvua nyingi na tuna viwanda vikubwa, hasa viwanda vile vya chai, tunavyo viwanda viwili katika eneo lile. Lakini pia viwanda vingine watu wanataka kuwekeza wanashindwa kwa sababu maeneo mengi hakuna umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna tatizo moja kwenye viwanda, kwamba umeme unapokuwa umekatika, kwa mfano transfoma inapokuwa imeungua, wamiliki wa viwanda wanatakiwa kununua hizo transfoma, kwa hiyo, imekuwa shida sana. Mara nyingi utakuta kwamba transfoma ikikatika zinaisha wiki moja mpaka mbili hawana transfoma na wananchi wanachuma chai hawawezi kuuza kwa sababu kiwanda hakifanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuombe sana; utaratibu huu wa kwamba wawekezaji ndio wanunue transfoma naona kama siyo mzuri. Ni vizuri TANESCO wawe wananunua hizi transfoma ili zinapokatika basi waweze kurudisha haraka ili wakulima waweze kuendelea kuuza chai yao, waweze kuendelea kuuza mazao yao na waweze kupata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ilivyo sasa hivi, kwa mfano zao la chai likichumwa tu lazima likauzwe na lazima lichakatwe siku hiyo hiyo, likilala siku ya pili chai inapoteza ubora na itakuwa ni ya kumwaga tu. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hasa kwenye maeneo haya ya uzalishaji kwenye maeneo kama ya viwanda vya chai; TANESCO wawe na transfoma zao na ikiwezekana wawe na transfoma za akiba ili pale ambapo umeme unakuwa umekatika basi waweze kuzipeleka haraka ili wakulima ambao wamechuma zile chai zao waweze kuuza siku hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mwekezaji yeye anaangalia faida tu, ukikatika umeme anakwambia umeme haupo kwa hiyo leo hatuchukui chai. Kwa hiyo, mwisho wa siku wanaopata hasara kubwa ni wale wakulima ambao wamechuma hiyo chai na mazao mengine. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, tuwe na utaratibu kwenye viwanda hivi tuwe na transfoma za akiba.

Mheshimiwa Spika, niseme juu ya umeme, hasa umeme unaozalishwa na makaa ya mawe pale Mchuchuma. Nikuombe sana Mheshimiwa, huu mradi ni wa muhimu sana kwa sababu umeme ule utakuja kutusaidia muda ambapo maeneo mengine au vyanzo vingine vitakuwa haviwezi kuzalisha umeme.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)