Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa tumefarijika sana kama Wizara kutokana na michango mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wabunge wameitoa kwa kusema na kwa kuandika. Tumepata ushauri na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ushauri na maoni hayo yalikuwa ya msingi na sisi tunaamini ushauri huu ni muhimu sana kwetu katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tumesikia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao nao wametoa ushauri mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa Serikali kwa hatua mbalimbali imekuwa ikiufanyia kazi. Pia Waheshimiwa Wabunge wapatao 10 wametoa michango yao kwa kusema; michango yao hiyo yenye maoni na ushauri tunayachukua kwa uzito wake na itatusaidia sana katika kuboresha utendaji wa kazi Wizarani. Aidha, Waheshimiwa Wabunge 18 wamechangia kwa maandishi ambao pia michango yao hiyo tumeichukua kwa umuhimu wa kipekee na itatusaidia sana katika kuboresha utendaji wetu.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba hoja zote zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge sisi kama Wizara tunazichukulia kwa uzito wa kipekee na mimi nimesimama hapa kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa. Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda tulionao yawezekana hoja zote hizi nisipate nafasi ya kuzieleza moja baada ya nyingine. Itoshe tu kusema kwamba tutaziwasilisha kwa maandishi kwa Waheshimiwa Wabunge ili pamoja na mambo mengine majibu yetu yawe rejea kwa siku za usoni.

Mheshimiwa Spika, Kabla sijaanza kujibu naomba na mimi nirudie tena kumshukuru tena na tena Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyotupa kwa kuanzisha Wizara hii ya Madini, na kwa kweli Wizara hii pamoja na kwamba inaweza ikaonekana inazo Taasisi chache ina mambo mengi ya kufanya kwa sababu shughuli zake zinasaidia sana ukuaji wa uchumi. Mheshimiwa Rais msukumo alioutoa ni wa kusababisha Wizara hii mchango wake utoke kwenye asilimia 4.8 ya kuchangia Pato la Taifa sasa uwe mchango wa walau asilimia 10 ifikapo 2020. Lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa yeye mwenyewe amekuwa kinara mkubwa sana wa kutusimamia na kutupa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka wakati tunaanzisha utaratibu wa kuanzisha masoko hapa nchini Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye mwenyewe ndiye aliitisha kikao cha Wakuu wa Mikoa wote nchini lakini soko la kwanza la masoko tuliyolianzisha yeye mwenyewe wala hakutuma mtu wa kufanya kazi hiyo kwa niaba yake alifanya mwenyewe. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa msukumo wake huo na sisi Wizara ya Madini tunapata imani kubwa na nguvu kutoka kwake.

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru pia Naibu Waziri wa Madini Mheshimiwa Nyongo kwa ushirikiano mkubwa anaonipa, yeye pamoja na wenzangu Wizarani, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wengine.

Mheshimiwa Spika, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kabisa kama sitakushukuru wewe mwenyewe binafsi. Tulifanya semina moja hapa Bungeni kwa ajili ya kuangalia masuala la madini na wewe ulikuwa mgeni rasmi nakumbuka kwenye hotuba yako maneno uliyoyazungumza, ni kwamba Wizara ya Madini lazima mtuondolee aibu ambayo imezunguka sekta ya madini. Maneno haya ni nyongeza tu ya msukumo mkubwa ambao wewe mwenyewe umekuwa ukiutoa kwenye kusimamia sekta hii. Uliunda Kamati mbili kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka na zote hizi zilikuwa na nia ya kuhakikisha kwamba tunasimamia vizuri sekta ya madini.

Mheshimiwa Spika, ninaweza kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, Kamati yetu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa michango yao, ushauri wao lakini sana kwa kufuatilia kwa karibu mambo mbalimbali yaliyoko. Mwisho lakini si kwa muhimu niwashukuru Wakuu wa Mikoa wote, vyombo vya habari na wadu wa madini; na wengine umewaona wako hapo wamekuja kutuunga mkono. Baada ya kusema shukurani hizo naomba sasa nijielekeze kwenye hoja chache ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezieleza.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja hapa imezungumzwa juu ya wananchi wa Tarime; na hoja hii imezungumzwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye eneo la madini na ambaye pia ndiye Mbunge wa Tarime. Lakini mimi nilikuwa najaribu kutafakari, jambo hili tumelifanyia kazi kwa karibu sana. Mheshimiwa mtoa hoja atakumbuka jambo hili mgogoro wake haujaanza leo umeanza mwaka 2009, 2012. Mimi nimekwenda na Mheshimiwa Heche Jimbo kwa kwake tumekwenda kushughulikia jambo hili la fidia ambalo limekuwa la muda mrefu. Mheshimiwa Heche nilitamani sana leo asimame hapa asema kwa kweli Serikali mnajitahidi kwa kuchukua hatua kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuta wananchi waliofanyiwa uthamini kwenye awamu ya 47 walio kwenye hati ya kulipwa na mgodi wako 66. Tumekwenda na Chief valuer kuangalia nyaraka mbalimbali tumekuta wananchi ambao walikuwa wamefanyiwa uthamini ni zaidi ya 117 wengine wamekatwa kwa hila; na fedha walizokuwa wametengewa kulipwa zilikuwa ni shilingi milioni 224 peke yake; tukakataa tukiwa na Mheshimiwa Heche tukasema hapana Watanzania hawa walichagua Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ili iwasemee, haiwezekani atokee mtu tena kwenye ardhi yao wakatiwe maeneo na wengine wapunguzwe na fedha waliupwe kidogo. Tumeamuru uthamini urudiwe upya. Hili jambo Mheshimiwa Heche nilidhani leo kwa niaba ya watu wa Nyamongo angeweza kufika hapa akapongeza Serikali kwa kufanya jambo hili kwa faida ya watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa mbunge anafaamu, jambo la utiririshaji wa maji kwenye mgodi wa North Mara limeanza kwa muda wa miaka 10 iliyopita. Tumeanza kwa awamu ya kwanza, huu ni mgodi mkubwa, ni kweli tunahitaji fedha kutoka nje, ni kweli tunahitaji ajira kutoka kwa watu wetu kwa ajili ya watu wetu lakini afya za watu ni muhimu kuliko jambo lolote. Nimekwenda mwenyewe na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mheshimiwa Mbunge mwingine aliyenialika Mheshimiwa Agness Marwa, tukafanya mkutano na wananchi wa Nyamongo tukawaambia warekebishe kasoro ifikapo tarehe 30 Machi hawakurekebisha kasoro; hatua ya kwanza kwa mujibu wa sheria tunapiga faini; na tumewapa wiki tatu baada ya wiki tatu kama kasoro hizo hazijarekebishwa tutachukua hatua inayofuata ambayo imetajwa kwenye sharia. Nilitarajia Mheshimiwa Heche angefika akapongeza walau kwa faida hiyo, kwa sababu sisi wenyewe ndio tumeamua sasa kuwasimamia wananchi wa Nyamongo bila kupepesa macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezunguzwa jambo lingine hapa kwenye eneo hili, kwamba je, haya mambo fedha mlizotoza faini warudishiwe wananchi? AG amelieleza vizuri sana na nilitamani sana Mheshimiwa Heche pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi tuchukue nafasi hii ya kuwaelimisha wananchi utaratibu ulivyo. Inawezekana kabisa tunatamani walipwe fidia ya fedha walizotoza faini, lakini unalipa against kitu gani kwa sababu tathimini ya madhara hayo haijawahi kufanyika? Lazima ikishafanyika tukajua ndio tunaweza kwenda kwenye hatua nyingina kama AG alivyozunguzma.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nikuhakikishie wewe pamoja Bunge lako, Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kipaumbele chake cha kwanza ni watu wake na maisha bora ya watu wake waweze kunufaika na rasilimali hizi, tutasimama kidete kulinda uhai wa watu wetu kwa gharma yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ameelze hapa Mheshimiwa Neema Mgaya juu ya taarifa ya GST na kuwafanyia utafiti wachimbaji wadogo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, Wizara ya Madini baada ya marekebisho makubwa ya sheria na kuifanya GST sasa kuwa taasisi inayojitegemea na si wakalaa, tunaenda kufanya utafiti kwa ajili ya maeneo ya wachimbaji wadogo. Na hatua ya kwanza ili uweze kufanya utafiti ni lazima ununue hivyo vifaa vya kufanyia utafiti; tumenunua mtambo maalum kwa ajili ya kuwafanyia utafiti wachimbaji wetu. Niwaombe wachimbaji wa Tanzania wawe na subira tunapoendelea kufanyia kazi mambo haya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Magige ameeleza vizuri sana na ameeleza kwa uchungu tabia ya baadhi ya watu kuendelea kutoza tozo ambazo Bunge hili limezifuta. Nilieleza hapo wakati najibu swali na naomba nirudie tena. Bunge hili halifanyi maigizo hapa, linatunga sheria na sheria hizo lazima zifuatwe, mtu yoyote anayetoza tozo ambazo Bunge hili limezifuta kwa mujibu wa sheria anatenda kosa. Ninaomba Mheshimiwa Magige atuletee mfano wa watu waliotozwa sisi tutachukua hatua. Nimewasiliana na Wizara ya Fedha wamesema hakuna maelekezo hayo.

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine ni tabia ya mtu mmoja tu, huyo mtu mmoja kwa vitendo vyake anavyofanya inaonekana Serikali nzima inanyanyasa watu. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Catherine Magige hakuna mtu atatozwa tozo hizo ambazo Serikali imeshaziondoa, na mimi nikuhakikishie kwamba tutaendelea kulifanya kazi kwa nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Spika, limeelezwa jambo la urasimu kwenye baadhi ya ofisi zetu na ikatajwa specific ofisi ya Geita, na Mheshimiwa Mbunge Ammar. Inawezekana ukaonekana urasimu, lakini tukubali kazi ya kusimamia Sekta ya Madini ndugu zangu imejaa mambo mengine, usipokuwa makini kosa moja la dakika moja unaweza ukaisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi. Hawa vijana tulionao ni wachache lakini jambo la msingi sana; tumefanya kazi Wizara nzima ya kupruni watu wengine ambao tulikuwa tunaona sio waaminifu tumebakiza watu ambao wanafanya kazi . (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawaomba waheshimiwa Wabunge hawa ni vijana wenu, hawa ni watoto wenu, hawa ni wanadamu pia wanahitaji kutiwa moyo; wamefanya kazi kubwa sana. Tunaangalia trend ya mapato inavyokwenda kwa sasa ni tofauti sana na miezi mitatu iliyopita, kazi hii wanafanya vijana hawa. Nikuombe sana Mheshimiwa Ammar, kama kuna specific case, ya mtu mmoja anayesababisa urasimu kwenye ofisi zetu sisi tutachukua hatua. Hata hivyo ombi lako la kuomba ofisi pale Nyang’wale naomba nikuhakikishie kwamba tunaendelea kufanya tathimini kwenye maeneo mbalimbali. Si tu Nyang’wale yako na maeneo ya Mbogwe kuna shughuli nyingi zinafanyika, tunaangalia kama tutapata uwezekano wa kupata human resource ya kutosha tutafungua ofisi ili watu wetu waweze kuhudumiwa kwa urahisi kuondoa mizunguko isiyokuwa na maana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, Mheshimiwa Amar anafahamu, maeneo mengi ambayo yalikuwa yameshikiliwa na makampuni makubwa yote tumeyapelekea default note na tuko kwenye utaratibu wa mwisho wa kuyafuta ili tuwapatie wachimbaji wadogo. Niwaombe wachimbaji wa Nyangh’wale na wachimbaji wa maeneo mengine Tanzania, wajiunge kwenye vikundi, lakini niwaombe pia wachimbaji wa Tanzania mfumo wa kuanza kuchimba wakianza kupata wanagombana hizo zilipendwa. Mheshimiwa Amar ni shahidi, wachimbaji hawatunawa-mobilise tunawaweka kwenye vikundi, wakianza tu kupata pesa migogoro inaanza. Niwaombe tushikamane tunapokuwa tunapata fedha kama ambavyo tunashikamana wakati tunatafuta leseni.

Mheshimiwa Spika, limeongelewa pia eneo hapa na Mheshimiwa Kapufi, juu ya makinikia na usafirishaji wake. Mheshimiwa Kapufi tumeshawahi kulizungumza hili jambo sio mara moja, sio mara mbili, tunayo changamoto ya kisheria, tunaiangalia changamoto hiyo; tunakisikia kilio chake na sisi tunatamani tumuondolee kero hiyo. Tunahitaji mapato kwenye mgodi wake, lakini tunahitaji pia na yeye fedha aliyowekeza iweze kurudi. Hii ni Serikali inayotaka kuona Mtanzania kwenye nchi yake anawekeza na anapata pesa anawekeza kwenye mambo mengine zaidi. Nimwombe Mheshimiwa Kapufi awe na subira tumalize hili jambo, ni jambo la kisheria, lakini kama nilivyomwambia mimi na yeye hapa ninavyozungumza moyo wangu na moyo wake inawasiliana kwa sababu tulizungumza, anajua ni wapi tumekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa hata nikisimama nikasema kesho aanze kusafirisha atakutana na kikwazo ambacho kitampa hasara kubwa zaidi. Naomba awe na subira Mheshimiwa Kapufi, mimi naumia, nimekwenda mwenyewe kwenye mgodi wake na wenzangu Wizarani tunalifanyia kazi, likikamilika tutampa utaratibu utakaofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maftaha ameeleza hapa juu ya One Stop Centre, hii inafanyikaje. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge; One Stop Centre ni mfumo tuliouanzisha wa kufanya biashara ya madini kwenye dari moja. Tunataka kuwaondolea urasimu wachimbaji wetu wa kutoka point moja kwenda point nyingine kwa ajili ya kutafuta huduma. Kwenye One Stop Centre ni jengo kubwa ambalo ndani ya jengo hilo ofisi zote zinazohusika kwa ajili ya utoaji huduma kwenye madini zitakuwepo kwenye ukuta huo. Jengo hilo ni kubwa, Uhamiaji watakuwa hapo, Valuers watakuwa hapo, watu wa kupima ubora wa madini watakuwa hapo, benki zitakuwa hapo, ukienda na madini yako vitu vyote unafanya kwenye eneo moja na kutoka na utaratibu wako unavyojua kwa ajili ya matumizi yako. Kwa hiyo, One Stop Centre sio refinery wala sio smelter wala sio kitu kinachofanya kazi ya kuchenjua, ni jengo kwa ajili ya kutolea huduma. Tutakapokwenda kulizindua nitamwomba Mheshimiwa Maftah tuandamane naye akaone One Stop Centre ilivyo ili aweze kujua tunafanya vitu vya namna gani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Musukuma amezungumzia habari ya watu wanaofanya kazi kwenye Ofisi ya Madini, uaminifu wao. Hilo tunalichukua, ni jambo ambalo tutaendelea kulifanyia kazi kila siku, lakini jambo la maana sana.

Mheshimiwa Spika, Mgodi wa GGM, toka mwaka 2017 tumekuwa na mgogoro na mipasuko kwenye maeneo ya Nyamalembo, nyumba 80 zilifanyiwa tathmini, lakini na sisi tukapeleka timu nyingine kwenda kuangalia. Tumetoka kwenye nyumba 800 tumekuta nyumba zilizoathirika ni zaidi ya nyumba 3,000 na mgodi umekubali baada ya timu ambayo tumeipeleka kule inayohusisha ofisi zote, mgodi walikuwemo, Halmashauri walikuwemo, Ofisi ya Ardhi walikuwemo, watu wa Madini walikuwemo, watu wa RS walikuwemo, ilikuwa timu kubwa imefanya kazi kwa muda ambao kwa kweli, ulizidi hata kiwango cha muda waliokuwa wamepewa.

Mheshimiwa Spika, wamekuja na ripoti nzuri sana juu ya fidia ya maeneo hayo. Nimwombe Mheshimiwa Musukuma, GGM wameanza kulipa fidia, inawezekana hizo fidia mtu mwingine anaweza kusema ndogo, lakini ndogo ukilinganisha na nini na ukilinganisha na tathmini gani? Sisi tunasema fidia hizi zimeanza kulipwa. Kama kuna mwananchi anadhani hajalipwa inavyostahili tuwasiliane na sisi tutampa vigezo.

Mheshimiwa Spika, wametokea watu wengine hapohapo Geita ambao walilipwa kipindi cha nyuma, wako wananchi kama watatu mmoja amelipwa milioni 74. Pamoja na kulipwa milioni 74 kwenye orodha hii tena ya kulipwa upya jina lake limo. Pamoja na kwamba huu mgodi ni wa mwekezaji lakini lazima na sisi tumwonee huruma. Watu ambao wanafikiri wanaweza kupata fedha kwa ujanja ujanja, nashauri tu watafute shughuli nyingine ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, tumewaambia hata watu wa Nyamongo wale walotegesha hawawezi kulipwa hata iweje kwa sababu, wametegesha. Hata wale ambao Mheshimiwa Heche anawajua wa awamu ya 21 na wenzao waliokuwa wanadai fedha, watu 1,934 1,800 walichukua cheki, watu 134 wakaacha cheki, tuliwaambia na wao wakachukue cheki. Tunapokuwa tunawatetea Watanzania ni lazima pia tuwalinde wawekezaji na baadhi ya watu wachache ambao sio waaminifu kwa sababu, pia ni wajibu wa Serikali kuwalinda wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Millya ameeleza hapa juu ya foleni kubwa kwenye ukaguzi wakati watu wanaingia mgodini. Ushauri wake tunaupokea na tunaupokea kwa heshima kubwa na tunauzingatia. Namwomba awe na subira, tunatafuta kibali cha kuajiri watumishi wengine. Mara baada ya kukamilika, tukipata watu tutaongeza workforce pale kwa ajili ya kuangalia watu wanavyoingia pale mgodini.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maige ameeleza maeneo mbalimbali ambayo wachimbaji wake wana mgogoro. Ameeleza eneo la Bushimangira. Ni kweli mimi na yeye tulikwenda. Eneo la Mwazimba ni kweli mimi na yeye tulikwenda na kuna changamoto zilizokuwepo hapo za utoaji wa leseni. Wale waliohusika kwenye utoaji wa leseni hizo kwa kukiuka utaratibu walichukuliwa hatua na Wizara. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maige wananchi wa Mwazimba na wananchi wa Bushimangila kwa Serikali hii wawe na amani, hawatapoteza leseni yao, watapewa leseni yao. Kwa sababu leseni ile ilitolewa katika mazingira ambayo ni tata, sisi Wizara tumechukua hatua moja kubwa zaidi kwa kufuata utaratibu tumeiandikia default notice ili tuweze kuzifuta tuwapatie wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Maige kama ambavyo yeye anasema ni mtetezi wa wanyonge, aendelee kuwatetea wananchi wa Mwazimba na wa Bishimangila. Nataka nimhakikishie Wizara ya Madini tutam- support kwa mambo yote hayo. Ameeleza habari ya fidia, jambo hili tunalifanyia kazi tupewe muda, lakini baada ya muda tutalimaliza na watu wanaohusika.

Mheshimiwa Spika, yako maeneo mengine ambayo nataka nimalizie. Jambo lililozungumzwa hapa ni habari ya Mgodi wa TANCOL, ameelieleza vizuri sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda. Tumeshapeleka barua kutoka NDC, Wizara ya Madini; NDC na yeye analalamika kwenye ubia ule anapunjwa. Tarehe 11 Mei, ametuletea barua na sisi baada ya bajeti hii tunapeleka timu ya wakaguzi maalum kutoka Tume ya Madini kwa ajili ya kwenda kujiridhisha na mambo yote yaliyomo kwenye barua iliyoletwa na NDC.

Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie hili jambo tumeanza kulifanyia kazi mapema. Hapa ninapozungumza TANCOL alikuwa analipa kodi kwa kutumia Sheria ya Madini ya mwaka 1998. Analipa kwa kutumia Net Back Value, kwa maana gani? Kwamba, yeye akishachimba makaa ya mawe, kodi anayotoza anatoza pale site kwa hiyo, wakati sisi tunachukua kodi kwa tani moja dola 53 yeye anasafirisha hayo makaa ya mawe anapeleka kwenye destination yake anauza tani moja dola 220. Sasa kodi tunachukua kwenye dola 53 badala ya dola 200 na kitu. Tumekuwa na ubishani mwingi wa kisheria, lakini hatimaye AG ametupa mwelekeo. Naomba niwahakikishie kwamba, jambo hili tunalifanyia kazi kabisa na Waheshimiwa Wabunge watapata matokeo baada ya taarifa yetu hii kwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niendelee tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge niwaombe kazi ya ulinzi wa rasilimali madini sio kazi ya Wizara ya Madini peke yake, ni kazi yetu wote. Niwaombe tuungane wote na kwa kweli, wachimbaji wadogo wa Tanzania kama hatuwezi kuwapongeza kwa kipindi hiki hatutawapongeza tena, wamekuwa watu wema mno, ndio wanaotupa taarifa. Nimeeleza hapa watu ambao tumewakamata wakitorosha madini wanaotupa taarifa ni wachimbaji wenyewe.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa heshima na taadhima na kwa niaba ya Wizara ya Madini niwashukuru sana wachimbaji wa madini Tanzania kwa kuitikia wito, kwa kuona wivu na rasilimali zao. Nataka niwahakikishie Wizara ya Madini itawapa kila aina ya support watakayoihitaji.

Mheshimiwa Spika, pia niwashukuru sana vyombo vya habari nchini. Uelewa wa sekta ya madini hapa nchini unasaidiwa sana na vyombo vya habari, wamekuwa mstari wa mbele kueleza udhaifu uko wapi, wengine wameandika makala za kiuchunguzi ambazo zimetusaidia kujua ukweli. Kwa mfano kule Mahenge, ilianza makala ya gazeti moja, tulivyokwenda tukakuta mambo mengi yaliyokuwa yameelezwa kwenye makala ile yalikuwa ya kweli. Naomba nirudie tena kuwashukuru sana waandishi wa habari kwa uzalendo wao, kwa kuipenda nchi yao na kwa kweli kwa kuona sekta yetu hii ya madini inakua.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nikushukuru tena kwa kunipa nafasi hii na naomba nitoe hoja. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naafiki.