Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia. Pia, nachukua fursa hii kuwatakia Waislam wote Tanzania na duniani kote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Madini Tanzania, madini ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu Tanzania na inachangia katika Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa hususan tangu imeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano. Cha kushangaza katika bajeti ya mwaka jana taarifa zinasema fedha ya miradi ya maendeleo iliyopokelewa na Wizara ni chini ya asilimia moja. Hili ni jambo la aibu kwa kuwa sekta hii inaingiza fedha nyingine katika Hazina ya Serikali. Sasa ikiwa Wizara imeomba Sh.19,620,964,000.00 badala yake, hadi Februari, 2019 Wizara ilipatiwa 100,000,000 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu haijawa tayari kuendeleza Sekta ya Madini ukilinganisha na nchi za Botswana, Malawi, South Africa, Rwanda na Burundi ambao tumewazidi kwa rasilimali ya madini tuliyonayo Tanzania. Miongoni mwa nchi nilizozitaja zina aina chache mno ama aina moja tu ya madini. Tanzania tunayo aina mbalimbali zikiwemo, almasi, dhahabu, tanzanite, ruby radolite, alexanderlite, blue sapphire, pink sapphire, red sapphire, white sapphire, red gainet, green tomoline, green gainet, rose acquamarine, chuma (iron) shaba, uranium. Aina hizi za madini ni ushahidi tosha kuwa Tanzania yetu ina utajiri wa kutosha na mkubwa katika Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, Serikali ihakikishe Sekta ya Madini inaboreshwa kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida angalau kwa asilimia 80 badala ya kupeleka asilimia 0.5, tuoneshe seriousness katika madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wachimbaji wadogo, ni ukweli usiofichika kuwa wachimbaji wadogo ndio chanzo/waanzilishi wa machimbo ya madini ya aina zote hapa Tanzania na maeneo mengine katika nchi mbalimbali. Nchini kwetu Tanzania wachimbaji wadogo wakishagundua madini, Serikali inawaita wavamizi na wanapelekewa Jeshi la Polisi (FFU) na kupigiwa, kunyanyaswa na kubambikiwa kesi za uvamizi au uhujumu uchumi, mahali pengine wachimbaji wanapigwa risasi na kufa ama kujeruhiwa. Mfano, ni maeneo ya Kalalani, Korogwe, Tanga; Dalini, Korogwe, Tanga; Ngombeni, Korogwe, Tanga; Mwakijembe, Mkinga; Kigwase, Mkinga na Uimba River Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya Serikali kuwaita wachimbaji wadogo, wavamizi, wangepatiwa elimu ya kutosha mitaji ya mitambo ya kuchimbia kama diggers na excavators, pamoja na kuwawezesha kupata mikopo ya masharti nafuu kutoka katika taasisi zetu za fedha.