Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri asubuhi ya leo. Katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 16 amezungumzia juu ya mpango wa ukuzaji wa utalii Kanda ya Kusini (REGROW) ambao unaenda kukuza utalii katika ukanda huo. Mpango huu bado hausemi chochote juu ya utalii katika fukwe za Pwani ya Kusini hususan Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia kina vivutio vingi vya utalii ikiwemo scuba diving, whale shark, sports, fishing, snorkeling na fukwe nzuri. Kupitia Mpango huu wa Kuendeleza Fukwe katika Kanda ya Kusini tunaiomba Wizara iingize ujenzi wa miundombinu katika Kusini cha Mafia kama ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kilindi mpaka Ras Mkumbi kilometa 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo la Ras Mkumbi Kaskazini mwa Kisiwa cha Mafia kina fukwe nzuri kwa ujenzi wa hoteli za kitalii sambamba na utanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mafia. Kwa kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka (runway) kutoka urefu kama kilometa 1.6 ya sasa mpaka kufikia kilometa 3.0 ili kuwezesha ndege kubwa kutoka nchi za nje kutua Mafia moja kwa moja. Upanuzi wa uwanja ulenge kwenye kujenga jengo kubwa la abiria na eneo la maegesho ya ndege (apron).

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wanyama waharibifu akiwemo boko bado ni tatizo. Katika Kisiwa cha Mafia tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Kanyasu alifanya ziara na kusaidia upatikanaji wa fidia ya aliyepoteza maisha kwa kushambuliwa na boko na wale walioharibiwa mazao yao. Hata hivyo bado tatizo halijakwisha na viboko wameendelea kuingia mashambani na kula mazao na kutishia maisha ya wananchi. Niendelee kuiomba Serikali itupatie kibali cha kuvuna viboko hao kwani idadi yao imeongezeka maradufu. Vile vile Serikali iangalie uwezekano wa kujenga uzio kuzunguka maeneo ya mabwawa wanamoishi viboko hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni Channel ya TV ya utalii haioneshi vivutio vya Kisiwa cha Mafia. Tunaomba wahusika waje Mafia kurekodi katika channel hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.