Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri, lakini zaidi niwapongeze wananchi wa Nzega kwa kutuletea jembe. Nimpe Waziri salamu zake kwa wale ambao tulijipanga Muhimbili kumchagua akawa Rais wetu wamemwambia kwamba, hawakukosea walijua yeye ni kichwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, naenda kutumia kigwanomics naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana. Wilaya ya Siha ni wilaya pekee Tanzania ambayo iko katikati ya milima miwili mikubwa na Wilaya ya Siha tulishajipanga kwenye cable cars zile za kupanda kwenye milima na tulitenga eka 800 kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali pamoja na hizo cable cars na mambo ya utalii. Tayari tumeshawakabidhi TANTRADE eka 200 zimebaki 600, aje kwetu Siha uchukue eka 600 ili tuweze kujipanga na ni mkakati mzuri kwa sababu, tukifikiria kutengeneza cable cars tukaanza kuitafakari Wilaya ya Hai, Wilaya ya Siha, tukiangalia vizuri tunaweza kupanga hizo cable cars ninaamini ni kitu ambacho kita-boost sana kuongeza pato la Wizara ya Maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba, Wilaya ya Siha iko katikati ya milima mizuri miwili, lakini imezungukwa, utakuta huku kuna Mlima Meru ambao kuna hifadhi, lakini kwa Kaskazini kwake kuna corridor ambayo wanyama wanapita kutokea huku upande wa Meru na kwingine Tarangire kuelekea upande wa Kenya. Maana yake ni utalii, lakini kunakuwepo na ule wakati wa kupanda Mlima Meru, ukipanda Mlima Kilimanjaro sio tu unapanda moja kwa moja kwenda Mlima Meru ukipitia Siha, unapanda Mlima Meru, lakini Mlima Kilimanjaro wakati unapanda Mlima Kilimanjaro unakutana na hifadhi na unakutana na wanyama, wanyama ni wengi sana. Maana yake tukiwekeza kwenye hizi cables wakati wanapanda Mlima Kilimanjaro lakini chini yake watakuwa wana-enjoy sana kuona wanyama wakiwa chini wanapoendelea. Kwa hiyo, kwa sababu sisi tulishachora mpaka michoro ya hoteli na hizo cables, namwomba Waziri atembelee Wilaya ya Siha ili aweze kuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Siha vilevile ukiangalia tuna mlima unaitwa Donyomorwak ambao ni sehemu ya kuhiji Wamasai Tanzania nzima. Pale kuna heka zaidi ya 3,500 ambayo sasa hivi wameshikiria Polisi CCP. Kwa kushirikiana na polisi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Idara ya Mambo ya Kale tunaweza pale tukatunza ule utamaduni wa Kimasai tukafanya cultural tourism kwenye ule mlima. Kila baada ya miaka saba Wamasai East Africa wanakutana pale. Tutaweka kwa ajili ya kutunza zile, tukatoa kama heka 500, heka 500 zile zikasaidia kupunguza makazi na shida za wananchi na zile heka zinazobaki tukawekeza ikasaidia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa pato lakini ikasaidia maliasili pamoja na vitu vingine. Kwa hiyo, mimi nasema hiyo tukifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Kilimanjaro tuna Uwanja wa Memorial lakini tuna CCP wana eneo kubwa sana; tunaweza tukajenga uwanja wa kimataifa wa mpira pale, Manchester United wakaja kucheza pale lakini wakafanya utalii wa kupanda mlima. Kwa hiyo ndiyo maana leo nikakwambia natumia Kigwanomics ili unisikilize uunganishe hivyo vitu ili twende pamoja tukatengeneze fursa, maana watu wengi wamekuwa wakizungumza yaliyokuwepo na yaboreshweje, twendeni tukaanzishe mapya ambayo yanaweza kutusaidia kuongeza fursa kwenye utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini dada yangu Mheshimiwa Sware ameongea vizuri kuhusu viwanda vya mazao ya miti. Mimi nafikiri ameongelea vizuri viwanda vya mazao ya miti, tuna nchi nyingi sana ambazo zimeingia vitani sasa hivi zinajengwa upya; lakini tukiwekeza vizuri kwenye mazao ya miti na kutafuta masoko nje na kuboresha hivi viwanda vya miti, tutatengeneza sana fursa mpya kwa watu wetu na kutafuta masoko nje na kwa sababu leo tunazungumzia utakuta wanaajiri watu wengi sana, saw-dust nyingi kuna watu wanakuja kuchukua bure tu kwenye maeneo yetu ambayo kuna hivi viwanda vidogo vidogo vya mazao ya miti. Tunaweza tukawekeza pale na tukaleta teknolojia na tukauza mambo mengi sana, nagongea tu vizuri alichokisema Dkt. Sware.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema tena, rafiki yangu Mheshimiwa Ruge amezungumzia kitu pale na akataka kulinganisha sayansi kubwa inayoendelea Stiegler’s Gorge na Song of Lawino. Pale Stiegler’s inaendelea sayansi kubwa sana ya ikolojia pamoja na nishati, huwezi kulinganisha kabisa na Song of Lawino. Kinachogomba kwenye taifa letu hapa si suala la kupata tu nishati, kinachogomba kwenye taifa letu ni kupata nishati ambayo ni bei rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukalinganisha gharama ya thermo energy (umeme wa jotoardhi) na umeme ambao tutazalisha pale ambapo pamekuwepo. Hapa kwetu viwanda vinashindwa kuja kwa sababu gharama ya umeme ni kubwa, hilo ndilo swali kuu ambalo watu wote tunatakiwa kujibu ndiyo maana mtaelewa kwa nini tukakimbia kule, tumekimbia kule kwa sababu kambi ilikuwa imeshauzwa na imenunuliwa na watu kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme hivi George Hartman ni nani anyway? Tanzania tunasema tunaenda kuwekeza kwenye umeme, umeme rahisi utakao-bust viwanda ndani ya Tanzania hii halafu anatokea mtu anaitwa George Hartman anakuja mtu amevaa suti nzuri amependeza kwa pesa za kodi ya Watanzania, anapinga vitu ambavyo vitaboresha kodi ya Watanzania, anakuja kuzungumza mambo ya Hartman hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema watu wamechanganyikiwa, tukisema tunaenda kwenye kamati; tunataka tuende hiyo kamati mpelekeni kwenye hiyo kamati achunguzwe na tuanze sasa kujua wasaliti wa taifa hili. Hatutaki mtu ukiwa Mbunge hapa, ukija hapa Bungeni kama unazungumzia masuala ya kitaifa na yale ya msingi usituletee idea za watu wenye interest na vita vya kiuchumi kwa ajili ya taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hili Taifa litakwenda kulindwa, mambo ya Hartman, huyu Hartman ndugu yake huko miaka 1800 aliwahi kuandika kitabu kuhusu Stiegler’s Gorge, akasema this is the cornerstone of development ya hiyo nchi yake wakati huo East Africa yaani huyo huyo babu yake alisema wakiwekeza Stiegler’s Gorge itakuwa cornerstone ya maendeleo ya Taifa lao wakati ule kutokea East Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo unatokea na ki- proposal cha mtoto sijui anaitwa Hartman thesis yake ya chuo kikuu unakuja kutuambia hapa Bungeni tukae tukusikilize, haiwezekani. Sisi tunachosema Tanzania iende kujengwa, tunataka vijana wazuri madaktari wenye akili nzuri kama Kigwangala, tunataka waende kuchapa kazi tukija hapa wakifanya kazi nzuri tunawaambia tumefanya kazi nzuri, wakikosea tunawaelekeza vizuri kwa sababu lengo ni kujenga Taifa hili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo siongei sana, nilikuwa nataka kusema hao, nimeshaongea na madalali wa siasa, asante sana. (Makofi)