Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie hoja hii iliyopo mbele yetu. Nianze na pongezi; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya ya kuutambua utalii.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Order ndani ya Bunge, order!

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa iliyopo sasa hivi ni jinsi gani Rais alivyojipanga na kuhakikisha kwamba sasa utalii unakuwa katika nchi yetu, ndani ya miaka mitano amefanya kazi kubwa sana. La kwanza, amenunua ndege, hizi ndege kununuliwa kwake maana yake zinaporuka nje ya nchi zinatangaza tayari Tanzania ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi nzuri anayoifanya, wakati huo huo nimpe pole kubwa sana kwa sababu kipindi kile baada ya kumaliza bajeti ya mwaka jana, 2018, alipata ajali mbaya sana. Hatukutegemea tena kwamba leo atasimama na kuisoma tena hotuba yake ya bajeti; yote hayo ni kwa sababu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, leo kamrejesha tena ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo inatokana na jinsi anavyojituma kwa Watanzania. Amesema Mheshimiwa Catherine Magige, amezunguka Tanzania nzima kuona kero ambazo zilikuwepo kwa muda mrefu na miaka mingi ambazo zilikuwa zinawagusa Watanzania; nimpongeze sana na nimpe pole sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Kanyasu, kwa kazi nzuri anayofanya, akimsaidia Waziri. Hata alipokuwa anaumwa alifanya kazi nzuri, lakini pia ushirikiano wake ni mzuri. Vile vile nimpongeze Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya na ushirikiano wanaompa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Bodi ya Utalii; bodi hii kwa sasa inafanya kazi, sasa imesimama. Niwapongeze sana kwa sababu Mheshimiwa Jaji na timu yake yote wanafanya kazi nzuri sana ya kuutangaza na kuusimamia utalii kwa ujumla. Hivi karibuni tumeona watalii ambao walifika kutoka China, lakini tumeona mambo makubwa waliyoyafanya. Kwa hiyo, niendelee kuwapongeza kwamba Tanzania sasa inapaa kwa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninze sasa kuchangia Mkoa wangu wa Tabora. Wakati nachangia Wizara ya Viwanda na Biashara nilitoa tahadhari na leo natoa tahadhari kwa sababu haya ninayoyachangia nachangia kwa Waziri, sichangii kama Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, nachangia kama Waziri wa Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora kuna vivutio vingi sana vya utalii ambavyo nchi hii ya Tanzania ikitaka kufuatilia vivutio vya Tabora na sababu yake, ni kubwa sana. Tabora kuna njia kubwa ya utumwa ambayo ilikuwa inatoka Tabora kwenda Kigoma, watumwa wale walikuwa wanapita njia ile, nimeomba katika miaka yote hii kwamba hii njia ifanyiwe utafiti ili iweze kuboreshwa na watalii wapite waone jinsi gani watumwa walivyokuwa wanasafirishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Tabora kuna njia ya watumwa ambayo ilikuwa inapita chini kwa chini kupitia boma kubwa inakwenda railway station ili wasiwatoroke. Kwa hiyo bado vivutio vikubwa sana viko pale. Wabunge wote wa Tabora kila mtu anayesimama ni lazima azungumzie habari ya utalii wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna boma kubwa la Ujerumani ambalo liko pale, kwa hiyo hakuna sababu ya kutokuwaleta Wajerumani Tabora ili waone vizazi vyao karne zilizopita walifanya nini, kwa hiyo ni history ambayo itatembea. Hata hivyo, pia kuna maboma makubwa ambayo yaliachwa na Machifu. Tabora ilikuwa inaongoza kwa Machifu, Tabora ndiyo kazi ambayo walikuwa wanafanya na mpaka wakasaidia kusitisha suala zima la utumwa. Kwa hiyo historia ambayo iko pale, nimwombe Waziri aione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mimi nikuombe lakini si hilo tu, pia tuna Ugala Reserve ambayo iko pale inasaidia pia, ukiwatoa watalii kwenye mambo ya historia unawapeleka sasa kwenye utalii ambapo wanaenda kupumzika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napitia vitabu hivi, nimeangalia kwenye ukurasa 69 na 70; nishukuru kwamba Wizara imetambua kwamba kweli kuna vitu vya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nina ombi, hakuna barabara zinazo unganisha kutoka pale Kwihala kwenda kwenye maboma ambayo yapo, njia za watemi, hakuna. Kwahiyo niombe basi Wizara yako itusaidie kuhakikisha kwamba kuna barabara za lami zinajengwa kutoka Urambo kwenda Ugala, lakini pia ijengwe barabara hata kama kwa changarawe kutoka pale kwihala kwenda kwenye maboma yale ambayo watumwa waliweza kufikia pale, lakini pia Warabu, Stanlety na Livingston walikutana pale. Kwahiyo kuna historia kubwa sana kama wataboresha; lakini pia hata katika ukarabati nimeona pale haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna historia ya uhuru. Wakati nauliza swali langu namba mia ngapi huko wiki iliyopita walisema kwamba hii historia ya uhuru inakwenda Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Hata hivyo ni vizuri pia hata Wizara ya Maliasili na Utalii ikaeleza historia ya Baba wa Taifa, ikaeleza tarata tatu zilipatikanaje, ikaeleza uhuru, kwasababu kuna utalii wa ndani. Watu wengine wanasoma tu kwenye vitabu lakini Tabora bado ipo, kuna watu ambao wamesoma Tabora, Tabora Waingereza waliitambua na ikawa ina shule nzuri, Kuna watu waliosoma Tabora Boys na Tabora Girls. Kwahiyo historia yake bado ikipangwa vizuri utalii unaweza ukafanikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu kuna suala zima ambalo nilitaka niliongelee, la TAWA. Wakati nimeuliza swali langu hapa nilimuuliza Naibu Waziri kuhusu Bodi ya TAWA, haijakabidhiwa mpaka hivi leo, tangu ya Naibu Waziri alivyotoa kauli, kwamba sasa mkoa iwakabidhi. Sasa hivi TAWA ina mipango mizuri lakini haiwezi kufanya kazi, haina meno. Siku ile niliomba sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba kwa nini utaratibu huu haufuatwi? Kama Wizara imetoa amri, maelekezo au waraka, kwamba sasa Bodi ile ianze kufanya kazi; hakuna kazi inayofanyika kwenye game reserve, hakuna kazi inayofanyika kwenye Zoo ya Tabora Manispaa; hakuna chochote kinachofanyika kwa sasa kwasababu hawana meno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nipate majibu vinginevyo hapa tena ndiyo itakuwa tabu. Nipate majibu kwanini mpaka sasa Bodi hiyo haijapewa nafasi ya kufanya kazi, na kwanini hawajahamisha kuwapa madaraka kutoka Mkoani kwenda kwenye Bodi hiyo ambayo ni ya TAWA? Mpaka sasa hawajapewa kitu chochote na bado makabidhiano hayajafanyika, hii figisufigisu inatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nililotaka kuchangia ni kuhusu Chuo cha Nyuki; hapa sasa leo napongeza. Niipongeze sana Wizara hii na hasa niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya kwasababu sasa kuna mabadiliko ya Chuo cha Nyuki. Yale mahitaji ambayo yalikuwa yanahitajika kwa kweli angalau Serikali imefanya kazi nzuri na imetambua. Sasa kwa kuwa kitakuwa chuo rasmi sasa cha kufuga malkia wa nyuki ni vyema sasa niiombe Serikali iongeze fedha na fedha zipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ombi langu kwa Chuo cha Nyuki, kuna uzio ambao walitoa ahadi kwamba utajengwa; niombe sasa fedha ziende kwa wakati ili ule uzio ujengwe kwasababu wananchi wanasogea na wakisogea wananchi kuwatoa ni gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo mimi niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii, nikuombe sana Mheshimiwa Kigwangala, hebu iangalie hii mipaka, kwa sababu kuna Chuo cha Ardhi ambacho kiko pembeni na kuna shule ya Msingi. Kwahiyo tusipoziba uzio na tusipoweka mipaka ya uhakika tutakuja kuwaondoa wale kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo mimi msisitizo wangu ni huo, kwamba Bodi ipewe meno ya kufanyakazi, kwasababu hata kama ina mipango ya kufanya kazi haitafanyika kwasababu tunakwenda kwa utaratibu na tunakwenda kwa sheria. Sasa kama ni sheria basi utakapokuja hapa kumalizia kutoa majibu nipate jibu sahihi lini Bodi ya TAWA itapewa meno ya kufanyia kazi au itakabidhiwa rasmi ili waweze kufanya kazi hiyo lakiniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono asilimia 100.