Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuleta hotuba nzuri. Napenda kuchangia maeneo mawili ya migogoro baina ya wafugaji na makundi mengine hususan wakulima na soko la samaki.

Mheshimiwa Spika, migogoro kati ya wakulima na wafugaji (pastoralists) imegharimu maisha ya watu, mifugo na uharibifu wa mazao. Wafugaji wanaohamahama kwa sehemu kubwa wanatafuta malisho na maji. Haya ndiyo maeneo yanayosababisha wafugaji kuchunga katika mashamba ya wakulima na wakati mwingine wanaingia katika maeneo yasiyoruhusiwa kama Hifadhi za Taifa. Hata mifugo wanaposafirishwa wakati mwingine wanaswagwa kupitia barabara kuu, wanaharibu barabara na kadhalika. Kwa nini usafirishaji wa mifugo usiwe na vyombo rasmi na inapobidi watumie National Stock Routes? Kama zimefifia, kwa nini zisifufuliwe?

Mheshimiwa Spika, suluhu ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja ni maandalizi ya matumizi bora ya ardhi, lakini kwa upande mwingine ni usimamizi wa sheria, sheria ndogo na kanuni zinazotawala matumizi ya ardhi. Aidha, ni muhimu Serikali ikajenga mabwawa maalum kwa ajili ya kunywesha mifugo na inapowezekana mifugo ijengewe mabirika ya kunywea maji (cattle troughs). Zamani Wizara ya Mifugo ilikuwa na kitengo cha kujenga mabwawa ya mifugo, kwa sasa ni vema watumie DDCA.

Mheshimiwa Spika, Soko la samaki (tuner fish); mwaka 2017 nilifanya ziara nchini Spain kutafuta soko la samaki aina ya tuner. Nilichokikuta huko ni kwamba, viwanda vya kusindika samaki hao vilikuwa vinaagiza samaki kutoka China. Sina uhakika kama samaki wote wanaotoka China kweli wanatoka huko. Hata hivyo, nilipofika Spain, walinipa ripoti iliyoandaliwa na wataalam kutoka Denmark inayoonesha kwamba tuner fish wanapatikana kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu kwa mwaka hapa Tanzania. Naleta swali hili Wizara ilifanyie kazi; je, ni kweli upatikanaji wa tuner fish hapa Tanzania ni mdogo na seasonal kiasi kwamba wawekezaji hawavutiwi kuanzisha kiwanda? (Mheshimiwa Waziri apeleleze).

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.