Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu pia naunga hoja maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tuna mifugo ya takribani zaidi ya milioni 30.5 kwa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Uvuvi na Mifugo kwa mwaka 2017/2018; na Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa takwimu hizi hazioneshi uhalisia wa Watanzania kunufaika na wingi wa mifugo. Kwa hiyo changamoto zilizopo kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi; nadhani sasa Waheshimiwa Wabunge wameeza kwa upana wake; changamoto tulizonazo ziko wazi. Tunakosa viwanda kwa ajili uzalishaji; Waheshimiwa Wabunge wameongelea masuala ya uzalishaji wa nyama, maziwa, pia viwanda vya ngozi. Tuna changamoto za kukosa sera na kanuni ambazo zingeweza ku-support tukapata ubora wa bidhaa, tukaweza kuuza ndani ya nchi na kupata masoko nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapata changamoto kwa kutokupata sera na kanuni ambazo zingewezesha wawekezaji kwenye Sekta Binafsi, wangeweza kuwekeza na tukapata viwanda na tukapata bidhaa ambazo zingeweza kulinufaisha taifa.

Mheshimiwa Spika, niongelee kwa kifupi, Mkoa wa Katavi tuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi, na tangu mwaka 1961 tulikuwa na hifadhi moja tu; lakini kwa sasa tunahifadhi za kitaifa zaidi ya tano. Sasa unaona tatizo la migogoro ya ardhi, kwa maana ya wafugaji kukosa maeneo ya malisho ni kutokana na Serikali kuendelea kuchukua maeneo tengefu, pia kuendelea kuchukua maeneo kwa ajili ya kutenga maeneo ya hifadhi. Kwa hiyo kama Serikali ikiendeela kutenga maeneo haya, kuchukua maeneo ya wananchi ambao kwa sehemu kubwa walikuwa ni wafugaji wakaweka hizo hifadhi, sasa hawa wafugaji wetu wanakwenda wapi? Ndiyo maana unaona wanasambaa kwenye mikoa mbalimbali, wanaenda kuvamia maeneo ambayo mengine ni maeneo ya wakulima, makazi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo Serikali, kwa sababu tuna eneo kubwa la misitu ione namna ya kuweza kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji, ili kuondoa migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo kuhusiana na Mkoa wangu wa Katavi. Kumekuwa na mauaji ya kipuuzi kabisa yanayoendelea; na ni nimseme tu kwa kifupi Mkuu wa Wilaya ambaye anajiita ni Muhando katika Wilaya ya Mpanda Vijiji, kwa maana ya Tanganyika, amekuwa anatumia ubabe ambao kimsingi ni unyanyasaji ambao unaendelea kwenye taifa na watu hawana sehemu ya kusemea.

Mheshimiwa Spika, ukihitaji nikupe CD ya mauaji ambayo yametokea katika Kijiji cha Lyamgoloka, ni hii hapa. Wananchi wamepigwa risasi, watu wanachomewa nyumba, mifugo inapigwa risasi, watu wanapigwa hawaelewi hatima yao ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa taifa hili mnalosema ni la wanyonge ni kwa nini Serikali hii ya Awamu ya Tano inakaa kimya? Ni kwa nini mnashindw ku-solve migogoro ambayo inaendelea katika Jimbo la Mpanda Vijijini? Na hawa askari wa wanyamapori ambao wengine wamekuwa si waaminifu wanapora ng’ombe, ng’ombe wanapigwa risasi. Ni kwa nini Serikali hii inashindwa kutatua migogo hii?

Mheshimiwa Spika, na huyu Mkuu wa Wilaya amekuwa sasa ana kashfa nyingi na wananchi wa Mpanda Vijiji hawamtaki kutokana na kero na matatizo ambayo yanaendelea kwenye hili. Vijiji ambavyo vimeathirika kutokana na Mkuu huyu wa Wilaya ambaye sasa anajifanya ni Mungu mtu kuna Kaseganyama, Mnyamasi, Karema, Ikole, Isengule, Kapalamsenga pamoja na Vijiji vya Iseganyama.

Mheshimiwa Spika, watu wanaishi kama wako porini, ni kwa nini Mkuu wa Wilaya anafanya matendo ya kinyama, anaamlisha Askari wa wanyamapori pamoja na Polisi kwenda kuwapiga wananchi; leo watu wanaishi kwenye mahema, watu hawaelewi hatima yao ni nini. Hivi leo wafugaji wamekuwa wanaishi katika mazingira ambayo hawaelewi hatima yao ni nini halafu mnasema nchi ni ya amani?

Mheshimiwa Spika, ninaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha aeleze ni namna gani atatatua mgogoro na huyu Mkuu wa Wilaya Muhando sisi hatumtaki, wananchi wa Jimbo la Tanganyika hawamtaki kwa sababu tangu ameingia katika Mkoa wa Katavi amekuwa ni kero na hana suluhisho katika migogoro ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, niongele masuala ya tozo; bado iko pale pale. Halmashauri ilitenga kwamba wafugaji wanapoingiza mifugo kwenye maeneo ambalo si sahihi, kwa maana ya hifadhi watozwe shilingi 50,000 kwa mara ya kwanza, kwa pili wanatozwa shilingi 100,000 na kuendelea. Sasa fedha hizi watu wamekuwa wanatozwa zaidi ya 100,000. Ng’ombe mmoja akiingia kwenye chanzo cha maji wanalipishwa mpaka milioni moja; sasa hizi pesa zinakwenda wapi?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Rhoda tunakushukuru sana.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante.