Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani Bungeni. Hotuba yetu ina vitu vizuri, tumeshauri vizuri, naiomba Serikali ichukue ushauri huo utawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kwenye Operesheni Nzagamba. Naenda moja kwa moja kwenye Operesheni Nzagamba kwa sababu ninafahamu ni nini ambacho ninakwenda kukizungumza na nini matokeo ya Operesheni Nzagamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposimama hapa, hususan mimi nikisimama ni kwamba si mgeni kwenye suala la ufugaji, hata uvuvi. Operesheni hii naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, kwamba tunapozungumza hii operesheni inawezekana wapo wachache ambao wanaielewa kwa udogo sana, lakini niwaambie kwamba jambo hili la Operesheni Nzagamba limesababisha matatizo makubwa sana. Limesababisha vifo, watu kufilisiwa ng’ombe wao; limesababisha matatizo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita hapa tulipitisha Sheria ya Mahakama za Kutembea, tukazibariki. Sasa hiyo sheria tuliyoipitisha mimi nasema imekwenda kutumika kwa wafugaji. Imetumikaje; hawa waliokuwa wanatekeleza Operesheni Nzagamba walikuwa wanakwenda wakiwa na timu nzima; wakiwa na mnunuzi wa ng’ombe, wakiwa na dalali, wakiwa na Mwanasheria, wakiwa na mgambo. Sasa kama ng’ombe wanapigwa Itilima atakayenunua wale ng’ombe si wa Itilima, unakuta ametoka Katavi, unakuta ametoka mikoa mingine. Sasa najiuliza kwamba, hawa waliokuwa wanaenda kununua hawa ng’ombe walikuwa wanajuaje kwamba kuna mnada wa ng’ombe Itilima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni changamoto ambayo ni kubwa. Kilichokuwa kinafanyika, wanakwenda na mgambo wakiwakuta wale wachungajhi wale, wanakimbia wanawaacha, wanawakimbia wale ng’mbe wao. Mgambo wanawazingira wale ng’ombe, wakishawazingira wale ng’ombe dalali anaanza kazi yake. Anaanza kufanya hivi, analeta ng’ombe mmoja-mmoja anasema ng’ombe huyu laki nne, anakosekana mnunuzi, laki tatu, anakosekana, laki mbili, anakosekana, laki moja, anakosekana. Anaweka pembeni analeta tena ng’ombe mwingine, laki nne, anakosekana, wakifika ng’ombe wanne anawaambia laki tatu kwa pamoja, mununuzi anapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipoteuliwa, Wasukuma wote tulifurahi katika uteuzi wa Rais, tulishangilia kwa sababu anafahamu jiografia ya wafugaji, lakini umekwenda kututelekeza. Leo wafugaji wanalia anajifanya kwamba hajui umuhimu wa wafugaji, jambo ambalo linasikitisha sana. Naomba wanisamehe kaka zangu wote wanaotoka Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Mpina ametutelekeza, haendani na kile tulichokuwa tunakitegemea sisi. Haiwezekani leo Mheshimiwa Waziri asisahau… (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi, Mheshimiwa Jenista kuhusu utaratibu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ni jambo la kiutaratibu na watu wanaweza wakaliona ni jambo ambalo halina maana, lakini naomba niseme Kanuni ya 64(1)(b) inampasa kila Mbunge anayechangia humu ndani kuchangia hoja kwa kuzingatia hoja ambayo imewasilishwa ndani ya Bunge. Hoja inayochangiwa inahusu Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Waziri mwenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi alipoteuliwa hakuteuliwa kwa muktadha wa kutazama kabila la Wasukuma, aliteuliwa ili kuwa na fairness, kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Sekta nzima ya Uvuvi na Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si sahihi sana kusema kwamba alipoteuliwa Waziri huyu, Wasukuma walifurahi lakini sasa Wasukuma wanasikitika amewatelekeza, siyo fair. Ni lazima tuseme siyo fair, tuchangie kwa kuzingatia utaratibu ambao… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Jenista. Mheshimiwa Gimbi maneno hayo ni ya maudhi kwa hiyo naomba uyaondoe.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama nimezungumza kitu ambacho ni cha ajabu sana, siamini. Nasema hivyo kwa kutumia lugha ya Wasukuma nikiamini kabisa kwamba Wasukuma ndiyo wafugaji wakubwa wakifuatiwa na Wamasai, nimezungumza hivyo. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Nimezungumza kwa uhalisia huo.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo...

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge naona muda umeisha, hamna taarifa wala nini, Mheshimiwa Gimbi endelea.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi naomba uendelee kutoa mchango wako kwa lugha iliyokuwa inastahiki Bungeni.

MHE. GIMBI D. MASABA: Nimezungumza haya kwa uchungu, sikutaka kwenda kwenye kitabu cha Waziri hata kidogo. Mara nyingi kwenye michango yangu nimekuwa nikisimama nazungumzia kuongezewa kwa bajeti…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini kuna nini tena. Mheshimiwa Gimbi kidogo, Mheshimiwa Chief Whip wa upande wa Upinzani.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepaswa nitoe taarifa hii kwamba hata wafanyabiashara wanafurahi kama Waziri mfanyabiashara ameteuliwa kwa sababu anaifahamu sekta. Kwa hiyo, Gimbi hakuwa na maana ya ukabila ila alikuwa ana maana kwamba kwa sababu Mheshimiwa Mpina ni mfugaji, basi wafugaji watafurahi kwa sababu anaifahamu sekta. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi naomba uendelee.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza uhalisia wa mazingira yenyewe, Mheshimiwa Waziri anajua, pamoja na kwamba wananchi walitaifisha hizo ng’ombe, kuna wananchi walikwenda mahakamani na walishinda kesi.

Sasa anataka kuniambia kwamba wananchi walioshinda kesi Mkoa wa Simiyu, hajui kama wanatakiwa kurudishiwa ng’ombe wao? Mpaka leo hawajawahi kurudishiwa ng’ombe, halafu leo wanataka tuzungumze maneno ya upole, kwa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la uvuvi, sawa Mheshimiwa Mpina amekulia dagaa lakini leo dagaa kwa wavuvi imegeuka almasi. Mkoa wa Simiyu tuna minada, leo ukienda kwenye mnada unatafuta dagaa huwaoni, lakini muuzaji wa dagaa yupo, maana yake ni kwamba dagaa ameficha guest, kwa hiyo ukimuuliza dagaa wapo wapi, zipo guest unataka? Huko ndiyo anatupeleka Mheshimiwa Mpina, dagaa wanauziwa guest halafu wanataka tuzungumze lugha ya kipole hapa, haiwezekani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ambacho hakifahamu Mheshimiwa Mpina kwa wafugaji na wavuvi, hapana haiwezekani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gimbi malizia sentensi yako.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo sekunde tu. Huu uanzishaji wa hifadhi za wanyamapori za jamii zimeleta changamoto kubwa sana. Mwaka jana nilizungumzia kuhusu suala la Hifadhi ya Maswa Reserve kuhusu kuongeza mipaka, wananchi wanakosa malisho na kila kitu, lakini wametanguliza watu wanakwenda kulaghai viongozi halafu wanachukua maeneo wananchi wanashindwa kupata machungio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanaudhi sana, nakushukuru sana. (Makofi)