Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja ya Wizara hii na kuipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha sasa Tanzania yetu inapata mafanikio katika Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi. Napongeza mikakati na mipango yote iliyopangwa na Wizara na naomba Serikali na sisi wadau tuhakikishe tunaungana na Serikali na Wizara hii kuhakikisha mipango yetu hii inafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi na shukrani hizo na pia naipongeza Wizara kwa kuanzisha kupitia upya Sheria ya Uvuvi na hasa pale walipoamua kwa makusudi kabisa kuwashirikisha wadau wote wa sekta hii ya uvuvi nchini kote Tanzania. Pamoja na hilo pia, naipongeza Wizara kwa kutafsiri Sera ya Uvuvi. Kama tunavyofahamu wavuvi wetu wengi ni masikini hawajasoma Kingereza kwa hivyo naipongeza Wizara hii kwa kuamua kuitafsiri sasahivi ile Sera ya Uvuvi, ili kila mvuvi aweze kutambua sera hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Wizara kwa kufufua Shirika la TAFICO. Najua mambo mengi yameshafanyika huko TAFICO, lakini pia naomba sasa Serikali iangalie hili jambo ambalo ni mwingiliano wa kisheria na kanuni na majukumu ya utendaji wa kazi kati ya Wizara hii ya Uvuvi na Wizara nyingine za Serikali. Jambo hili likifanyiwa kazi kuna changamoto nyingi zitaweza kutatuka. Pia naomba Serikali iangalie tozo mbalimbali kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara nyingine, kuna tozo zinaingiliana na hivyo kuleta mkanganyiko katika utekelezaji wa majukumu ya kazi ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nigusie kidogo uvuvi wa bahari kuu. Napongeza sana mchakato wa Wizara na mchakato wa Serikali ulioanza wa ujenzi wa bandari ya uvuvi. Naomba mchakato huo sasa pia uanze na uendelee kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Sisi kisiwa chetu cha Zanzibar hatuna rasilimali nyingine isipokuwa bahari, tumezungukwa na bahari, mapato yetu yanategemea sana bahari. Naomba sana Serikali iangalie sasa zile tozo ambazo zinatozwa kwa wanaoomba kuvua kwenye bahari kuu, yaani zile leseni za uvuvi ziangaliwe upya zile kodi na tozo ili angalau na sisi hizi leseni zikitolewa nchi yetu nayo itapata mapato kupitia hii sekta ya uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye sekta ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji. Naipongeza sana Wizara na imepeta fedha hivi karibuni kwa ajili kuimarisha sekta hii ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji na hasa ufugaji wa samaki. Pamoja na hilo liende sambamba na Maafisa Ugani ili wawe na teknolojia mpya katika ufugaji samaki na mazao mengine ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huu ufugaji hautaki elimu kubwa sana; kwa hivyo naomba kile chuo cha uvuvi kinachofundisha mambo ya ufugaji samaki kiangalie ile mitaala au vile vigezo vya kuingia kwenye chuo kile cha kujifunza ufugaji wa samaki, kwa sababu tunaona hata majumbani watoto wadogo wa miaka saba wanawafuga wale gold fish na wanauza; kwa maana hiyo haitaki elimu kubwa. Hivyo vijana waliomaliza darasa la saba wakiwezeshwa, wakipewa mitaji na wakipewa elimu hii ya ufugaji samaki tunaweza kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu wa darasa la saba na vijana wa form four kwa sababu elimu inayohitajika si kubwa sana. Tuandae programu za muda mfupi za kuwafundisha hawa vijana ambao wamemaliza shule mapema ili wajiajiri kwenye sekta hii ya uvuvi na ufugaji wa samaki pamoja na kuwasaidia njia bora za kupata mikopo kwa gharama nafuu au kwa masharti nafuu waweze kukidhi kupata hivyo vifaa vya ufugaji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na huduma mbalimbali za kuwasaidia wavuvi wetu naomba sana Serikali ione Wizara kwamba huduma za kijamii kama vile vyoo, vituo vya afya, vituo vya Polisi kwenye maeneo yale ya madago wanakovua wavuvi vipewe kipaumbele kwa sababu kule nako wanaishi binadamu na kunatokea milipuko ya maradhi, lakini pia kunatokea na hujuma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba Serikali na Wizara iendelee kuwaboreshea wavuvi wetu zana bora za uvuvi ili kupata uvuvi wenye tija na wenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naelekea kwenye Wakala wa Maabara na …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khadija malizia, kengele ya pili imelia.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kuipongeza Wizara hii kwa kuanzisha viwanda vya ngozi, viwanda vya usindikaji maziwa na viwanda vingine vipya vya usindikaji wa nyama. Tuko pamoja tunawapa nguvu viongozi wetu hawa, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Maafisa wote, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.