Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia mawili; la Kwanza ni Kuhusu Mifugo. Tanzania tuna mifugo mingi sana, kama 32,000,000 lakini mifugo hii inachangia Pato la Taifa asilimia 7.6, ni kidogo sana, kwa sababu mifugo yetu haikuboreshwa. Sasa na suala la kuboresha mifugo ni suala la elimu. Muwaelimishe wafugaji jinsi ya kuboresha mifugo yao na si suala la kusema kwamba punguzeni mifugo, punguzeni mifugo. Tupunguze tuipeleke wapi? Kwa hiyo suala wale maafisa ugani wafanye kazi ya kuelimisha wafugaji jinsi ya kuboresha mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile mifugo inahitaji maji, mabwawa ni shida. Kwa hiyo mimi nilikuwa na shauri kwamba maeneo yote mabwawa yachimbwe ili wafugaji wapate mahali pa kunywesha mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri nimewahi kutembelea Botswana na Namibia. Botswana watu wachache, asilimia ndogo sana lakini wana mifugo haifiki hata 3,000,000 lakini mifugo kwa nchi ya Botswana inachangia takriban asilimia 40 ya Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema badala ya kuhimiza watu wapunguze mifugo, mboreshe, muelimishe wananchi ufugaji bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nizungumzie suala la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania. Niliuliza swali hapa, hata Mheshimiwa Waziri ulikuwepo, ulikuwa Mbunge mwenzangu hapa; kwamba ni lini Serikali itaanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo; na niliomba Makao Makuu yawe Mpwapwa. Kweli Serikali ilitoa jibu kwamba basi tutafanya mpango tuhakikishe kwamba tunaanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania. Hiyo Taasisi imeshaanzishwa lakini jambo la kushangaza Mheshimiwa Waziri kwakweli mimi Mbunge wa Mpwapwa mnanionea. Mmehamisha kituo cha uchunguzi wa magonjwa, VIC Mpwapwa mmeleta Dodoma, Dodoma hakuna vifaa ni majengo yale! Lakini sasahivi majengo ya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo yale yaliyopo majengo yako Mpwapwa yanaharibika, yanachakaa hayana kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini mnahamisha vituo vyote? Sasa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ilianzia Mpwapwa leo mnahamishia kwenye maghorofa NBC pale, pale ghorofa la NBC kuna mifugo? Hivi wageni wakiwatembelea kutoka nje mtakuja kuwaonesha yale maghorofa? Maana kituo cha utafiti ama taasisi inatakiwa Makao Makuu yawe pale ambapo kuna mifugo, hata wageni wakija mnawatembeza kwenye mashamba ya mifugo. Sasa kila kitu mnahamishia Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Makao Makuu yarudishwe Mpwapwa pale. Jengeni majengo maofisa wote wawe pale. Haiwezekani kabisa! Mifugo iko Mpwapwa Taasisi Makao Makuu kwenye maghorofa ya NBC, haiwezekani! Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, umehamisha VIC, umehamisha Makao Makuu ya Taasisi ya TARIRI, kuja Mpwapwa kuja Dodoma, hapana! Ni kweli Dodoma ni Makao Makuu ya nchi lakini Mpwapwa vilevile iko Dodoma. Kwa hiyo nakuomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliojenga Chuo cha Uchunguzi wa Magonjwa VIC wenzenu waliona mbali. Pale kuna Kituo cha Utafiti wa Mifugo, kuna Chuo cha Mifugo na Taasisi ya Uchunguzi wa Mifugo. Hii ilikuwa inasaidia wale wanafunzi walikuwa wanajifunza pale practicals, sasa wanasafiri kutoka Mpwapwa kuja Dodoma, gharama gani hii? Gharama kubwa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu Kituo cha Uchunguzi au Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa. Kile kituo kimeanzishwa mwaka 1905, mimi naanza kusoma darasa la kwanza mwaka 1958, kile kituo n a baba yangu mzazi mimi ndiye alieanzisha kile kituo. Sasa Mheshimiwa Waziri, kituo kina mahitaji mengi sana. Zamani kulikuwa kuna matrekta, kulikuwa na magari mengi, kulikuwa na vitendea kazi vingi sana; na pale unaposikia Kituo cha Utafiti wa Mifugo kuna mifugo, na ile mifugo inahitaji chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kinahitaji vitendea kazi vya kutosha; wanahitaji mashamba ya kulima majani ili mifugo ipate chakula. Sasa kuna trekta moja tu, hakuna hata jembe moja la kulimia. Hicho ni kituo cha Uchunguzi Mpwapwa, Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba sana katika bajeti yako; nashukuru kwamba umeelezea hapa lakini nakuomba kile kituo ndicho cha kwanza Tanzania, Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa, ndicho cha kwanza. Kwa hiyo naomba ukiboreshe. Tunaomba vitendea kazi vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine, Serikali ilipunguza watumishi wahudumu wote pale waliondoka, hakuna hata mhudumu; sasa sijui mlitegemea nani wafanye kazi. Kuna mambo ya bush clearing, hao watafiti wana ma- degree watakwenda kufyeka kule? Watakwenda kukamua dairy? Haiwezekani! Na bahati nzuri kituo kimeajiri vibarua. Wako zaidi ya 76, sasa ni mwaka wa tatu hawajalipwa hata senti tano; na hawa ni binadamu na wana familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana hawa vibarua mliowaajiri pale ndio wanaochunga, ndio wanaokamua, ndio wanaofanya kazi zote za nje, walipwe basi haki zao. Mimi nimechoka foleni, kila siku nyumbani kwangu, Mheshimiwa Mbunge tusaidie tulipwe pesa zetu. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, walipwe hela yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Kabla sijagongewa kegele, naunga mkono asilimia 100 Wizara hii lakini Mheshimiwa Waziri ujibu hoja zangu. Usipojibu hizi hoja hasa za kuhamisha Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo, nakamata shilingi leo. Ahsante. (Makofi)