Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake wawili kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kilimo chetu kinanyanyuka.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme mambo mawili makubwa, na jambo la kwanza ni ambalo limesemwa kwa kiwango kikubwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, lile la kufikia asilimia 10 ya bajeti yetu kupelekwa kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inatambua sana umuhimu wa sekta ya kilimo katika kufikia dhima ya mpango wetu wa pili wa maendeleo wa miaka mitano. Hakuna viwanda bila kuwa na malighafi na hakuna malighafi bila kuwa na kilimo.

Mheshimiwa Spika, nimeanza kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, mchango wa kilimo chetu, kwenye uchumi wetu wa taifa unaonekana sasa na unaendelea kukua; mwaka huu ime-register ukuaji mzuri tu na mimi nawapongeza sana. Hiyo yote imetokana na Serikali kuwekeza katika kilimo chetu. Ndiyo maana pamoja na mambo mengi ambayo Serikali inayo ya kufanya, kwa mfano tunaangalia uhalisia wa mapato yetu kwa mwaka husika ukilinganisha na mahitaji ya lazima yanayohitajika ili mambo mbalimbali yaweze kutendeka. Kwa mfano ulipaji wa Deni letu la Taifa ambalo lilitumika kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya miradi yetu ya maendeleo. Vilevile tunatakiwa kuhakikisha watumishi wetu wanalipwa mishahara yao kwa wakati, jambo ambalo Serikali yetu inatenda sasa tangu imeingia madarakani.

Mheshimiwa Spika, pia Waheshimiwa Wabunge tusisahau kwamba tunavyowekeza kwenye kilimo siyo ile pesa inayokwenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Kilimo. Tunaweza tukapeleka pesa nyingi kwenye kilimo lakini kama hatuna miundombinu hatutaweza kuleta athari chanya kwenye kilimo chetu, na ndiyo maana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi aliimarisha sana miundombinu. Mikoa yetu yote imeunganishwa na sasa tunaenda kukamilisha Mkoa wetu wa Kigoma kuunganisha na mikoa mingine.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunataka kuhakikisha tumbaku inayozalishwa Tabora, pamba inayozalishwa Mwanza inasafirishwa kwa siku moja kufika Dar es Salaam. Hata kama ni viwanda vyetu vya nguo vinavyoenda kuanzishwa kule Bariadi – Simiyu, tunataka kuhakikisha nguo zile zinafika ndani ya siku moja Dar es Salaam. Tunaenda kuwekeza kwenye SGR ili kuhakikisha kilimo chetu kinaleta tija kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, tunaposema Tanzania ya Viwanda, nimesema huwezi kuwa na viwanda bila kuwa na malighafi. Moja ya malighafi ni umeme wa bei nafuu ambao upo unapatikana kwa wakati wowote, ndicho Serikali ya Awamu ya Tano inafanya, kuhakikisha kilimo chetu kinaleta tija katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao yetu ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo hayo, hatujaisahau Wizara ya Kilimo na bajeti nzima ya maendeleo, ndiyo maana mwaka huu tukiangalia kitabu hiki cha bajeti ya kilimo kwenye bajeti ya maendeleo tumeongeza bajeti ya maendeleo kwa asilimia 46. Hii ni kwa sababu tunajali na tunathamini kilimo chetu kwenye mnyororo mzima kuanzia uzalishaji mpaka kwenye mazao yake ya mwisho.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulisemea mchana wa leo ni kuhusu VAT refund. VAT refund sote tunafahamu kwamba Taifa letu liliumizwa kwa kiwnago kikubwa, tunaendelea kulipa madeni haya ya VAT refund…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naomba niseme tu kwamba tayari deni la bilioni 20.8 limeshahakikiwa na linalipwa ndani ya mwezi huu na bilioni 28.8 nalo pia tunamalizia uhakiki wake tunaenda kuwalipa Watanzania na ambao wanatudai ndani ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba nirejee kusema naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)