Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie hoja hii ambayo iko mezani ya Wizara ya Kilimo, na nianze kwa kuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na machache ambayo yanakwenda kusaidia katika hatua ambayo Serikali inajaribu kuchukua katika kuhakikisha kwamba katika uboreshaji wa kilimo na namna ambavyo tunawezesha Wakulima wetu kuweza kupata ardhi ya kutosha na kuweza kuzalisha kama ambavyo wengi wanasema kilimo kinachukua karibu zaidi asilimia 65 kwa maana ya wanaohusika na kilimo hicho.

Mheshimiwa Spika, nianze tu kwa kusema kwamba nia na dhamira njema ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakipa kipaumbele kilimo, tumeanza na ile hatua ya kuanza kunyang’anya yale mashamba ambayo yametelekezwa ili baadaye yaweze kupangiwa matumizi mazuri katika kilimo kama ambavyo Serikali imekusudia.

Mheshimiwa Spika, tuna mashamba zaidi ya 45 ambayo yamebatilishwa na mashamba haya ambayo tayari yamebatilishwa baadhi yake yameshapangiwa pia shughuli hiyo tukianza na shamba namba 217/1-6 la Mkulazi ambalo limetengwa kwa ajili ya kilimo cha miwa. Pia tunalo shamba lingine la Makurunge Bagamoyo namba 3561/1 nalo limetengwa kwa ajili ya kilimo cha miwa.

Mheshimiwa Spika, pia hatukuwaacha nyuma wananchi wetu ambao nao pia wamekuwa na tatizo kubwa katika suala zima la ardhi. Wote ni mashahidi kwamba katika Mkoa wa Morogoro nadhani unaongoza katika migogoro ya ardhi ambayo sehemu kubwa ni masuala ya maeneo ya kilimo. Kule nako katika yale mashamba yaliyofutwa tumefuta shamba namba 32, 33, 34, 35, mpaka 36, yaliyoko
Mvumi pamoja na mashamba namba 4, 5, 8 na 10 yaliyoko Msowelo lakini, mashamba haya yamerejeshwa kwa wananchi ili waendelee na kilimo kwa sababu lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunazalisha kwa wingi. Tunapozungumzia Tanzania ya Viwanda pia tuweze kupata malighafi itakayokwenda katika viwanda hivyo. Haya yanafanyika ili kuweza kuona ni jinsi gani tunaweza tukapeleka nguvu zaidi katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi maelekezo ya Serikali pia yalishatoka kwenda katika Halmashauri zetu zote, waliombwa kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo na hasa kwa ajili ya vijana ambayo yangeweza kutumika kwa kilimo na masuala mengine, lakini mpaka dakika hii ninapoongea ni Halmashauri chache ambazo zimeweza kuzingatia hilo. Hili lingeweza kusaidia zaidi katika kuwawezesha vijana, lakini pia kuwaweka katika maeneo hayo wangeweza kulima kilimo chenye tija. Kwa sababu wengi tunaotegemea mbali na graduates ambao wanamaliza, lakini pia hata wale walioko katika maeneo yetu ya Halmashauri, wengi wamekuwa wakiwezeshwa na Wizara husika, Wizara ya Kazi, ambayo imekuwa pia ikisaidia katika kuhakikisha kwamba vijana wengi wanapewa elimu kwa ajili ya kilimo, kwa ajili ya ufugaji na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Spika, niziombe pia Halmashauri zetu, zizingatie maelekezo ya Serikali yanapotolewa, kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunainua kilimo. Kilimo kina mambo mengi ndani yake, kama hujawatambua wakulima wako kama ambavyo mtoa hoja amesema, utashindwa pia kujua wanahitaji pembejeo kiasi gani, utashindwa kujua mkwamo wao uko wapi, lakini utashindwa kujua pia, scale ya kilimo ambacho wao wanafanya, wanafanya kilimo cha biashara, wanafanya kilimo cha chakula au wanafanya kilimo gani. Ukishawatambua maana yake ni kwamba pia utakuwa unawatolea huduma kwa hao Maafisa Ugani tunaowazungumza, tunaweza kujua Afisa Ugani mmoja anahudumia wakulima wangapi? Sasa kama usipojua idadi ya wakulima, obvious hata kujua idadi ya Maafisa Ugani wanaotakiwa inaweza ikawa ngumu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kikubwa hoja ya Serikali ya kuanza kuwasajili wakulima inasaidia pia katika kuwatambua na kujua mahitaji yao ya ardhi ni kiasi, lakini pia katika suala zima la kuona kwamba tunaongeza ardhi ya kilimo, tunao wawekezaji ambao tunasema ni wawekezaji kama ambao wameshindwa, ambao wametelekeza mashamba yao, wako zaidi ya mia moja, lakini wengi wao pia wamekopea mashamba hayo. Wamekopea mashamba lakini wameenda kuendeleza maeneo mengine.

Sasa Serikali pia inapitia hawa wote kuweza kujua ni wangapi na wako wapi ili tuweze kuwanyang’anya yale mashamba yaweze kufanya kazi ile iliyokusudiwa halafu wao watafute dhamana nyingine ya kuweza kuweka katika mikopo yao.

Mheshimiwa Spika, hayo yote yanafanyika katika dhamira njema ya kuhakikisha kwamba Sekta hii ya Kilimo inaimarishwa na inakuwa pia ni chachu katika mwelekeo wa Serikali wa Tanzania ya Viwanda ili tuweze kuwa na maeneo ya uzalishaji yalio mengi na yanayozalisha kwa tija.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)