Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri kwa kazi nzuri sana wanayoifanya kwenye sekta hii. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kati ya maeneo muhimu sana ambayo nilitaka nichangie kwa maslahi ya muda ni uelewa ambao tunatakiwa wote tuwe nao. Moja, Mheshimiwa Waziri ujue kwamba hakutakuwa na Mapinduzi ya viwanda nchini kama hatutakuwa na Mapinduzi ya kilimo ni kwa sababu asilimia 65 ya malighafi yanayokwenda viwandani yanatoka kwenye kilimo. Pili, hatutakuwa na mapinduzi ya kilimo kama hatutakuwa na mapinduzi kwenye mfumo wa kufikisha pembejeo kwa wakulima wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu vizuri, wakulima wetu wengi wapo vijijini, na pembejeo za kilimo kwa maana ya mbolea, mbegu bora na viuatilifu vinapatikana mjini. Ili huyu mkulima aweze kuzalisha kwa tija ni lazima atumie mbolea nzuri, mbegu bora na atumie viuatilifu. Kama hivi vyote vinaendelea kupatikana mjini maana yake huyu mkulima mdogo ni lazima asafiri kupata hii huduma, na unamuongezea gharama za uzalishaji. Akishazalisha zao Lake, anakuja kuliuza kwa gharama kubwa kwa sababu anataka kufidia gharama.

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao Serikali unaufanya ni mzuri, wa kuhakikisha kwamba vijijini kunakuwa na maduka madogo madogo ya wauza pembejeo. Maduka haya vijijini yatauza mbolea, mbegu bora na viuatilifu.

Mheshimiwa Spika, changamoto tunayoipata kwenye hii sekta ya kilimo ni gharama za kufungua haya maduka vijijini, wajasiliamali wengi vijijini wamejengewa uwezo na uelewa wa umuhimu wa kuuza pembejeo vijijini ili mkulima mdogo aweze kupata huduma kwa karibu.

Mheshimiwa Spika, sasa vyeti vinavyotokana na kupata hicho kibali ni gharama kubwa sana. TOSIC peke yake wanataka 100,000, TFRA wanataka pia fedha lakini TPRA wanataka 320,000, TFDA wanataka 100,000, kabla hujafungua duka la pembejeo kijijini, lazima uwe na shilingi zaidi ya 600,000; hapo hujaweka shelves dukani, hujanunua bidhaa. Sasa mjasiriamali gani wa kijijini atakuja kuwekeza kwenye hii biashara ili kumsaidia mkulima mdogo kupata huduma kwenye sekta hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ili tupate mapinduzi ya kilimo, Mheshimiwa Waziri azipitie tena hizi tozo na gharama, ikiwezekana aziondoe, kama haiwezekani basi zipunguzwe kwa kiwango ambacho kitamsaidia mjasiliamali mdogo aweze kuwa msaada kwenye hii value chain ya inputs kwa maana ya pembejeo, tusipofanya hivi tutaendelea kuwatesa wakulima na hatutapata majibu. Ninayo mifano halisi, Kigoma peke yake zaidi ya wajasiriamali 159 wamejengewa uwezo lakini wameshindwa kufungua maduka kwa sababu hawajakidhi viwango vya kuwa na vyeti kwa sababu ya gharama.

Mheshimiwa Spika, ukienda Mkoa wa Kagera wakulima 461 wamejengewa uwezo kupitia Shirika la Agra, lakini ni wakulima 139 tu wameweza kulipia gharama hizi na kufungua maduka vijijini, tutapata wapi mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kuwekeza kwenye mfumo wa pembejeo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)