Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kutoa pole kwa Chama cha Mapinduzi, hususan Chama cha Mapinduzi Zanzibar kwa kifo cha Mzee wetu Shamhuna, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema na msiba wake unaendelea kutukumbusha kwamba, sisi wote ni udongo na tutarudi kuwa udongo. Kwa sababu hiyo, tuenende kwa unyeyekevu na hekima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nieleze tu kwa sababu nina dakika 10 kwamba, naunga mkono Mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu zao la korosho kuanzia aya ya 80 mpaka aya ya 92 na mapendekezo yote hayo kuanzia ukurasa wa 23 na 26, yahesabike vilevile kama ni sehemu ya mchango wangu ili nijielekeze kwenye nini sasa tufanye baada ya kadhia nzima ya korosho ambayo kwa ukubwa wake, hii kashfa ya korosho inafanana na EPA, inafanana na Escrow, inafanana na Richmond, inafanana na kashfa zenye sura ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya namna hii tunapaswa turejee kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Ibara ya 63(20), imetamka kwamba, Bunge ndio chombo kikuu ambacho kwa niaba ya wananchi kina wajibu, sio tu wa kuishauri Serikali bali pia, kuisimamia Serikali. Hapa tunahitaji kuisimamia Serikali na kutaka uwajibikaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunapotaka uwajibikaji wa Serikali Kiongozi wa Shughuli za Serikali hapa Bungeni, kwa Katiba ya nchi yetu, Ibara ya 52 inamtamka kwenye Ibara Ndogo ya (2) kwamba, ni Waziri Mkuu na Ibara Ndogo ya (1) inasema, sio tu hapa Bungeni Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku kwa kazi za shughuli za Serikali za kila siku.

Mheshimiwa Spika, sasa kama hili suala la korosho kwa siku zote hizo limeendelea na kashfa ya uozo wa namna hii, ni wakati sasa Waziri Mkuu katika majumuisho ya Wizara hii afike Bungeni atangaze kujiuzulu yeye mwenyewe nafasi yake kabla hajawajibishwa. Hii ndio italinda dhana ambayo Mheshimiwa Mwakyembe alisimama siku chache zilizopita akimjibu Mheshimiwa Msigwa wakati aliposema Waziri Kabudi anatakiwa kujiuzulu, Waziri Mwakyembe alisimama kwa niaba ya Serikali, kwa niaba ya Waziri Mkuu akasema jambo hili ni la uwajibikaji wa pamoja, sasa uwajibikaji wa pamoja uonekane ukitanguliwa na Waziri Mkuu mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la uwajibikaji wa pamoja linaongozwa na Katiba yetu, Ibara ya 53(2), nitanukuu inasema:

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano chini ya mamlaka ya Rais itakuwa ndio itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya sera za Serikali kwa ujumla na Mawaziri,” Mawaziri nasisitiza, “Mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja Bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kadhia hii imewagusa Mawaziri wengi kidogo, imewagusa wale walioondolewa mwanzoni, wakati Rais alipotoa kauli akafikia hatua mpaka kusema wale mashangazi kule Kusini watapigwa, wakaondoka baadhi ya Mawaziri. Wakaingia wengine, lakini hawa walioingia badala ya kurekebisha tatizo wamelikuza na kuliendeleza tatizo mpaka hivi sasa tunavyozungumza. Ndipo yanapokuja masuala kama ya Indo Power ambayo pamoja na kuwa Mheshimiwa Profesa Kabudi ndio anaonekana kwenye picha pale mbele, mstari wa mbele, Mawaziri wanaohusika ni Waziri wa Fedha ndio maana Gavana wa Benki alikuwepo, anatakiwa awajibike, Waziri wa Viwanda na Biashara anatkiwa awajibike, Waziri wa Kilimo naona tunamkwepakwepa Waziri huyu eti kwa sababu ni mpya wakati mkataba umesainiwa yeye akiwepo anatakiwa kuwajibika, Waziri wa Mambo ya Nje anatakiwa kuwajibika, Waziri wa Utawala Bora ambaye Usalama wa Taifa uko chini yake wenye wajibu wa kuishauri Serikali anatakiwa kuwajibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mzigo wote huu wa uwajibikaji, lazima Waziri Mkuu ndio awe minara wa kwanza wa kuwajibika kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri Mkuu. Waziri Mkuu akishajiuzulu maana yake… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa John Mnyika kwa mtu ambaye hajui nini kimekuwa kikiendelea, ikiwa ni pamoja na mimi mwenyewe, tungependa kujua wawajibike kwa sababu gani? Endelea tu.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze na hili la Indo Power ambalo mnataka kusema as if kwa sababu, hawajauziwa korosho sio shida. Kwenye uchumi kuna kitu kinaitwa opportunity cost, gharama ya fursa; yaani kwamba, walituahidi kununua korosho laki moja na tukasaini na hawakununua na korosho zikakaa kwenye maghala mpaka zimeoza, tunavyozungumza hivi sasa tumekosa mapato ya nje. Hii gharama ni kubwa ni ya yale makosa yanayopelekwa Mahakamani unasikia, huyu awajibike kwa uzembe na kuisababishia hasara Serikali kwa uhujumu uchumi, hao wanatakiwa kuonesha uwajibikaji, ili sasa wale walioishauri Serikali vibaya, kama kuna watu nyuma walioishauri ukiondoa hawa Mawaziri, nyuma ya Serikali hawa nao wanapaswa kuwajibika.

Mheshimiwa Spika, hili ni suala la Kikatiba tena…

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nazungumza nikiwa nimetoka Ruvuma, Mtwara na Lindi kwenye shughuli za chama na nimekutana na wakulima. Wanapozungumzia korosho huwa zina muda wake, muda ukipita korosho zinasinyaa, zikishasinyaa zinakosa soko na ndiyo maana Serikali…

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, taarifa…

MHE. JOHN J. MNYIKA: imeanza kuwarudishia wananchi, naomba niendelee…

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, mimi naomba niendelee kwa sababu anani…

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika pokea taarifa hiyo.

MHE. JOHN J. MNYIKA: …wananipotezea tu muda wangu.

Mheshimiwa Spika, ninachokisema ni kwamba kuna wakulima wanarudishiwa korosho zao wanaambiwa Serikali haizitaki tena zipo chini ya kiwango kwa sababu Serikali inajua haziuziki nje inaanza kuwarudishia wakulima. Kuna wakulima hawajalipwa, kuna mambo mengi nisipotezwe nje ya mstari naomba niendelee…

MHE. KATANI A. KATANI: Taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Katiba ya nchi…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, taarifa…

SPIKA: Naomba tumuache aendelee, endelea Mheshimiwa…

MHE. KATANI A. KATANI: Tuweke clarification hili…

SPIKA: Dakika zako zitavurugika, endelea.

MHE. KATANI A. KATANI: Nilitaka nijibu korosho wapi zimeoza maana najua.

SPIKA: Mheshimiwa Katani muachie, za kwako ulizitumia vizuri, ungeongea.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, Katiba ya Nchi yetu Ibara ya 54 inayozungumza kuhusu Baraza la Mawaziri ibara ndogo ya 3 inasema bila kuathiri masharti yaliyomo Ibara ya 37 ya Katiba hii, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo cha kumshauri Rais juu ya masuala yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake. Inaendelea mbele, kwa ajili ya muda nisiinukuu yote.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba huu uozo wote wa korosho, kuanzia ushauri wa kwanza wa kumshauri Rais kwamba korosho zikusanywe na zibebwe na jeshi na kuleta azimio hapa Bungeni la kumpongeza Rais; huu uamuzi Baraza la Mawaziri lilimshauri Rais vibaya, Baraza la Mawaziri linastahili kuvunjwa. Mpaka uamuzi wa kwenda mbele kuitafuta hiyo Kampuni ya Kenya ya Indo Power kwamba itanunua korosho…

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: …za laki moja. Baraza la Mawaziri limemshauri Rais vibaya, Baraza la Mawaziri linastahili kuvunjwa na ili livunjwe Waziri Mkuu ajiuzulu…

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika…

MHE. JOHN J. MNYIKA: …na kama hajiuzulu tutaleta hoja ya kutokuwa na imani naye ili kuiwajibisha Serikali.

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika pokea taarifa ya Mheshimiwa Innocent.

T A A R I F A

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA – NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mnyika tunamsikiliza lakini ukiangalia…

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika bado dakika zako, hii ni kengele ya kwanza eeh, endelea.

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA – NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ukiangalia hoja anayojenga Mheshimiwa Mnyika anai-deduct kutoka kwenye kuoza kwa korosho. Taarifa tumempa kwamba hakuna korosho iliyooza kwa hiyo kwa sababu ana-deduct hoja yake kutoka… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA – NAIBU WAZIRI WA KILIMO: kwenye kuoza kwa korosho na si kweli, hoja yake haipo-valid ni void. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka nimpe taarifa, una-derive hoja yako kutoka kwenye kuoza kwa korosho lakini hakuna korosho ambayo imeoza.

SPIKA: Ahsante sana, wanasemea neno kuoza, Mheshimiwa Mnyika unapokea hiyo taarifa? Bado dakika zako mbii.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Hivi mtu akileta korosho yenye kiwango halafu hiyo korosho ikawekwa kwenye maghala ikaharibika ikawa chini ya kiwango, anarudishiwa amefanya nini?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. Hoja yangu siyo ishu ya kuoza peke yake na kuna taarifa hapa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mbona taarifa za huku unazikataa, taarifa za huku unazikubali? Hiyo ni double standard, mkaribishe tu huyu anatoka kwenye eneo la korosho aseme kama korosho haziozi au la atoe ufafanuzi. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: naomba umpe taarifa basi, pokea taarifa hiyo kuhusu korosho kuoza kutoka kusini.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea. Hoja siyo jambo la korosho tu kuwa chini ya kiwango ambayo tunakubaliana na kwamba CAG akachunguze tasnia nzima ya korosho…

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika…

MHE. JOHN J. MNYIKA: …lakini hoja nyingine hapa kadhaa…

SPIKA: Subiri Mheshimiwa Mnyika. Nilikuwa nalinda dakika zako, nakulinda wewe mwenyewe nikiamini una cha kusema. Nilifanya hivyo kwa sababu huyo unayetaka atoe taarifa amepata dakika zake saba za kuzungumza hapa, unanielewa eeh?

Eeh subiri, amepata dakika zake za kuzungumza. Kuna kuhusu utaratibu huku sijui upande gani, Mheshimiwa Naibu Waziri.

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa Kanuni ya 64(1) (a); kuhusu kudanganya. Kwanza mimi ni mkulima wa korosho, yeye si mkulima wa korosho. Korosho ina utaratibu wake, ina muda wake maalum unaofikiwa na kuitwa kwamba imesinyaa, tulisema na tukaiweka katika utaratibu ukaitwa unyaufu. Katika muda huo ambao tumezikusanya korosho mpaka hii leo, hamna uwezekano wa kusema korosho imeoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena, mimi ni mkulima wa korosho, ninazo kwangu korosho na ninazo za kwangu mwenyewe pia vilevie korosho. Kwa hiyo suala la kusema kwamba korosho imeoza, huo ni uongo mkubwa na aache kupotosha na urongo wake huo. (Makofi)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Selasini nimekuona Chief Whip.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Mheshimiwa Mwambe ukishamuona Mheshimiwa Selasini amesimama au unashinda naye? Kaa Mheshimiwa Selasini aongee Mheshimiwa Mwambe. (Kicheko)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Selasini ni bosi wako bwana anaposimama mnatakiwa kuheshimiana kidogo, ahsante Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, tumemuomba.

Mheshimiwa Spika, tusipotoshe hili jambo, tukiwa sisi kwenye kamati tumeletewa malalamiko, wanasema kwamba wanaomba kujenga maghala ya kuhifadhia korosho kwa sababu storage facilities zetu ni transit. Kwa hiyo, korosho ukiweka muda mrefu kwenye hayo maghala zinaharibika, they go bad. Na kwa kuthibitisha hili SIDO Mtwara waliamua kutunza korosho zilizobanguliwa ili wapate ile room temperature (AC) walikuwa wanawasha, wamewatoa wafanyakazi wote wakawa wanawasha AC, ninaweza kuthibitisha ndani ya hili Bunge na tulipowaambia wakazitoa. Wanasema wanajenga maghala ya kuhifadhia korosho zilizobanguliwa Dar es salaam, Kurasini, kazi hiyo haijafanyika. Ndiyo maana tunaomba CAG aende akakague aje atueleze hapa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwambe tumeshakusikia. Issue ni kwamba anasema waliambiwa kwenye Kamati kwamba ukiweka korosho kwa muda mrefu katika maghala zinaweza kuharibika, kitu chochote ukikiweka katika muda mrefu kitaharibika. Anachosema ni kwamba katika muda huu tangu zimechukuliwa mpaka sasa hazijaharibika, katika muda huu, lakini katika muda mrefu huo mnaosema inaweza hilo likatokea.

Na kinachozungumzwa hapa ni terminology tu ya neno kuoza, kwa hiyo msemaji anaweza akarekebisha neno lake akaweka sawa na kwa sababu hakuna zilizooza, kwa hiyo maana yake hoja ya Mnyika imekufa, ndiyo wanachosema wenzako. Nakurudishia umalizie maana bado dakika moja tu hapo. (Makofi)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, kama hilo neno linawakera sana naliondoa lakini hoja yangu mimi si suala la kuoza peke yake; nimesema kuhusu mkataba wa Indo Power, kuhusu Serikali kukosa mapato nje (forex), kukosa mapato kwa ujumla wake ambayo tungeyapata kwenye mauzo ya korosho. Mambo ni mengi kweli kweli ambayo kwa pamoja yanataka kama CAG hamumruhusu kuchunguza basi Kamati Teule ya Bunge iundwe iende kuchunguza na hatua zichukuliwe. Wakati tukiendelea na uchunguzi wa Bunge, Serikali iwajibike Waziri na Mawaziri wajiuzulu na kama hawajiuzulu tutaleta hoja ya kutokuwa na imani na Serikali, ahsante sana. (Makofi)