Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami niungane na Wabunge wenzangu kuzipongeza Kamati zote zilizohusika; Kamati ya Afya, Kamati ya Elimu, Kamati ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo kwenye suala dogo tu la elimu. Asilimia 90 ya Watanzania wanaopeleka watoto wao shule, shida yao kubwa ni mtoto kumaliza shule na kupata ajira. Naona kwenye majumuisho yote, sioni mahali panapoongelewa suala ajira. Suala hili la ajira ni lazima tuendelee kulijadili kwa mapana makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwona Mheshimiwa Waziri anaendelea kufunga vyuo vingi ambavyo havikidhi mahitaji ya kielemu. Ushauri wangu, badala ya kuvifunga vyuo, Mheshimiwa Waziri alete Muswada humu Bungeni ili mtu akitaka kufungua chuo au kusajili wanafunzi ahakikishe asilimia 80 ya wanafunzi wamepata ajira ndiyo a-qualify kupata leseni ya chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, qualification ya chuo isije ikawa majengo kwa hali ilivyo sasa hivi. Mtu kama aweza kutoa ajira asilimia 80, yeye mwenye chuo ndio akatafute ajira ili hata kama mtu ana chuo chini ya mti, watu wetu wanapata ajira, apewe leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu sasa hivi ni kweli kuna utapeli mkubwa sana kwenye vyuo. Watu wetu wanalima, wanapika gongo, wanachimba madini kwenye matope, wanampatia mtu wa chuo kweli anawapa karatasi. Kama sheria itakuja hapa kwamba ili wewe uanzishe chuo u-confirm kwetu kwamba wanafunzi unaowachukua lazima wape kazi. Wasipopata kazi, ushitakiwe kwa kesi ya utapeli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo Mheshimiwa Waziri ataleta huo Muswada Bungeni, unaweza ukatupunguzia mgogoro na watakuja watu wengi sana kufungua vyuo ili kusudi qualification ya chuo isije ikawa majengo. Hata kama mtu atasoma kwenye jengo zuri, kama hakupata kazi inamsaidia nini? Waheshimiwa akina Nelson Mandela na akina Mugabe wamesoma magerezani, lakini wamekuja kuwa viongozi leo na wote tunawatukuza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hana sababu yoyote ya kugombana na wenye vyuo; alete Muswada Bungeni, tupitishe Muswada, mtu yeyote anayetaka kuanzisha chuo; Waganga wa Kienyeji wanafundishwa Uganga, watu wanaendelea vizuri na Waganga tunawaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaye humu Mheshimiwa Karamagi, Waziri wa Nishati, ni Mganga wa Mifupa. Alisoma chuo gani? Ni Mganga wa Mifupa! Kwa hiyo, nakuomba … (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Kalemani.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Karamagi. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Naamini ulimaanisha Mheshimiwa Kalemani, siyo?

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kalemani, yah, yah, ni Mheshimiwa Kalemani. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kalemani ni Mganga wa Mifupa na anatibu na anaponyesha, lakini hakusoma kwenye chuo chenye majengo, alisomeshwa kwenye Chuo cha Waganga wa Kienyeji na ni Mganga. (Makofi/Kicheko)

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliongea bila mpangilio)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana wenzetu hawa wa mitaala ya shule; watu wanaikwepa VETA sasa hivi, naona Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani wanazungumzia suala la VETA, wananchi hawaitaki VETA kwa sababu VETA unaenda kujifunza kupaka rangi miaka mitatu, inawezakana kweli kupaka rangi miaka mitatu? Haiwezekani! (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani kujifunza kupaka rangi miaka mitatu. Mtu kama ameelewa kupaka rangi na soko halihitaji cheti, kwa nini siku nne asiondoke akaendelee na shughuli za zake? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri afungue uwazi, watu wote watakubali. Kwa mfano, kutengeza simu; mtu aruhusiwe kutengeneza simu, akishafahamu siku nne, mruhusu aende akaendelee na shughuli zake. Maana soko haliulizi cheti. Hakuna mtu anaenda kutengenezewa simu kwa kuulizwa umesoma wapi na cheti kiko wapi? Unapeleka simu yako wanakutengenezea. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu atusaidie sana ili kupunguza huu mgogoro. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la hospitali, tunaishukuru sana Serikali kwa hospitali, zahanati kila kitu kipo. Tatizo kubwa lililopo ni kwenye matibabu hasa X-Ray na vitu vingine. Ukienda benki kuuliza statement au kuuliza balance ya pesa, hawakuchaji gharama ya kompyuta, kwa sababu ile kompyuta ndiyo investment ya benki. Sasa inawezekanaje nikienda hospitali unanichaji gharama ya X-Ray? Kwa hiyo, X-Ray ni investment ya hospitali, maana inamsaidia Daktari kujua ugonjwa wangu, haiwezi kuwa package ya kunichaji mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea, wewe ukifika unaumwa mle ndani, hawa wana X-Ray karibu nane; kuna Ultrasound na nyingine. Unapelekwa zote sehemu kumi, halafu unaletewa bill unaambiwa ni shilingi 300,000/= halafu unaambiwa nenda kanywe maji mengi. Inawezekana kweli! Haiwezekani na hakuna mtu anaweza akambishia Daktari. Nani humu anaweza akambishia daktari? Haiwezekani!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Afya na Kamati yako, tunaomba mtengeneze mamlaka kama EWURA ambayo itadhibiti bei za dawa na bei za vipimo. Haiwezekani sisi tunadhibiti mbolea, tunadhibiti mafuta lakini hatuna mamlaka inayodhibiti bei ya vipimo na bei ya dawa. Haiwezekani! Maana yake sasa hivi ni tatizo kubwa kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli jamaa zetu hapa walikuwa wanalalamika kuhusu suala la maiti; kuna matatizo makubwa sana. Mtu amefariki, acha ile issue ya bill, kwa sisi kama Waislamu, ukifika pale wanakwambia tumeshaihudumia maiti, tunakudai shilingi 300,000/=. Sasa unashangaa, sisi tunataka kuzika leo, wanakupa bill kwamba wameshaihudumia maiti. Sasa wewe hujui umehudumiwa nini? Kwa kweli Mheshimiwa Waziri wa Afya, tunaomba sana sana, hasa sisi Wabunge ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Afya ajaribu sana kufikiria suala hilo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho kabisa ni usajili wa Zahanati. Medical Assistant akitaka kusajili leo Zahanati, shida anayopata matokeo yake wanazifunga. Daktari aliyestaafu akitaka kusajili hospitali, anashindwa; lakini Mganga wa Kienyeji anasajili ndani ya dakika kumi na anaruhusiwa kulaza wagonjwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inaingiaje akilini? Wote humu mnafahamu, mmesoma na Madaktari wamo, kweli Mganga wa Kienyeji anasajili dakika kumi, Medical Assistant au daktari bingwa mstaafu hawezi! Anapata shida ngumu sana na wote wanazifunga. Leo watu wa mionzi wanazunguka wanaendelea kufunga Zahanati, lakini Waganga wa Kienyeji wanaendelea kulaza wagonjwa. Itawezekanaje? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli ni kitu ambacho kweli kinaingia akilini! Tunaomba sana Kamati ya Mheshimiwa Serukamba, afikirie kabisa shida ya wananchi wanayoipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo, nashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)