Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kwa hatua hii kwa sababu mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyazungumze leo yana itifaki kubwa sana katika mustakabali wa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru wewe kwa kuendesha mjadala huu vizuri, na unaweza ukaona pande zote zinaridhika kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi vizuri sana katika masuala yote ya miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, kaka yetu Mheshimiwa Kitandula na Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa Kamati. Lakini kwa aina ya pekee naomba niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kipindi chote cha miaka minne iliyopita, wamekuwa wakitoa msaada mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapoona Wabunge wanakuja kwenye kiti chetu hapa si kwamba wanakuja kuomba misaada au miradi ya umeme vijijini kwa upande wao, mara nyingi huja kutoa ushauri. Na kwa kiasi kikubwa tunawashukuru sana, tumezingatia sana ushauri wenu na ndiyo maana tumefika hatua hii. Waheshimiwa Wabunge kwa kweli tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee sasa kuchangia kwenye mada ya leo. Yapo mambo mengi yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge, lakini kwa sababu ya muda nitaongea kwa ufupi sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu. Katika awamu hii, yako mambo mengi sana ambapo Tanzania itakumbukwa katika vitabu vya Watanzania kwa historia ya miaka mingi ijayo. Kuna miradi mikubwa sana ya vielelezo ambayo imetekelezwa na kila mtu ni shahidi. Mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji almaarufu Julius Nyerere, kama ambavyo mnafahamu, unaenda kuondoa kero zote zilizokuwepo katika masuala ya undeshaji wa nishati hapa nchini. Kwa hiyo, ni hatua kubwa sana Awamu ya Tano imefanya katika jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nami nawashukuru Waheshimiwa Wabunge jambo hili mnalifahamu. Jambo la pili katika hili, tumeingia katika historia ya kidunia. Mradi huu tumekuwa tukisema mara zote na ninapenda nirudie tu, ni mkubwa sana katika mabwawa yote duniani. Kwa mara ya kwanza tunaingia kwenye kitabu cha kidunia cha kutekeleza miradi mikubwa kama hii. Ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kabla ya mwaka 2015 tulikuwa na uhaba mkubwa sana wa umeme. Tulikuwa na upungufu wa umeme takribani Megawati 270, ndiyo maana tulikuwa tuna mgao wa umeme, kwa maana ya kugawiana kidogo tulichokuwa nacho. Kwa leo mnaona kuna mabadiliko makubwa sana, tuna zaidi ya Megawati 280 mpaka 320 kwa siku. Hii ni hatua kubwa sna imefanyika kufikia hatua hiyo.

Mheshimiwa Spika, tunatarajia sasa kwenda kwenye jambo kubwa sana la pili la kihistoria kwa nchi yetu; kuendesha treni itakayotumia umeme katika mwendo kasi. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuanza kutumia umeme, kuendesha treni ya mwendo kasi. Tumetenga takribani ya Megawati 70 na treni kama mnavyojua, itakwenda umbali wa speed kubwa. Huu ni umbali mrefu sana, tunajenga mradi huu kwa umbali wa kilometa 160 na gharama yake ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, napenda niseme tu kwamba haya ni mabadiliko makubwa ambayo hayatasahaulika. Ingawaje halijajadiliwa hapa, lakini niseme, haya masuala mawili katika miaka miwili ijayo mradi mkubwa utakamilika Juni, 2022, na huu mradi wa SGR utakamilika hivi karibuni ikiwezekana mwakani, mtaona matokeo yake jinsi nchi itakavyopaa kiuchumi na tunasema Tanzania inaweza ikawa ni Tanzania ya miaka zaidi 40 kwa mfano wa nchi za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye hali ya umeme nchini. Ni kweli hali ya umeme imeendelea kuimarika sana. Nyote ni mashahidi, wote mliokuwa mnapita Kariakoo, mliokuwa mnapita Manzese, mlikuwa hamwezi kupokea sumu kwa wakati huo kwa sababu ya kelele za majenereta. Leo hii Awamu ya Tano imezima majenereta, unaweza ukaongea na simu wakati wowote, maeneo yoyote bila kuwa na wasiwasi. Ni kielelezo rahisi sana lakini ni rahisi kukiona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la msingi kabisa, toka mwaka 2015 mtandao wa umeme nchini ulikuwa ujafikia asilimia 70, leo tunapoongea hapa katika nchi yetu tumeshatandaza umeme kwa umbali wa kilometa 130,000 nyaya kote nchini zimeshapita, hakuna mahali nyaya ya umeme haijafika kwenye nchi hii. Ni jambo ambalo ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na idadi ya nguzo kwa wakati huo milioni 1.1, leo tuna idadi ya nguzo zilizosimikwa na zenye umeme milioni 3.3, ni jambo kubwa sana. Tulikuwa na transfoma takribani 65,000, leo tuna transfoma 142,000. Ni kazi kubwa sana zimefanyika.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwa sababu ya muda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia ya mwisho.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mambo ya msingi ambayo ningependa nizungumzie hapa ni umeme Vijijini. Mwaka 2005 tulikuwa na umeme katika vijiji 231; mwaka 2008 tulikuwa na umeme katika vijiji 561, mwaka 2015 tulikuwa na umeme katika vijiji 218; leo tunapoongea kwa heshima ya Watanzania wote, tuna vijiji takribani 8,674 vina umeme hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jambo hili unaweza ukaliona ni jepesi. Kwa Afrika sisi kwa sasa hivi ukiondoa Nigeria ambao wameshafikia asilimia 72 na wanaelekea 75, sisi tunategemea kufikia asilimia 76 mwakani na kuipita Nigeria. Kwa hiyo, tunaweza tukaanza kuongoza katika umeme Vijijini. Jambo hili ni kubwa sana na tunaomba sana tuipongeze sana Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na kupeleka umeme katika vijiji nilivyotaja, nchi yetu ina takribani ya Wilaya 180 na kitu; hivi sasa Wilaya 34 tumekamilisha kupeleka umeme katika vijiji vyake vyote. Wilaya hizo tutapeleka umeme kwenye Vitongoji tu, lakini kama Wilaya tumeshakamilisha. Hata kwako, vile Vijiji vya Saigoni, Makutupa pamoja na Soni na Laiboni, tumeshakamilisha na kwa kwako tutapeleka Vitongoji tu. Kwa hiyo, niseme kwa niaba ya Watanzania, nawashukuru sana wananchi kwa kukubali hili. Kazi kubwa imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hilo, umeme tunaopeleka katika Vitongoji kwa kweli ni mara ya kwanza mnashuhudia, hakuna nyumba ya Mtanzania inayoachwa bila kupelekewa umeme. Nyumba za aina zote wananchi wanafurahia; wa maisha ya chini, kati na juu wanafurahia katika mpango huu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kalemani.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, la mwisho LNG…

SPIKA: Nakushukuru sana, ahsante sana.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)