Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, John Pombe Magufuli kwa kuanza kutekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2014, hasa kwa kuondoa au kwa kufanya elimu ya msingi na sekondari iwe elimu bure. Hii imewasaidia Watanzania wengi ambao walikuwa wanashindwa kupeleka watoto wao shule za msingi na sekondari kuweza kupata elimu. Kwa hiyo, imeongeza access to primary and secondary school education. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto ambazo Wabunge wameendelea kuzisema, lakini kwanza tumefungua access, tumewawezesha Watanzania wote waweze kupata fursa ya kupata elimu ya shule ya msingi na sekondari. Hizi changamoto nyingine tutaendelea kuzitatua kadri muda utakavyokuwa unaendelea. Kwa hiyo, lazima uanze kwanza kuweka fursa, lakini baadaye katika fursa unakuwa na changamoto nyingine nyingi ambazo tumesema kuna changamoto za miundombinu, changamoto za resources mbalimbali ambazo tutaendelea kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Elimu kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hii, namwamini, yupo makini na atatufikisha pale ambapo tunatakiwa tufike, lakini pia nimpongeze Naibu wake wa Elimu, Mheshimiwa Stella Manyanya na nimpe pole kwa msiba aliopata wa mama yake. Mungu aendelee kumrehemu na aendelee kumpa nguvu katika kipindi hiki ili arudi kutekeleza majukumu muhimu sana ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika nianze kusema jambo moja linalowakera sana Walimu hasa madai ya Walimu. Pamoja na mambo mengine yote jambo la madai ya Walimu, ndiyo pengine yanachangia kuathiri kiasi kikubwa kufisha elimu au inachangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa elimu. Walimu wanapokuwa wanadai nyongeza ya mishahara, wanapodai kupandishwa madaraja, hii inawakatisha tamaa. Kwa hiyo, muda mwingi wanakuwa wanawaza kuongezewa mishahara, muda mwingi wanawaza madai yao mbalimbali na changamoto mbalimbali, kwa hiyo, wanaenda kazini wakiwa wamevunjika moyo wa kufanya kazi, hivyo hawafanyi kazi vizuri. Pamoja na kwamba tumeajiri Walimu wengi lakini ukifika kwenye mashule tuna Walimu wengi sana, lakini wanaoingia darasani ni wachache, lakini katika wachache wanaofundisha ni wachache sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wengi wanaingia wakiwa wamekata tamaa, wanaingia wakiwa wanawaza maisha, wanawaza mishahara yao, anawaza atarudije nyumbani, anawaza ataishi namna gani kule nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Wizara zinazohusika hasa, Wizara ya TAMISEMI, ihakikishe kwamba madaraja ya Walimu yanapanda kwa wakati na zile stahiki zao kwa maana ya madai yao ya likizo, madai yao ya mishahara mbalimbali na madai mengine yanatekelezwa kwa wakati ili Walimu wawe na moyo wa kufundusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua huwezi kuwa unafanya kazi vizuri zaidi, kama unakuwa na madai mbalimbali, kama unakuwa unalaumu vitu mbalimbali ambavyo hujatekelezewa. Kwa hiyo, niombe Wizara ya TAMISEMI wakishirikiana na Elimu pia, tuweze kuhakikisha kwamba, madai ya Walimu yanalipwa kwa wakati na pia madaraja ya Walimu yanapandishwa kwa wakati. Kuna huu upandishwaji wa madaraja baada ya miaka kadhaa, Walimu wengi wanaokwenda kusoma mara nyingi wamekuwa wakicheleweshewa sana kupanda madaraja yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wamekuwa wakirudi nyuma, akiondoka kwenda kusoma, akirudi anakuta Mwalimu aliyemwacha ambaye ana elimu ndogo kuliko yeye amepandishwa daraja na yeye anabakia nyuma. Kwa hiyo, hili nalo linakatisha sana tamaa Walimu. Kwa hiyo, niombe madaraja ya Walimu yaende sambamba na muda aliyofanya kazi lakini sambamba pia na elimu yake aliyoipata ili angalau tuweze kuwamotisha hao Walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme jambo moja lingine ambalo wamesema Waheshimiwa Wabunge wengi sana juu ya mikopo ya elimu ya juu. Hili nalo limekuwa ni tatizo kubwa wale walengwa ambao wanatakiwa kupewa mikopo wamekuwa hawapati, hasa watoto wa maskini wanaoishi huko Vijijini, wanapewa wakati mwingine asilimia ndogo, asilimia 40 au wakati mwingine asilimia 30 na mwisho wa siku wanashindwa kulipa ada wanabaki wakihangaika tu na wengine imefika mpaka wakati mabinti zetu wanaanza kutafuta njia nyingine za kuweza kupata fedha za kujikimu wanapokuwa chuoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuombe uwekwe utaratibu mzuri kama tulivyosema kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wanafunzi wote watakaokuwa wamedahiliwa kwenda chuo kikuu kwa kuwa wana sifa ya kusoma chuo kikuu wapewe mikopo asilimia 100 na kwa sababu ni mkopo wapewe wote kuliko kuweka haya madaraja kwa maana wengine wanapewa asilimia 80, wengine 70, wengine 60 na 40; hiyo inaleta matatizo na inaleta migomo na maandamano yasiyo na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Elimu alisimamie hili, wanafunzi wote wanaokuwa wamedahiliwa kwenda chuo kikuu, basi wapewe mikopo asilimia 100 ili tupunguze baadhi ya matatizo ambayo wamekuwa wakipata hawa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema na Wabunge wengi wamesema juu ya changamoto za Walimu wa sayansi kwamba Walimu wa sayansi hawapo au wapo wachache, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, tuna upungufu wa Walimu wa sayansi 93 na wakati huo huo tuna upungufu wa Walimu 158 wa shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunasema kwamba, tunataka twende kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda, hatuwezi kwenda kwenye uchumi huo kama hatutakuwa na Walimu wa sayansi wa kutosha. Kwa hiyo, naomba kwanza kabisa tuanze kuwahamasisha wanafunzi wetu toka shule za misingi waweze kupenda masomo ya sayansi. Walimu wa shule ya msingi wawa-encourage watoto waweze kupenda hisabati, waweze kupenda masomo ya sayansi na hatimaye wakifika sekondari waanze kupenda kusoma masomo ya sayansi, ni uamuzi tu, tuwaweze hawa Walimu wanaofundisha, tuwawezeshe Wakuu wa Shule pia ili waweze kusimamia vizuri kuhakikisha kwamba katika shule zao wanafunzi wanafaulu masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest nami ni Mwalimu, nimekuwa Mkuu wa Shule, shuleni kwangu wanafunzi hakuna option, wanasoma masomo yote yale ya msingi, yote yale tisa na wanafaulu zaidi sayansi hata kuliko art. Kwa hiyo, tukiamua tukaweka miundombinu vizuri, tukaweka mazingira mazuri, wanafunzi wanaweza wakafaulu vizuri masomo ya sayansi na hatimaye tukapata wanafunzi wanaokwenda vyuo vikuu kusomea masomo ya sayansi, kwa hiyo, tutaweza kutokomeza jambo hilo, tutaweza kusaidia kupunguza uhaba wa Walimu wa kuanzisha utaratibu wa kuweza kuwahamasisha watoto wa shule za sekondari waweze kupenda masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja kama nilivyosema, la nyumba za Walimu, katika shule zetu nyingi hasa za Kata tuna uhaba mkubwa sana wa nyumba za Walimu, hata katika Jimbo langu tuna uhaba mkubwa sana wa nyumba za Walimu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI watakavyopanga katika ujenzi wa zile nyumba zile 30 ambazo zinachukua Walimu wengi na mimi wanifikirie kule kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule mbili hazina hata nyumba za Walimu kabisa, shule ya Ndinga na shule ya Mrunga kule, kwa hiyo, mnisaidie ili niweze kupata hizi nyumba angalau na Walimu wangu waweze kukaa katika maeneo ya shule na hivyo kufundisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo linguine, wamesema la Mdhibiti wa Ubora, zamani tulikuwa tunaita Kitengo cha Ukaguzi, lakini niseme kwamba Mkaguzi wa kwanza ni mkuu wa shule, tumwezeshe mkuu wa shule aweze kusimamia shule yake vizuri na hatimaye tuwezeshe Kitengo cha Udhibiti Ubora cha Halmashauri au cha Wilaya ili waweze kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao vizuri na Wakaguzi wa Kanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakaguzi hawana fedha kabisa, hawana fedha za mafuta, wanashindwa kwenda kwenye mashule kwenda kukagua. Sasa huwezi kuamini kwamba kama Mkaguzi hawezi kufika kwenye shule kwenda kufannya ukaguzi, je, huko shuleni kutakuwa na kitu gani? Atajuaje ubora kama upo kwenye shule hizo husika. Kwa hiyo, tuombe Wizara husika nazo ziwawezeshe hawa Wadhibiti Ubora kwa maana ya Wakaguzi wetu wa Halmashauri, Wakaguzi wetu wa Knda, lakini pia tumwezeshe Mkuu wa Shule aweze kusimamia vizuri taaluma kwenye shule yake kwa kuwa yeye ni mkaguzi wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iliwekwa ile pesa ya majukumu, sh. 200,000/= kwa Walimu wakuu; Sh. 250,000/= kwa Wakuu wa Shule na sh. 300, 000 kwa Wakuu wa Vyuo. Tukiwapa hizi fedha wataweza kusimamia taaluma vizuri, wataweza kukagua vizuri na kuhakikisha kwamba Walimu wao wanafundisha vizuri. Ilivyo sasa hivi unaweza ukafika Mkaguzi wa Halmashauri au wa Kanda akafikiri Mwalimu anafundisha vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanachofanya darasani kule wanatoa notes, wanatoa kazi, wanasahihishana mle darasani, halafu mwisho wa siku akija Mkaguzi, anaangalia madaftari anakuta kuna mazoezi ya kutosha, anaangalia lesson plan na schemes of work zimekaa vizuri, lakini kumbe kinachoendelea darasani sicho hicho kilichopo kwenye hivi vitabu mbalimbali. Kwa hiyo, tuwawezeshe kwanza Wakuu wa Shule ambao wako jirani na baadaye Idara nzima ya Ukaguzi ili tuweze kuboresha elimu.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.