Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Awali ya yote nawapongeza Kamati zote mbili na Kamati shirikishi zilizokuwemo humu ndani na hasa Kamati yangu ya Ardhi Maliasili na Utalii. Kusema kweli katika miaka hii iliyokwisha, Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii imefanya kazi kubwa sana na ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa namwangalia msemaji mmoja ambaye ni Mjumbe wa Kamati, Mheshimiwa Mch. Msigwa akiwa anazungumza habari nyingi inayomhusu Waziri wa Maliasili na Utalii, nikakumbuka kwamba huko nyuma tulikuwa tunafanya summit kubwa sana, wakati tunafanya mambo ya utalii, tumetangaza muda mrefu sana; na tulikuwa na summit moja tumekwenda mpaka kule Sunderland kwenye ule uwanja wa Stadium of Light tukafanya matangazo ya kutosha na Sunderland wakaja hapa kwetu wakajenga Kituo cha Kindergarten hapa ambayo iko kwenye udongo mwekundu; tumefanya matangazo Wachina wakaja hapa kwenye nchi yetu karibu 1,000; matangazo ya kutosha ya Israel, wamekuja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilipomwona mwanaume mwenzangu anapiga piga yote hapa nikakumbuka ile misafara waliyokuwa wanabebana na Waziri mwenzake Nyalandu kwenda Uganda na kwenda Marekani ndiyo hiyo inayomsumbua saa hizi hapa. Kwa sababu sasa Waziri wetu hana mkataba wa kwenda Ulaya naye, sasa amekuwa chongo kwenye mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu lazima tuwe na utalii wa ndani. Kuwachukua vijana wetu wa kwenda kufanya kuhamasisha utalii wa ndani, siyo kosa. Je, ikitokea katika nchi yetu watalii hao wa nje wasipokuja kwenye nchi yetu tunafanyaje? Tunakuwa na mapori ya aina gani?

Kwa hiyo, nafikiri kwamba vitu vingine lazima tufanye mambo ya ndani na mambo ya nje. Kwa hiyo, nampongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kazi yake nzuri sana anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nizungumzie habari ya uvuvi na Waziri wa Uvuvi anisikilize vizuri. Huwa najiuliza sana, hivi makokoro yanaisha lini? Kama nchi yetu ilikuwa na mifuko ya nylon, tukapiga marufuku ikaisha, hivi makokoro ni mtaji wa nani? Ni mradi wa nani? Kwa sababu makokoro haya sasa hayaishi.

Mheshimiwa Spika, ni lini sasa upande wa Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi atakaa na wavuvi sasa watengeneze logistic za kutosha za kuamua nyavu na milimita sita za sangara ziweje? Nyavu za furu ziweje? Nyavu za gogogo ziweje? Nyavu za nembe ziweje? Kwa hiyo, tutakaa tutengeneze formula ambayo itatuwezesha sasa kwenda kuvua, tukasema mwaka huu tumeepukana na haya mambo ya uvuvi haramu?

Mheshimiwa Spika, sasa uvuvi haramu umekuwa ni kama chanzo cha mapato cha watu. Wakati fulani tuna watu wa samaki, tuna Maafisa Uvuvi wako kule kwenye ziwa. Sasa inatoka hapa timu inaenda kufanya operesheni. Kama hawa wako barabarani, unajua vitu hivi mimi huwa sivielewi!

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, matrafiki wa kutoka Dodoma mpaka Arusha wako barabarani, lakini leo inatokea wanasema leo tumefanya operesheni ya kukamata mabasi. Sasa hao matrafiki walioko barabarani wamewaondoa au wamewafukuza kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao Maafisa Wavuvi walioko kwenye maeneo, leo mnaenda kufanya operesheni na wenyewe wapo, unamaliza kufanya operesheni unawaacha pale pale, kitu gani kitatokea? Tunaomba sasa tupate muafaka kwamba ni lini shughuli za makokoro zitaisha kwenye shughuli hizi za uvuvi?

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la pamba na bahati nzuri watu wa pamba wako vizuri sana. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ameteua vijana wazuri sana kwenye pamba. Naomba sasa watumie akili zao kuelewa haya mambo. Hivi ushirika wa sasa unatusaidia au unatugandamiza? Ushirika uliopo sasa hivi unatusaidia nini?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ushirika ule ile Kamati ya Ushirika ni Mawakala wa Makampuni, lakini ushirika wa sasa unazuia makampuni kushindana, kwa sababu ushirika wa sasa inabidi wewe kama unataka kununua pamba uende kwao. Kama ni Kituo A, kama ni Maliwanda, uende Maliwanda wewe Kampuni ya S & C, Kampuni ya Olam, Kampuni ya Kingu, Kampuni ya Bon wote mwende kwenye ushirika huo. Halafu wanawapangia muda wa kununua pamba; wewe leo utanunua mpaka hapa, wewe utanunua hapa. Ushindani wa pamba utatoka wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa wale washirika wa zamani walikuwa na pesa. Ushirika wa sasa ulikuwa na pesa ya kununua pamba, unashindana na makampuni binafsi. Ushirika wa sasa ni mawakala.

Mheshimiwa Spika, sasa huwa najiuliza, pamba ikitoka kwa mkulima ikienda kwenye ushirika anafika pale kwenye ushirika hana hela ya kununua pamba; amekopa tayari. Huo ushirika ukichukua pamba kutoka kwenye ghala kupeleka kwenye kiwanda hawana hela. Sasa najiuliza, hivi pamba inayochukuliwa kwenye ushirika kwenda kwenye kiwanda ikianguka au ikiungua moto humo ndani analipa nani? na je tunapeleka pamba kwenye ghala halafu lile ghala likaungua analipa nani?

Mheshimiwa Spika, mimi naona, ni kweli tunataka ushirika, lakini basi tuimarishe tukubaliane ushirika wa zamani urudi, tutafute fedha tuwape ushirika wanunue pamba washindane na makampuni, vinginevyo sasa utakuwa ni wakala tu; wako pale wanakula hela na watu hawataki, wananchi hawawataki tunang‟ang‟ana nao tu wanakula hela. Nishukuru tu kwamba Mheshimiwa Waziri amesema kwamba angalau kipindi hiki basi tunaweza tukafanya mambo ya watu walipe kutokana na benki, inaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya TANAPA, TANAPA ni shirika letu tumewapa mzigo wa hifadhi 22 kutoka 16, lakini hifadhi zenye faida ni tano; hata hivyo zenye faida zaidi ni mbili tu, ni Serengeti na Kilimanjaro; sasa wanamzigo wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, hili takriban ni Bunge la Nne wameomba kupunguziwa kodi. Hawaombi hela, wanaomba kupunguziwa kodi. Hivi inakuwaje leo TANAPA wakienda kunijengea mimi madarasa ya watoto shule, wanajenga Sekondari na wanalipizwa VAT? Wanalipa VAT kujenga mradi wa kijamii? Shida nini?

Mheshimiwa Spika, tumeomba hapa, wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika umesema, tumesema, sasa tufanyeje ili TANAPA wapunguziwe kodi ili waweze kujiendesha? Kwahiyo mimi naomba hili jambo lizungumzwe na liweze kufanya mafanikio kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, tuna TAWA, TAWA sasa inaonekana ni mamlaka ndogo ambayo sasa kila wakati tumekuwa tunainyanganya uchumi fulani kwa manufaa yetu sisi binafsi badala ya manufaa ya nchi kwa kweli. Kwa mfano suala la umeme wa Selous linaendelea kwa yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini mapato yao wamepandisha nadhani kutoka 33.8 bilion wamepandisha mpaka 48.8 bilion; lakini sasa uendeshaji wa TAWA kwenye shughuli zao za kawaida ni bilioni 150. Sasa kama hatuwezi kuwasaidia hawa TAWA na wanalinda mapori yetu, mapori ya akiba, mapori Tengefu, maeneo oevu, kama hatuwezi kuipa fedha za kutosha watafanyaje ili wajiendeshe?

Mheshimiwa Spika, muhimu ni mishahara ya watu wa TAWA, lazima sasa Serikali sasa kama hatuna uwezo kuipa TAWA fedha za kutosha tusaidie mishahara ya watu wa TAWA ifanane na watu wa TANAPA; maana haiwezekani! Watu wanaolinda ndio walio kwenye ukingo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana ahsante naunga mkono hoja.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naungo mkono hoja.