Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utambulisho wa mwanadamu ni utu wake! Je mifumo yetu ya elimu inajali utu wa mwanadamu? Utu ndiyo msingi mkuu wa haki za binadamu. Lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia linasema ensure inclusive and equitable, quality education and promote lifelong learning opportunities for all; elimu shirikishi, sawa, bora kwa wote! Meli ya elimu Tanzania inazama, sisi tunaosafiri ndani ya meli hiyo hatujitambui, both quality and quantity of education are being eroded. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania pole pole tunaondolewa kwenye mkondo muhimu wa maendeleo. Leo ni Ijumaa, Mtume Muhammad (S.A.W.) anasema “mwenye kutaka akhera na asome, mwenye kutaka dunia na asome, na mwenye kutaka vyote na asome! Elimu ni kitu chake kilichompotea Muislam, popote akipatapo na akichukue”
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Biblia Takatafu Mithali 4:13, “Mtafute sana Elimu usimuache aende zake, yeye ndiyo uzima wako” popote umtafute! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza na hayo kwa sababu leo hii tunazungumzia ada elekezi. Ada elekezi maana yake nini? Serikali iingie kwenye ushindani, wala sio suala; ada elekezi, mabasi ya njano, kodi zisizotabirika kwenye sekta ya elimu! Mambo haya tuliongea na Mheshimiwa Rais Mstaafu wakati tunachangia BAKWATA mwaka juzi, shule ya Sekondari Al-Haramain pale Dar es Salaam na tukakubaliana kimsingi kodi kwenye sekta ya elimu ziondolewe, elimu ni huduma sio mambo ya kutoa kodi kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii niyapongeze Mashirika ya Dini kwa kazi nzuri wanayofanya na hasa Dayosisi ya Moshi, Askofu Fredrick Shoo, Askofu Isaack Amani na kazi wanazofanya zote hizo wanafanya kwa niaba ya Serikali wakiwepo Sekta Binafsi. Kwa hiyo, haya mambo ya ada elekezi na nini naomba wala tusipoteze muda, badala yake Serikali itoe ruzuku kwenye Mashirika ya Dini, kwenye Sekta Binafsi, wayape nguvu ili waweze kutoa elimu, Taifa letu likielimika, Taifa linafaidika kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Walimu, mafao yao, Walimu kukaa mbali na familia zao na wewe umelisemea vizuri sana, tunaomba watu wote waje karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la Walimu sio suala la kuzungumzia tena! Leo hii Wizara ya Elimu inalijua vizuri. Juzi nilikuwa natoa vyetu, ukitoa vyeti leaving certificate vimeandikwa TAMISEMI, Academic certificate, Wizara ya Elimu, sasa watu hawa wanajichanganya, ni vitu gani vya ajabu sana! Jina la Wizara yenyewe, danadana tangu tumepata uhuru mpaka leo hatujui hata jina la Wizara ni kitu gani. Waziri akiingia kwenye Wizara ndiyo mfumo yaani Waziri ndiyo mfumo, aliyofanya Shukuru Kawambwa umekuja kuyapindua yote, utakayofanya sasa hivi wewe akija mwingine anayapindua yote, akija mwingine anayapindua yote, hili linakuwa tatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya BRN yamekwenda wapi leo hii? Yaani ni vitu vya ajabu tu! Miaka kumi mambo hayaeleweki. Jimbo la Vunjo tuna shule za msingi 128, shule 102 ziko hoi bin taabani, je, ni karne ya kuzungumzia mambo ya mifumo ya vyuo? Nilikuwa nasoma mitaala ya elimu ya awali, naunga mkono wale wote waliozungumzia walemavu. Ukisoma lile lengo la 326 kuhusu madarasa ya vyuo na namna ya walemavu kuweza kupata haki zao, leo hii ziko kwenye hali gani? With due respect hali inazidi kuwa mbaya, mbaya, mbaya! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vitabu; Sera ya vitabu ya mwaka 91; Sekta ya Binafsi waandikie vitabu, Taasisi wakague vitabu, EMAC imevunjwa hapa Bungeni tarehe 5 Juni, 2013, siku ya Jumatano, Bunge hili tumevunja EMAC, nani anahariri vitabu leo hii? Afadhali magazeti yanahaririwa vizuri kuliko vitabu vya shule za msingi na nitatoa mfano hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tulilonalo hapa ni itikadi zetu za siasa na Mwenyezi Mungu atatulaani kwa hilo. Tulikuja hapa mwaka 2013 na hoja ya elimu, ninayo hapa! Yote tunayozungumza kwenye Bunge hili nimeisoma hii jana mpaka saa nane na nusu za usiku, yamo humu ndani, lakini itikadi zikaingia hapa, mpaka na Kiti kikaingia kwenye mambo ya itikadi, tukashindwa Wabunge kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu leo jioni Wabunge wachukue nafasi yao ya kuisimamia Serikali wakati wa Kamati ya Matumizi kama Serikali hii haitashika adabu! Naomba sana with due respect, ninayo kwa mfano Mheshimiwa Ndalichako, Sera ya Elimu hii hapa! Iliyozinduliwa mwaka jana na Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, imetumia zaidi ya bilioni 50, ukisoma ukurasa wa 22 inaelezea mtaala unafundishwa elimu ya msingi, yaani mtaala unafundishwa! Ukisoma ukurasa wa 27 unasema mtaala ni mwongozo mpana, hata hawajui maana ya mtaala ni nini, Sera ya Elimu hapa!
Mheshimiwa Naibu Spika, nakala hizi zililetwa mezani hapa mwaka 2013. Nikahukumiwa kwamba nimesema uongo, wanaonesha kwamba ni Taasisi ya Elimu Mitaala ya 2005, lakini hapa hapa Mungu si Abdallah sio Athumani, leo hii mmeweka kwenye website yenu toleo la 2007, leo hii mmeweka kwenye website yenu! Yaani kwamba Serikali ilidanganya Bunge hili kuleta mitaala ya uongo ya kugushi ndani ya Bunge hili! Tunamdanganya nani? Huwa tunamdanganya nani? Tanzania ni yetu sote, leo hii ndiyo mitaala iliyo kwenye Website yenu. Hii mitaala mliyoenda, anakiri Bhalalusesa - Kamishna wa Elimu na ulikuwa kwenye ile Kamati kwenye Bodi ya Spika, Bhalalusesa umenisikitisha sana Kamishna wa Elimu – umesema uongo kwenye mitaala hii hapa na evidence zote ninazo. (Makofi)
Mitaala ya elimu ya msingi Bhalalusesa unasema mmefanya editing, lakini hebu nikuambie, malengo ya elimu Tanzania, lengo la tatu, sentensi moja ina „na‟ „na‟ „na‟ mara saba, mtaala wa elimu wa shule ya msingi hapa. Malengo ya 2020 - 2025 ukisoma hata copy and paste mtaala wa shule ya msingi na awali ni tofauti, ku-copy tu lengo la elimu! Malengo ya elimu Tanzania leo hii, mtaala wa awali ni tofauti na ya sekondari, ni tofauti na ya diploma ni tofauti na Walimu, tunamdanganya nani? Ku-copy mitaala ya elimu nchini, mtaala mmoja ni tofauti na mwingine. Mtaala wa awali yako 10, mtaala huu mwingine yako mengi tu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka Vunjo, kwa sababu ya muda tunazungumzia vitabu, vitabu ninavyo hivi hapa! Ukisoma kitabu cha juzi hiki hapa nimechukua Vunjo, kina mhuri wa EMAC japo tulishaivunja EMAC! Angalia ukurasa wa kule mwisho jedwali, juzi nimekikuta shule ya msingi Kochakilo, 2X7=15! Hii hapa! Nimeichukua!
Mheshimiwa Naibu Spika, chukua kitabu cha hisababti darasa la kwanza, pale mwanzoni kabisa wanasema namba nzima ni moja hadi 99, hiki hapa! Hii ndiyo sumu tunayowalisha Watanzania leo hii. Ukiangalia cha Kiingereza, chapter four ndiyo inaanza na a,e,i,o,u wakati huku mwanzoni wanaanza na sentensi, vitu vya ajabu tu! Ukisoma cha Kiswahili cha ajabu, usiku nilikuwa nasoma kitabu cha sayansi, kitabu cha sayansi, hapa tunatukana watoto huku, ukurasa wa 67 tunafundisha watoto wa miaka minane namna ya kujamiiana, mambo ya ngono, ndiyo maadili tunayowafundisha watoto wetu leo hii na imewekewa mihuri ya EMAC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hoja ya elimu nilisema nini? Tulisema, ukiangalia mambo yote, angalia hisabati, angali akila kitu, ukiangalia vitabu vyote hivi hapa, nimechukua vichache tu lakini jana usiku nikasema ; Ewe Mungu tunapeleka wapi Taifa hili. Tulisema udhaifu uliopo katika sekta ya elimu unahusiana na mfumo wa utoaji wa elimu, ndicho kirusi kilichoambukiza udhaifu kwenye sekta nyingine zote katika Taifa letu. Sababu ya msingi ya kusema mambo yote, maendeleo ya Taifa lolote, kijamii, kiteknolojia, kiuchumi na kisiasa ni tunda la mfumo wake wa elimu. Uhai wa taifa lolote lile hutegemea wingi wa matumizi ya wananchi wake walioelimika na mwisho tulisema hapa hapa kwamba; elimu ndiyo mapigo ya moyo ya Taifa letu, mapigo ya moyo yakienda kinyume na asili yake, uhai huweza kupotea, tunao wajibu wa kutunza uhai huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba sana Rais Mheshimiwa Magufuli afumue Wizara yote ya Elimu. Kama kuna ufisadi wa kupita ni Wizara ya Elimu na watendaji wa Wizara ya Elimu, hasa Taasisi ya Elimu yaani ndiyo hovyo kupindukia ndani ya Taifa la Tanzania. We are eroding our education, tunaua Taifa letu, tunambabaisha nani? Tunamdanganya nani? Labda tuondoe Hansard, tufungiane humu ndani, wenyewe tu tuondoe na media, tuelezane ukweli wa Taifa hili, la sivyo tunaangamiza Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitimisha. Mtume Muhammad anatuasa anasema: “Ukiona uovu unatendeka, zuia, ukishindwa kuzuia, kemea, ukishindwa kukemea onesha basi hata chuki” na Zaburi moja inasema…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mbatia! Nilikuwa nasubiri umalizie sentensi
MHE. JAMES F. MBATIA: … inasema: “Kheri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki…… (Makofi)