Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikushukuru wewe Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa nafasi, ili niweze kuchangia hoja zilizoko mbele yetu. Kwanza nianze kwa kupongeza, niungane na waliokwishazungumza kupongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa taarifa nzuri. Nawapongeza Wenyeviti hawa pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Kamati hizi kwa maoni na ushauri waliotupa na tunawaahidi tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali anayoiongoza pamoja na Watanzania tunafanya kazi usiku na mchana kujenga uchumi wa viwanda. Na ukiangalia takwimu tunaenda vizuri, lakini wapo wachache wanazungumza kwa ujumla na statement zao zinapotisha dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mchango wa Mheshimiwa Lema; pamoja na mchango wake maana ameuzungumza kwa ujumla kwamba, utawala bora na sekta ya viwanda na biashara viko-linked na hajatumia takwimu katika kueleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia nianze na takwimu ya Rand Merchant Bank ya Afrika Kusini kwenye ripoti ya mwaka jana mwaka 2019, Ripoti ya Where to Invest in Africa, Tanzania tumechukua nafasi ya saba kati ya nchi 54 Afrika ikiwa ni nchi yenye, best nation ya investiment, Tanzania tumechukua nafasi ya saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msisitizo nisome kipengele ambacho kinaisema hii Tanzania, kinasema hivi kwenye hii ripoti, “in the ranking Tanzania maintains the 7th position as the most attractive country to invest in the continent with a score of 5.57 in 2018 against a score of 5.59 in 2017.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia FDI nchini zinaongezeka, lakini ukiangalia takwimu pia za UNCTAD FDI flows mwaka 2018 hapa Tanzania zilikuwa ni US Dollar milioni 938 na mwaka jana ikapanda kwenda bilioni 1.1 sawa na ongezeko la asilimia 17.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Lema anavyosema kwamba, wawekezaji hawaji nchini kwa kweli, ni jambo la kupotosha. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge statement tunazozitoa kama hazina takwimu ambazo ni official tunajiharibia sisi wenyewe kwa sababu, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania tunafanya kazi kwa bidii sana kujenga uchumi wa viwanda kwa hiyo, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunasemea mazuri na jitihada nzuri ambazo Serikali inazifanya, ili kuendelea kuvutia uwekezaji, lakini tunaenda vizuri Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ningependa kutaja takwimu chache tu zinazoonesha namna tunavyoenda kwenye sekta ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Mchango wa Sekta ya Viwanda kwa ajira nchini, mwaka 2015 mchango wa sekta ya viwanda ilikuwa ni 8%, lakini hivi sasa imepanda kuwa 12.5 na malengo ya Serikali ni kufika mwaka 2025 mchango wa sekta ya viwanda kwa ajira uwe ni 20%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukiangalia mchango wa manufacturing sector mwaka 2015 ilikuwa ni 5.5%, lakini hivi sasa imepanda ni 8.3%, lakini ukiangalia mchango wa ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa ujumla wake, yaani in aggregate terms, mwaka 2015 mchango wa sekta ya viwanda ilikuwa ni 21.1% na hivi sasa ni 23.7% na ukiangalia mikakati ya kujenga miradi ya vielelezo hasahasa kwenye uwekezaji mkubwa ambao nchi yetu inafanya kwenye sekta ya miundombinu takwimu hizi zitaongezeka kwa sababu, miradi hii itachochea ukuaji wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaenda vizuri kwenye ujenzi wa sekta ya viwanda na tuendelee kushirikiana kusemea mazuri haya, ili kuendelea kuvutia uwekezaji na kuwapa moyo wale wawekezaji ambao tayari wako hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Development Budget. Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni bajeti ya Serikali nzima, yaani trilioni 33.1 tulizopitisha kwenye mwaka huu zote zinaenda kwenye kujenga uchumi wa viwanda.

Kwa hiyo, tunakosea pale tunapoangalia ile Development Budget ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, yani kama sekta kwamba, ndio Development Budget kwa sababu, ili uweze kujenga uchumi wa viwanda sekta zote, zile sekta ambazo ni za huduma za jamii, zile sekta ambazo ni za uzalishaji, zote kwa pamoja zinaungana kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara yangu pamoja na kwamba, bajeti ya maendeleo bado tunaendelea kupokea kwa mwaka wa fedha huu tunaotekeleza, lakini hata zile trilioni 4.9 ambazo ziko kwenye Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano zile na zenyewe ni sehemu ya mchango wa sekta ya viwanda kwa hiyo, tunaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kwenye Maoni na Mapendekezo ya Kamati wamesisitiza sana kulinda viwanda vya ndani. Serikali tunafanya jitihada kupitia kuongeza import duties, kutoa huduma za biashara mipakani, kudhibiti bidhaa fake kwenye njia za panya, lakini pia hata sisi Watanzania tuna jukumu la kuhakikisha tunalinda viwanda vya ndani na bidhaa wanazozizalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia majirani zetu wananchi wamepata elimu ya kupenda bidhaa zao za ndani na kwa kufanya hivyo, yaani ule uzalendo wa kusema kwamba, tukipenda bidhaa tunazozalisha wenyewe tutatengeneza ajira za vijana na akinamama ndugu zetu, yaani unakuta tunakuwa tumeshapunguza ule mzigo wa Serikali kufanya kila kitu kudhibiti, lakini sisi wenyewe kama raia tukihamasika tukatumia bidhaa zetu hiyo na yenyewe ni kuchochea sbhughuli za viwanda vyetu hapa nchini na kuhakikisha viwanda hivi vinazalisha, ili vizidi kutengeneza ajira hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha wananchi kupenda bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini, lakini kwa upande wa Serikali tunaendelea kufanya jitihada kwa kufanya tafiti. Na zile bidhaa ambazo tunazalisha hapa nchini tutaendelea kuongeza kodi pale inapowezekana, ili kuendelea kulinda viwanda hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia na jambo hili alizungumzia Mheshimiwa Mwakajoka kwamba kero kwa wafanyabiashara Serikali hatujafanya vizuri, ningependa nitofautiane naye kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye World Bank cost of doing business Tanzania tume-improve kutoka nafasi ya 144 kuja nafasi ya 141. Kwa hiyo tume-improve kwa nafasi tatu. Mikakati niliyoielezea na nitakayoitaja hapa kwa mfano blueprint, tayari ni document ambayo Serikali imesha-commit kwa Watanzania na wawekezaji kwamba tutatekeleza blueprint hii ambayo imesheheni changamoto ambazo wafanyabiashara na wawekezaji wamekuwa wakiilalamikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali imewasikiliza, tumeandaa blueprint, huu mwaka wa fedha tunaotekeleza kuna kero 54 zimeshafanyiwa kazi na hivi sasa kabla ya Bunge la Kumi na Moja kwisha, mkakati wa Serikali ni kuleta Muswada wa Uwezeshaji Biashara. Muswada huu ndiyo umebeba changamoto zote ambazo ziko kwenye blueprint ili tuweze kuhakikisha zinasimamiwa na legal force, yaani kwa maana tuwe tuna sheria inayosimamia utekelezaji wa blueprint.

Kwa hiyo, baada ya kufanya hivyo, tutazidi kuondoa keroambazo zinawakumba wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeendelea kuboresha taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Tunajua BRELA, TBS na TANTRADE ni taasisi ambazo zinatoa huduma kwa Watanzania kila siku. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali na ninyi ni mashahidi, sasa hivi hizi taasisi tunaziboresha kwa kasi kubwa sana.

Mheshimjiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye hizi taasisi, kipindi cha nyuma kulikuwa hakuna Idara za customer care, kulikuwa hakuna hotline, ukienda kwenye huduma za biashara mipakani kulikuwa hakuna namba za Maafisa wanaohudumia ili kama hujaridhika na huduma zao upige simu Wizarani na kumlalakimia Afisa fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Mikakati yote tunayo kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tuendelee kusaidiana muendelee kutupa ushirikiano ili tutekeleze mikakati hii tuzidi kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti inayokuja, tumepanga kuweka maafisa yaani commercial attache kwenye nchi ambazo tunafanya biashara nazo sana ili commercial attache hao washirikiane na TANTRADE kuhakikisha tunawasaidia wafanyabiashara wetu waweze kufanya biashara na mauzo ya nje ya wafanyabiashara wetu yaweze kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo, naomba nizungumzie mikataba iliyozungumzwa humu Bungeni kwenye maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Mkataba wa Ursus hata sisi Serikali hatujaridhika nao, tayari tumeshapendekeza kuunda government negotiating team kwa ajili ya kupitia mkataba huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hili tayari tumeshalifanyia kazi, bado hii GNT ianze na mkataba huu utaboreshwa kwa manufaa ya nchi yetu. Pia tumeenda mbali, hata Mkataba wa TANCOL hatujaridhishwa nao. Tumefanya uchambuzi tumekuta Mkataba wa TANCOL hauna maslahi kwa nchi yetu na tayari tumeshaanza mchakato wa kuunda GNT ili tuweze kupitia Mkataba wa TANCOL kama tulivyofanya kwenye Barrick na kama tulivyofanya kwenye AIRTEL. Tutaenda na wembe huo huo kwenye Mkataba wa TANCOL. Pia hata Mufindi Paper Mill baada ya kutembelea Kiwanda kile tumegundua uhasi ambao unaukuta kwenye TANCOL na Mikataba mingine upo pia kwenye Kiwanda cha Mufindi Paper Mill. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, Serikali tutaendelea kupitia vile viwanda ambavyo vilibinafsishwa baada ya kuchambua na kujiridhisha kwamba kuna maeneo hasi, hatutasita kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na Taarifa za Kamati wamelalamikia urasimu katika utoaji vibali, wamelalamikia masuala ya electronic stamps (ETS), wamelalamikia VAT ambazo kwa miaka mingi zimekuwa hazilipi kwa wafanyabiashara na wenye viwanda na vile vile wamelalamikia urasimu na mkanganyiko ambao upo ndani ya TASAC na kero za bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mimi kama Waziri wa Viwanda na Biashara sekta ambayo ndiyo driving force ya kujenga uchumi wa viwanda, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango tuko naye hapa, Waheshimiwa Mawaziri wa upande wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi wapo; baada ya kikao hiki tutakaa tuangalie namna tunavyoweza kushirikiana kama Serikali kuhakikisha tunatatua changamoto hizi ili jitihada nzuri na maoni yenu ya ushauri mliotushauri, tutakaporudi mwakani changamoto ambazo mmezitaja tuwe tumezitekeleza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, lakini nawashukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti Suleiman Saddiq, Makamu Mwenyekiti pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipa Wizara yangu. Nawashukuru sana, tuendelee kushirikiana na maoni na ushauri ambao mmetupa tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)