Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kupata hizi dakika tano za kuchangia taarifa hizi za Kamati mbili, lakini nitajikita zaidi kwenye taarifa ya Kamati moja ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kuboresha Bandari mfano, Mwanza, vilevile kuboresha gati kwa zile bandari ndogo ndogo kama ambavyo taarifa inavyojieleza hapa. Pia kama ambavyo taarifa inavyojieleza kumekuwa na ahadi ya Serikali ya kujenga meli mpya kwenye Maziwa Makuu mfano, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika. Tumeona kwenye Ziwa Victoria baadhi ya meli mpya zimeweza kuwasili, lakini pia ukarabati uliofanywa kwenye meli mbalimbali zilizopo ndani ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu tu kwa Serikali, kwa kuwa ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliowekwa wa mwaka mmoja na miaka mitano wamepanga kutengeneza meli kubwa ndani ya Ziwa Tanganyika ya kubeba abiria lakini meli pia kwa ajili ya mizigo. Tuwaombe tu Serikali waone umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu ndani ya Ziwa Tanganyika tumepakana na nchi jirani ya DRC na nchi jirani ya Zambia. Kwa kufanya hivyo tutaweza kufanya biashara ya kutoka Tanzania na kuelekea Congo vis-a-vis Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikigusa uchukuzi naomba pia niguse suala la miundombinu kwa maana ya sekta ya barabara. Kwenye Jimbo langu Serikali ilipokea pesa kiasi cha shilingi bilioni 35 kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Abu Dhabi kwa ajili ya kujenda barabara yenye urefu wa kilomita 51.1 kutoka Uvinza hadi Malagarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Serikali ipokee pesa hizo leo tunavyoongea ni mwaka wa tatu utekelezaji hakuna, niombe tu Serikali sasa hivi hali ya mvua ile barabara imeharibika sana, kila wakati tunapofanya maintenance bila kujenga barabara kwa kiwango cha lami inakuwa haitusaidii na badala yake tunapoteza pesa za Serikali. Kwa hiyo niombe Wizara ione ni namna gani itatangaza tenda ili hii barabara ya Uvinza hadi Malagarasi iweze kujengwa pamoja na kile kipande cha Chagu hadi Kazilambwa chenye zaidi ya kilomita 48. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mfupi naomba nizungumzie kidogo kuhusu NIDA. Natambua kwamba dhamira ya Serikali ni njema katika kusitisha wale wote ambao hawajasajili simu zao kwa alama ya vidole, lakini hii nchi ni kubwa na miundombinu yake sio rafiki. Hivi ninavyoongea katika Jimbo langu hata asilimia 20 haijafika, kwa hiyo niiombe sana Wizara niiombe Serikali wanapokuwa wanatupa taarifa Wabunge watambue kwamba hata wale Maafisa wa NIDA hawapo site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ndani ya Wilaya ya Uvinza Maafisa wa NIDA hawapo, wananchi wamezimiwa simu zao, mawasiliano yao, wazazi wana watoto wao Dar es Salaam, wana watoto wao Dodoma wanatumiwa pesa kwa kutumia simu zao. Niombe tu Serikali ije na mkakati maalum waone ni jinsi gani waweze hata kuwasajili kwa vitambulisho hivi vya wapiga kura, kwa sababu Watanzania wengi wana vile vitambulisho vya kupigia kura, lakini hivi vitambulisho vya uraia kwa masharti ambayo Serikali imeweka kwa kweli itakuwa na wakati mgumu sana, tunaweza tukamaliza mwaka bado Watanzania hawa walioandikwa humu milioni 15 wakawa bado hawajasajili simu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niunge mkono hoja na nishukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)