Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala unaoendelea wa Kamati ya Kudumu ya Miundobinu na ya Viwanda. Kwanza nipende kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri na njema inayowafanyia Watanzania kwa sasa. Tumeona barabara zikiwa zinajengwa katika maeneo mbalimbali, tumeona minara ya simu, madaraja, bandari na vitu vingi. Hata hivyo, napenda kujikita kidogo kwenye taasisi ya TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS inafanya kazi nzuri na iliyotukuka lakini kuna baadhi ya maeneo kuna upungufu kidogo. Kuna maeneo ambayo ujenzi tayari unaendelea, lakini watu wa maeneo husika hawajalipwa fidia mpaka sasa. Mfano wa barabara ya kutoka Itoni – Njombe – Ludewa – Manda kile kipande cha Lusitu – Mawengi kimeanza kufanyiwa kazi na sasa hivi kilometa kama 12 tayari zimeshakamilika barabara ya zege, lakini watu wa maeneo ambako barabara inajengwa walio wengi bado hawajalipwa fidia kwenye maeneo yao hayo.

Kwa hiyo naiomba sasa Serikali iweze kulipa fidia kwenye barabara ambazo inazifanyia kazi, sio Ludewa tu, pia na maeneo mengine ya nchi ambako barabara zinajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumzie kidogo Shirika la Posta; Shirika hili kweli limebeba madeni makubwa, kama ilivyozungumza Kamati, ya kulipa wale wafanyakazi waliokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mzigo ule ni mkubwa sana kwa Shirika la Posta. Tunaomba sasa Serikali iweze kuchukua huo mzigo na ikiwezekana iongezee mtaji shirika hili ili liweze kujiendesha kibiashara, ili liweze kujiendesha kwa kutumia resources ambazo inazitoa kuwalipa wale watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifuatilia kwa kiasi kikubwa juu ya madeni haya ambayo Shirika la Posta linaidai Serikali kwa sababu waliopaswa kulipa zile pensheni wale watu wa Jumuiya, ni Serikali. Kwa hiyo posta inalipa kwa niaba ya Serikali, kwa hiyo matokeo yake sasa inaondoa mtaji wa uendeshaji inalipa yale madeni na Serikali imekuwa kidogo hailipi kwa wakati. Ndiyo maana unaona sasa hivi kuna madeni mengi sana Shirika la Posta inaidai Serikali. Kwa hiyo naomba na kushauri Serikali ichukue ule mzigo wa kuwalipa wale ile pensheni na pia iwaongezee mtaji ili iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa maeneo ya mawasiliano. Mawasiliano ya simu kwenye maeneo mengi yamekuwa ni mazuri na tumeona, lakini upo upungufu. Imejengwa minara mingi sana, lakini kuna baadhi ya maeneo minara ile inachukua muda mrefu sana kuanza kuwashwa baada ya kuwa imejengwa. Mfano, maeneo ya kwetu kule ipo minara kadhaa ambayo tayari imeshajengwa, lakini mpaka sasa bado haijawashwa. Kwa hiyo niiombe Serikali iiwashe minara ile na tuone namna gani ya kuweza kuisadia hii UCSAF kuipa hela za ku-operate ili Watanzania walio wengi waweze kupata mawasiliano ya uhakika na yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Kamati ya Viwanda; kuna hili suala la Mchuchuma na Liganga, suala hili limeshakuwa ni la muda mrefu na tumesema kwamba miradi hii ni miradi kielelezo, lakini ukijaribu kufuatilia na kuiangalia hata kwenye taarifa yenyewe ya Kamati imepewa weight ndogo sana. Miradi kielelezo ninavyofahamu mimi ndiyo ingekuwa chachu ya kuchochea uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaagiza chuma kutoka nje ya nchi wakati chuma Liganga kipo. Naamini tungetengeneza concentration kubwa kwenye eneo hilo, tungeweza kupata impact kubwa ya kiuchumi kwenye eneo letu. Ukijaribu kuangalia mradi wa Mchuchuma na Liganga, tafiti zinaonesha kwamba zinaajiri Watanzania wasiopungua 32,000, lakini multiplier effect yake inaenda mpaka kwa Watanzania 300,000. Sasa ajira za watu 300,000 ni ajira kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna haja sasa pamoja na kwamba wanapitia ule mkataba lakini muda umekuwa ni mrefu sana. Yaani kuanzia tunaingia Bungeni hapa toka 2016 ule mkataba unaendelea kupitiwa, umepitiwa 2016, ukapitiwa 2017, 2018, 2019 mpaka leo 2020 bado tunazungumzia tu kupitia mkataba. Nadhani sasa ufike wakati hili suala liishe ili tujue sasa hatma ya miradi hii ya Mchuchuma na Liganga imefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa watu wa maeneo ya kusini na Tanzania kwa ujumla tunaona kabisa miradi ile ni miradi yenye tija, kwa sababu leo hii tunaagiza chuma kutoka nje wakati chuma tunacho. Miradi hii ikianza bado leo hii tunazungumzia suala la viwanda, viwanda ni umeme, viwanda ni nishati. Tunao pale umeme wa megawati 16 pale Mchuchuma, makaa yale yamekaa tu. Kwa hiyo, naomba Serikali iipe uzito unaostahili hii Miradi ya Mchuchuma na Liganga, la sivyo kila siku tutakuwa tunazungumzia Mchuchuma na Liganga na inawekwa kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pia kuna fidia ya watu ambao wamepisha ile miradi kwenye maeneo yale ya Mchuchuma na Liganga na inawekwa kwenye bajeti kila mwaka. Mwaka huu 2019/2020 zimewekwa bilioni tano kwa watu wa Liganga pale Mundindi na imewekwa bilioni tano kwa watu wa Mchuchuma pale Nkomang‟ombe, lakini hatuoni jitihada ambazo zinafanyika kuwalipa fidia watu hawa kwa sababu hizi zimeshaanza kutengwa leo ni mwaka wa tatu lakini hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Serikali iichukue yenyewe, kwa sababu mwanzo hii fidia ilisemekana kwamba italipwa na mbia, lakini sasa maadam wameingia kwenye eneo la majadiliano ya kimkataba, fidia hii ichukuliwe na Serikali yenyewe ili iweze kulipwa tuondokane na malalamiko ya wananchi ambao wamepisha hiyo miradi kwenye maeneo yale husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna hii pia la reli ya kutoka Mtwara kuja Songea - Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga, sijajua mpaka sasa wamefikia wapi na sijaiona kwenye ripoti. Kwenye ripoti humu sijaiona kama imezungumziwa chochote lakini nakumbuka kwenye bajeti ya mwaka jana wamesema kuna mbia amepatikana na wanaendelea na mazungumzo. Kwa hiyo naiomba Serikali ije sasa na maelezo tuone kwamba reli ya Mchuchuma imefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)