Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kukamilisha hoja ambayo iko hapa Mezani. Kwanza napenda niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwa maandishi na kwa kuzungumza hapa Bungeni. Nikianza na Mheshimiwa Augustine Vuma, Mheshimiwa Sonia Magogo, Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Jitu Soni, Mheshimiwa Richard Mbogo, Mheshimiwa Ester Mmasi, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Shally Raymond, Waheshimiwa Mawaziri ambao kwa kweli wamechangia na kutoa ufafanuzi mkubwa sana; Mheshimiwa William Lukuvi (Waziri wa Ardhi), Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe (Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Mheshimiwa Stanslaus Nyongo (Naibu Waziri wa Madini), Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango) na Mheshimiwa Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, sitapenda sana kusema kila mmoja alivyosema, nita-wrap up kwa pamoja. Kwanza napenda niseme kwamba Waheshimiwa Wabunge naomba tuelewe tafsiri ya gawio. Ukisema gawio hatuzungumzii ile dividend per se. Tumesema neno gawio kwa maana tumejumuisha vitu vitano humo ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mashirika ambayo yanafanya biashara (commercial entities) wanalipa gawio na hii inakokotolewa baada ya kuwa umeshapata faida na baada ya faida sasa ndiyo unapata gawio lake. Vilevile kuna mchango wa asilimia 15 wa growth turnover ya kila taasisi ambayo inatoa huduma pamoja na wakala. Vilevile tuna fedha asilimia 70 ya redemption excess capital, rejesho la mtaji uliozidi kwa hizi taasisi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata asilimia 28 kutokana na mapato ya TTMS, mfumo wa mawasiliano ya simu na vilevile Serikali inapata mapato kutokana na riba ambayo inakopesha kwenye hizi taasisi. Kwa hiyo, kwa ujumla wake ndiyo gawio. Hata Waheshimiwa waliokuwa wanazungumza hapa ni kwa sababu wanajua dividend; wanasema kwa nini tunapata hasara? Wanatoa dividend, hapana. Hoja ni kwamba kila taasisi ya Serikali ambapo Serikali ina hisa pale ndani, imewekeza, kama siyo gawio, itoe mchango kwa Serikali. Ndiyo maana yake hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, naomba sasa niwashukuru wale wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi. Pia hoja za Taasisi za Umma kutoa gawio kwa Serikali zimezungumzwa na Wabunge wengi humu ndani. Naendelea kusisitiza kwamba Serikali ihakikishe taasisi zote zinazotakiwa kutoa gawio zinafanya hivyo na mashirika yanayotakiwa kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali yanatimiza takwa hilo. Kamati inaamini kuwa bajeti ya Serikali inaweza kuendeshwa kwa kutumia mapato yatokanayo na kodi na mapato yasiyotokana na kodi ambayo ndiyo Kamati yangu imekuwa ikisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la marekebisho ya sheria na kuhusu suala zima la kufanya kazi kwa taasisi ambazo zinakiuka matakwa ya Sheria ya Fedha Na. 16 ya mwaka 2015, viongozi wake waweze kuchukuliwa hatua. Wakikiuka matakwa ya sheria hii, lazima Serikali iwachukulie hatua kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kuhusu watumishi kukaimu nafasi. Hili limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwa kweli tungependa kuona kwamba nafasi ambazo zinakaimiwa, Serikali inachukua hatua za makusudi ili kuweza kupata watendaji ambao ni substantive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la michango, kwa mfano suala la miradi ambayo haijakamilishwa ya National Housing, Mheshimiwa Lukuvi ameelezea vizuri sana, sina haja ya kurudia tena. Nafikiri hata Mheshimiwa Mdee amemwelewa vizuri, kwamba Serikali imeangalia baadhi ya mikataba ambayo ilikuwa na matatizo, ndiyo maana inafanyia utafiti mzuri ili kupata solution ya kudumu ili mashirika yetu yaweze ku-perform inavyotakiwa. Nakushukuru sana Mheshimiwa Lukuvi kwa kutoa ufafanuzi ambao kwa kweli ni wa kina na ninajua kila mmoja ameweza kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la TTCL na hili Mheshimiwa Dkt. Mpango amelizungumzia vizuri; na suala la STAMICO Mheshimiwa Nyongo amelizungumzia vizuri, sina haja ya kurudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la sheria kupitwa na wakati, ni kweli sheria nyingi za taasisi hizi toka kuanzishwa kwake zimepitwa na wakati. Kwa hiyo, kuna haja kubwa ya kuanza kupitia mchakato wa sheria hizi ili kuwezesha mazingira yaliyopo yaendane na hitaji la kisheria la sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la madeni, inasikitisha kuona kwamba baadhi ya taasisi za Serikali zinashindwa kulipa madeni yake, na hata ku-collect madeni ambayo inadai. Kwa hiyo, tunatoa msisitizo kwa Serikali ihakikishe kwamba tatizo hili linaondolewa haraka iwezekanavyo ili taasisi zinazotoa huduma ziweze kuendelea na majukumu yake na kuwa na ukwasi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa Sera ya Gawio, limezungumzwa hapa na Serikali imeshasikia, tumeshatoa maelekezo kwamba lazima kila taasisi inayofanya biashara lazima iwe na Sera za Gawio. Hiyo imeshakuwa concluded. Hatuna shaka kwamba Serikali itafuatailia na TR ana maelekezo mahususi ya Kamati yangu kwamba lazima kila shirika na taasisi ya Serikali inayopaswa kutoa gawio iwe na Sera ya Gawio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekezaji katika taasisi ambazo Serikali ina hisa chache; Serikali inatakiwa kufanya tathmini ya kina na kuona namna bora ya kuwekeza katika taasisi ambazo ina umiliki wa hisa chache kwa kuwa uwekezaji huo utaongeza faida kwa Serikali na njia ya gawio na pia njia ya mafanikio mbalimbali wanayopata wananchi wa Tanzania walio katika maeneo ya uzalishaji wa taasisi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kuhusu suala la Ofisi ya TR. Mheshimiwa Dkt. Mpango amefafanua vizuri zaidi, sina haja ya kuirudia, kwamba iwezeshwe kwa maana ya rasilimali fedha na rasilimali watu iweze kufanya kazi yake vizuri pamoja na kuboresha suala zima la TEHAMA katika ofisi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Star Media Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe amelieleza vizuri sana. Ilikuwa inasikitisha, baada ya Kamati kushindwa kupata taarifa na kuzungumza na hawa watu, lakini baada ya Serikali kuingilia kati, tumeona mafanikio, mpaka wametoa na gawio la shilingi milioni 500, hiyo ni hatua moja wapo. Naamini kabisa kwamba Serikali itaendelea kulifanyia kazi kwa umakini zaidi na kuhakikisha kwamba suala la Star Media na TBC linapatiwa ufumbuzi unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ambayo tunaomba Serikali iichukue kwa nguvu zote ni kurejesha fedha za madai ya VAT. Makampuni na taasisi nyingi zinalalamika, Serikali hamrejeshi. Tunaomba sana hili kama Serikali, tuweke mkazo ili tusizidi kuyaumiza mashirika na kampuni ambazo yame-tie up capital katika suala zima la VAT refund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa nafasi ya pekee, nafikiri hata Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla mtaungana nami kabisa. Licha ya Mheshimiwa Jenista Mhagama kuzungumza kwamba NSSF imefanya kazi vizuri zaidi; na kwa kweli kama alivyosema shirika limebadilika, mfuko umebadilika sana. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama kwa jitihada ambazo amezifanya katika Mfuko huu wa Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, yote haya ni tisa, kumi tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Toka ameingia madarakani umeona kwamba gawio kwa taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma zilikuwa haziji. Leo hii tumeweza kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 1.05, ni historia. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kama inawezekana tuwe na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua hiyo. Fedha hizi ni kwa Watanzania, ndiyo maana miradi inaendelea, inafanyika kwa sababu tuna fedha ambayo ilikuwa haipatikani lakini sasa inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa maelezo hayo, naomba kutoa hoja ya Kamati. (Makofi)

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.