Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kufika hapa ndani saa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwe wazi kwamba mimi nina shule, vilevile ni Mwalimu na nina Kituo cha Watoto Yatima. Hivyo vyote kwangu ni mwiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na suala la watoto yatima, tunaongelea suala la mikopo, kwangu mimi mwenye Kituo cha Watoto Yatima nimekuwa na watoto na vijana zaidi ya 451 ambapo 15 walitakiwa kwenda chuo kikuu kwa njia ya mkopo lakini hawakuweza kufanikiwa, sielewi ni vigezo vipi ambavyo vimekuwa vikitumika kwa ajili ya kupata mikopo. Hivyo naona kuna matatizo kwenye mikopo, Bodi ya Mikopo ina matatizo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niombe uone namna utakavyofuatilia suala hili na kuhakikisha kwamba vigezo stahiki vinatumika kwa ajili ya mikopo hiyo hasa kwa watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la Walimu; mimi kama Mwalimu nina uchungu sana, nina uchungu na maisha wanayoishi Walimu kwa sababu mwenyewe nimekuwa katika mazingira hayo magumu. Mwalimu inafika hatua Afisa Elimu anakuchapa makofi au vibao, mfano, kule Rukwa kuna Mwalimu alichapwa na Afisa Elimu, jamani haki ziko wapi kwa Walimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo haitoshi Walimu wanapangiwa kwenda kufanya kazi maeneo ya mbali. Mfano pale Njombe nina Walimu zaidi ya watano walipangiwa kazi Mwanza. Walimu hawa walikuwa ni wanandoa, lakini unakuta Mwalimu wa kike anapangiwa Mwanza, mume wake anapangiwa Kondoa. Hapa naona vilevile Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inakinzana na Sheria ya Ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa tuone namna gani tunawasaidia Walimu kwa kuweka sheria hizi mbili vizuri kwa sababu sasa hivi tunaongelea suala la UKIMWI na Mkoa wangu wa Njombe ninavyoona ndiyo unaoongoza, halafu bado tunawatenganisha Walimu hawa wanandoa, kwa kuwapeleka kukaa maeneo tofauti, tunategemea nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, akisaidiana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, waone namna gani tunawasaidia Walimu hawa, wanandoa naomba wapangwe sehemu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la mitaala; miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2005 mitaala ilikuwa imejielekeza zaidi kwenye maarifa, lakini baada ya mwaka 2005 mitaala hii ilibadilishwa na ikaja kuboreshwa mwaka 2013. Mitaala hii imekuwa angamizo kwa kweli, kwa nini imekuwa angamizo? Watoto wetu sasa hivi wanajua kusoma vizuri na kuweza kutoa maana ya vitu fulani au kujieleza lakini hawajui kufanya kazi yoyote ile. Mfano mtu mpaka yuko Chuo Kikuu hajui hata kusonga ugali, mtu yuko chuo kikuu hajui kufua nguo, sasa hiyo ni mitaala ya namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri turudi kwenye mitaala ambayo tulisoma sisi kule nyuma. Mtu kuanzia darasa la nne anajua namna ya kufanya kazi ndani ya nyumba, namna ya kuelekeza hata wadogo hata kama yeye ni mdogo anajua namna ya kuelekeza mdogo wake, anajua kufua nguo, anajua kuosha vyombo, lakini sasa hivi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sayansi ya jamii haipo tena, nitoe tu mfano mdogo tu, tukiwa darasa la nne, mimi nikiwa darasa la nne, nilijua hata maana ya pazia, unapoweka pazia ndani ya nyumba, unapoweka kwenye dirisha ugeuzie wapi na maana yake nini, lakini hata ukimuuliza mtu aliyemaliza chuo kikuu hajui hata maana yake, hajui hata lengo la pazia ndani ya nyumba ni lipi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tutumie njia yoyote turudi kwenye mitaala yetu ile tuliyoiacha, elimu tumeipeleka wapi? Sayansikimu tumeipeleka wapi, watoto hawajui kupika. Kwa hivyo, niombe tafadhali, Serikali ilione hili tusaidiane kuhakikisha tunarudi kule nyuma, tuwasaidie, tuokoe Taifa hili linaloangamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine, sasa hivi tumeanza kwa nguvu zote na ni jambo jema, kuwahamasisha watu ambao walikopa na wengi wetu humu ndani nafikiri tulikopa, tumesoma kwa mkopo, lakini hebu tujiulize, tunapohamasisha kurudisha hiyo mikopo hao watu wote wamepata ajira! Watu wengi wako mitaani na ndiyo maana inakuwa vigumu kufuatilia kuwa na mapato makubwa yanayotokana na mikopo kwa sababu wengi hawajapata ajira, hivyo tuone ni namna gani tunawafuatilia wale wa mitaani tutumie njia ya kisasa kuweza kuwafutilia hao walioko mitaani na kuhakikisha tunakusanya pesa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tutengeneze mazingira ya wao kuajiriwa na hata kama inawezekana basi, tutumie njia ya kuwafundisha au kuielimisha jamii namna gani iweze kuwa na njia za kujitegemea au ujasiriamali ili waweze kurudisha pesa hizi ambazo wananatakiwa warudishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la uhamisho. Sasa hivi wanahamishwa watumishi toka kona moja hadi nyingine, lakini hawapati pesa za uhamisho. Unakuta Mwalimu anapangiwa kwenda kufundisha mfano Mwanza au Tabora, anafika kule hana hela ya kujikimu, hana sehemu ya kukaa, mwisho wa siku anaanza kuombaomba, huyo ni Mwalimu na huko ni kumdhalilisha Mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, tuwasaidie watu hawa, tunapowapangia tuhakikishe basi pesa ya kujikimu tumeiandaa na mahali pa kukaa tumepaandaa na nyumba za Walimu ziandaliwe. Walimu wengi sasa hivi wamekata tamaa wanahama fani kutokana na ugumu huo wa maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge hoja ya Upinzani kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.