Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata pumzi zake na leo kusimama hapa, lakini pia namshukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Mpango wa Maendeleo. Kabla ya yote, napenda niipongese Serikali kwa hatua kubwa sana za maendeleo ambazo imechukua na sasa tunaona kwamba hatua tunazokwenda, tunakwenda vizuri. Kwa hiyo, naishukuru sana Wizara ya Fedha pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Tunamwombea Mungu aendelee kuchapa kazi na aendelee kufanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo unasema kwamba penye nia pana njia. Kwa nini nikasema hayo? Ukiwa una nia ya kitu, basi njia ya kulitekeleza kile kitu itatokea. Sasa naishauri Serikali, tumeweka shilingi trilioni 107 katika Mpango ule wa Miaka Mitano kwenye ugharamiaji, lakini tukaweka shilingi trilioni 59 kwa ajili ya Serikali kwamba ndio itagharamia huo Mpango; lakini shilingi trilioni 48 ndizo ambazo zitatumika na Sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nije katika sekta binafsi, je, kuna jitihada za kutosha kuhamasisha sekta hii kugharamia huu Mpango? Kwa sababu cha Serikali tunakijua, tutakuja kwenye bajeti hapa, tutapitiasha mipango kwenye bajeti, itakapopita tutajua kwamba hii ni kasma ya Serikali katika kugharamia Mpango, tumeiona. Isipokuwa hatuioni wazi wazi sekta binafsi inavyotumika kugharamia Mpango huu. Kwa maana hiyo, hata hizi figures ambazo tumeziweka, ina maana labda tuje tujumuishe mwisho baada ya miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iwe na umakini na ichukue hatua za kutosha katika kuhamasisha sekta binafsi. Sekta binafsi hazijahamasishwa vya kusha na huu Mpango ni mipango yetu, imewekwa kwa ajili ya Serikali na sekta binafsi. Kwa hiyo, hilo nilikuwa naliomba. Kwa mwaka ukichukua average, sekta binafsi ilipaswa ichangie kwenye Mpango huu shilingi trilioni 9.6. Sasa je, tunazipata hizi? Kama tunazipata, sasa tumeshakwenda miaka mitatu, tumebakia na miaka miwili, hizo shilingi trilioni 48 za sekta binafsi zitapatikana? Kwa hiyo, naishauri na naiomba Serikali itumie kasi kubwa zaidi katika kuhamasisha miradi ambayo imepangwa kufanywa na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, kuna msemo unaitwa nia na azma. Azma, unaweza ukaazimia tu, lakini nia unatia nia wakati kile kitendo kiko njiani kwenye kukitekeleza. Nimesema hivi kwa sababu kuna mambo humu yanaonesha kama ni azma siyo ya nia. Huu Mpango umeandikwa kwa ajili ya mwaka unaokuja. Sasa kuna mambo yameandikwa lakini utekelezaji wake huwezi kuja kuyaona, kwa sababu yatafanywa na sekta binafsi. Sasa naiomba Serikali ijaribu kuangalia kitu ambacho wana nia nacho, kile cha azma tukiache kule kwenye Mpango Mkuu, yale mambo ni mengi, sasa mengine yameazimiwa, lakini hayajatiliwa nia kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee kitu kimoja katika msemo huu, kuna kitu kwa Kiingereza wanaita scope. Umetajwa mradi hapa wa bandari ya uvuvi wa bahari kuu, ununuzi wa meli; najiuliza, hii scope itakuwemo ndani ya mwaka unaokuja yote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa wa 66 umetajwa uvuvi wa bahari kuu katika kitabu cha Mpango. Sasa kama kitu tuna nia nacho, basi tukiandike kile ambacho tuna nia nacho kuliko tukiweka scope kubwa halafu baadaye tukaja kushindwa kuifikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, naishukuru Serikali kwa kuleta Mpango huu na kuyaona hayo mengine na kuyaweka, lakini tunahitaji tuboreshe. Tuweke kitu ambacho kitafanyika kwa karibu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni mambo mawili, bandari zetu na reli. Tunajenga reli, ni sawa, ni kitu kizuri, lakini mapato ambayo tulitarajia tuyapate kule yalikuwa ni makubwa. Speed ambayo tunaenda nayo au tuliyoanza nayo nahisi bado ni ndogo. Kwa sababu tulisema itakapofika mwaka 2025, tuwe tuna kipato cha kati. Mwaka 2025 kwa mujibu wa Mpango huu, iwe tuna ukuaji wa asilimia 10. Itatoka vipi hiyo asilimia 10? Ni kama tutaziweka bandari zetu vizuri pamoja na reli. Angalau hii mipango imepangwa humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaweza ikaja ikatufungua katika kufikia hiyo asilimia 10, lakini Mpango huu wa miaka mitano ambao tumeenda nao tuliolenga hiyo asilimia 10, sasa tumebakia na miaka miwili: Je, tunaweza tukaifikia hii asilimia 10? Kama tunataka kuifikia, hata kama kwa kuchelewa kidogo, basi tujaribu kuangalia bandari zetu pamoja na reli ambazo zitachukua mzigo kupeleka nje. Tanzania ni nchi ambayo imebarikiwa, iko katika eneo zuri, tuna majirani ambao wanatutumia vizuri. Kwa hiyo, nasi ili tuweze kupata uchumi wa nchi hizo, ina maana ni lazima bandari zetu na reli ziwe zinakwenda sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, niongelee viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege. Tunaishukuru Serikali, ni kweli tumenunua ndege, tunapongeza, lakini bado zile ndege haziko busy vya kutosha. Ili ndege ziwe zinaleta faida na ufanisi, ina maana kwamba ziwe angani, zisiwe kwenye zimepaki. Sasa ndege zetu zinapaki sana. Tatizo ni kitu gani? Ni viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru viwanja vya ndege vya kanda vimejengwa vikubwa ambapo ndege zetu zinakwenda, lakini tujaribu kuwa na viwanja vya ndege vikubwa vya mikoa ili hizi ndege nazo zitumike vizuri ziweze kusaidia uchumi katika nchi hii. Kwa hiyo, Serikali imesema kwamba itasimika taa za kuongezea ndege, ndio; lakini tujaribua kuangalia kwa mikoa sasa. Kanda ya Kusini tumeona, Kaskazini kuna kiwanja kikubwa, tumekiona; Kanda ya Kati, kitakuwepo kiwanja hapa na hiki kingine kimeboreshwa; lakini tujaribu kutizama kwa mikoa, kwa sababu huu uchumi wetu tunaotaka uende, kama tutakuwa na hizi ndege na viwanja vya ndege vikikaa sawa, tutakuwa tunao uwezo mkubwa sana wa kukuza mapato katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimekusudia niliongelee ni uvuvi wa bahari kuu. Uvuvi wa bahari kuu ni sehemu ambayo hatujaenda na mkakati mzuri wa kuweza kusema kwamba tutakwenda kuukamata uvuvi huo wa bahari kuu au uchumi huo unaopatikana kutokana na uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, page ya 66 amesema Mheshimiwa Dkt. Mpango kwamba wao watajenga bandari au Serikali itajenga bandari, itanunua meli za uvuvi. Tulikuwa tunaomba ingeshirikishwa na sekta binafsi. Acha Serikali ijenge bandari, lakini ununuzi wa meli kwa nini tusiachie sekta binafsi? Kwa sababu kujenga bandari peke yake ni shughuli; na kama nilivyosema kwamba hata hapa scope yake mimi kidogo naona haikukaa vizuri sana, kwa sababu limesemwa jambo moja pana sana na kutekelezeka kwake katika Mpango na bajeti hii nahisi itakuwa siyo rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kubinafsisha baadhi ya mambo, siyo lazima kwamba Serikali inunue meli, inaweza ikaweka hayo mazingira mazuri kwa ajili ya upatikanaji wa huo uvuvi wa bahari Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika uvuvi wa bahari kuu, naiomba sana Serikali itoe tamko au iseme wazi, ule mrahaba wa 0.4; mrahaba ule unavunja shughuli zote za uvuvi wa bahari kuu. Tulikuwa tunapokea meli 81 ambapo kila meli inalipa dola 36,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi baada ya kuweka huo mrahaba, hakuna meli zinazokuja. Hiyo imeweka kwa Kanuni. Sasa tulikuwa tunaomba Serikali hebu iwe wazi, iondoe hicho kitu, at least tuwe tuweze kupata mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza katika hotuba yake aliyoitoa ukurasa wa sita, alizungumzia...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ali King, malizia sasa hapo.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono...

MWENYEKITI: Nasema malizia dakika zimeisha.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ingeweza kukusanya mapato mazuri sana kutokana na hiko kitu. Kwa hiyo Serikali iwe wazi, hiyo Kanuni kama ipo ieondolewe kwa sababu tunakosa uchumi kutokana na uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante sana. (Makofi)