Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu kuhusu Mpango wa Maendeleo ya Taifa na nashukuru kwa kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii. Dhima ya Mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano ni kuangalia suala zima la uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi huu wa viwanda utaendana na ukuaji wa uchumi lakini na maendeleo ya watu. Tunajadili Mpango huo mwisho wa miaka mitano, ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani ingekuwa ni vema sana Serikali ikajitathmini katika miaka minne ya utekelezaji wa Mpango; je, tumetekeleza kwa kiwango kipi, tumekwama wapi na tunafikiri nini turekebishe ili yale malengo tuliyojiwekea kwa miaka mitano sasa tuuweke kwenye Mpango huu ambao umebaki wa mwaka mmoja ili kufidia kuziba mapungufu yaliyojitokeza katika Mpango uliopita. Nilidhani wangefanya hivi ingeweza kusaidia sana kujipima kwamba, katika miaka mitano mipango yetu ya miaka mitano ni kiwango gani tupo na tunaendelea vipi, hali yetu ya uchumi ikoje, maendeleo ya watu wetu kwa ujumla yakoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni dai la muda mrefu hasa Kambi ya Upinzani, tumekuwa tukidai sana kuwepo na sheria ya kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa. Tumedai muda mrefu na hii sheria itasaidi mfano tukifanya tathmini tukaona kuna upungufu fulani na upungufu kama unahitajika kuzibwa na sheria, basi ni muhimu sasa tukawa na sheria ya utekelezaji wa Mpango huu. Tukiwa na sheria hii maana yake pia tutakuwa na uwajibikaji wa kutosha kwa watekelezaji wa Mpango huu lakini tutasaidia kufanya reallocation mbalimbali za bajeti ambazo ziko nje ya mpango. Maana yake mpango ule ambao utakuwa umepitishwa Bungeni kama tutakuwa tuna sheria kwa kiwango kikubwa itaziba hii mianya mingine ya kuibua miradi mingine au mipango mingine mingi mingi ambayo kwa kweli kwa kiasi kikubwa inaenda kuathiri bajeti ambayo tumejiwekea au bajeti ambayo imepitishwa hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama nilivyosema tukiwa na sheria kutakuwa na uwajibikaji wa kutosha, Serikali itawajibika kwa kuhakikisha kwa kweli mipango inatekelezwa kwa kiwango kikubwa na kwa asilimia hata mia moja ikiwezekana inaweza kufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kutokutekelezwa kwa miradi ya maendeleo. Tumeona, tunashindwa kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sababu tunakuwa na mipango mingi ambayo haiendani na bajeti, haiendani na makusanyo yetu ya ndani, lakini tunakuwa na mipango mingi na miradi mingine mikubwa ambayo kwa kweli kwa kiwango kikubwa hatutaweza kutokana na fedha zetu kutekeleza. Ndiyo maana nikatoa rai hapa mwanzo kwamba ni lazima tufanye kwanza tathmini tuone tumejikwaa wapi, tumeshindwa nini ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia Bunge limekuwa likiidhinisha bajeti hapa lakini utekelezaji wa bajeti hiyo hasa kwenye miradi ya maendeleo kwa kweli ni kiwango cha chini sana. Ukirejea hotuba ya Kambi yetu ya Upinzani inaeleza mfano, kwenye Wizara ya Kilimo na Sekta nzima ya kilimo. Tukielewa umuhimu wa Sekta ya Kilimo hapa nchini tunajua ndiyo watanzania wengi wanategemea kilimo lakini kilimo hiki ndiyo tunategemea. Kama tunataka viwanda maana yake tunategemea kilimo tupate malighafi, viwanda viweze kuendelea na hatimaye hicho tunachokisema kwamba tunataka uchumi wa viwanda ili kuchochea maendeleo ya watu na hali ya uchumi kwa ujumla tuweze kufikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa hatutekelezi miradi ya maendeleo, kama tutakuwa Bunge lako linaidhinisha bajeti hapa halafu hazifiki kwenye wizara husika maana yake tutakuwa hatupigi hatua tunarudi nyuma. Kwa hiyo, ni muhimu sana sana tukaangalia kuwa na miradi michache ambayo tunajua tunaweza kutekeleza na miradi hiyo ikapitishiwa fedha hapa Bungeni na kwa kweli ikatoka kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, ukienda kwenye Wizara ya Kilimo, ukienda kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukienda kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, wizara zote ambazo zinafungamana na hicho ambacho tunakitaka, uchumi wa viwanda zote fedha zake za miradi ya maendeleo kwa kweli hazijafika hata asilimia 60, 70 au asilimia 100. Kwa hiyo, ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Serikali sasa hivi inatekeleza miradi mikubwa mitatu, kuna Stiegler’s Gorge, kuna SGR na ununuzi wa ndege, hii yote ni miradi mikubwa ambayo inahitaji fedha nyingi. Sasa tunakuwa na miradi mikubwa kwa mara moja ambayo inahitaji fedha nyingi maana yake ni kwamba fedha zozote zinazopatikana zinaenda kwenye miradi mikubwa. Halafu huku kwingine kwenye miradi midogo midogo ambayo kwa kiwango kikubwa ina mgusa mwananchi wa kawaida haifikiwi na hatuwafikii watu wa kawaida. Kwa hiyo, rai yangu kwa Serikali kwamba mnapokuwa na miradi mikubwa mje na mkakati wa ziada wa kuonesha ni namna gani miradi mikubwa inaweza ikatekelezwa, ni namna gani itakuwa financed ili miradi hii iweze kutekelezwa. Ni muhimu sana ili tusiweze kuathiri mambo mengine, utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudi kwenye Serikali zetu za Mitaa kuna hali mbaya sana. Tuligemea kwamba, na tunategemea kwamba Serikali za Mitaa ndiyo kwa kiwango kikubwa ndiyo wananchi wako kule, ndiyo kwa kiwango kikubwa tunategemea miradi muhimu ambayo inamgusa mwananchi mmoja mmoja; maji, barabara, kilimo, masoko, kwa kiwango kikubwa mwananchi kule kwenye Serikali za Mitaa ndiyo inamgusa. Serikali za Mitaa hizi sasa hivi zimekuwa hoi bin taabani, hakuna kitu, fedha zote za makusanyo zimebebwa. (Makofi)

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy taarifa nimekuona.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba anasema Serikali yetu haipeleki miradi katika wilaya. Tangu uhuru haijajengwa hospitali za wilaya 67, tumejenga zahanati hazina hesabu, sasa nashangaa anasema hatupeleki wakati miaka yote 45 sijui hakuna… kama Namanyere tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya acha kwake. Juzi ametoa hospitali ya wilaya pale Ubungo tena kwa mpinzani, sasa anasema wapi hatupeleki miradi midogo midogo!

MWENYEKITI: Amesahau kidogo unajua tena hayo mambo, Mheshimiwa Cecilia si unajua alikuwa kwenye utaratibu maalum! Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

Tunatumaini mjukuu hajambo! Endelea Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante taarifa ya Mheshimiwa Keissy siipokei na siipokei kwanini! Ukifanya tathmini kwa sababu si toka tumepata uhuru nchi hii inaongozwa na Chama cha Mapinduzi, nchi hii ndiyo inakusanya kodi. Ukifanya tathmini toka tumepata uhuru mpaka leo yaani tulipaswa Tanzania hii kuwa ulaya, kama kwingine maana yake ni tumechelewa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapoongelea Namanyere ndiyo wamepata hospitali ya wilaya wamechelewa sana, walipaswa wapate kwenye miaka labda ya 80 huko, 70, miaka ya 90 mnaongelea habari za hospitali za rufaa kwenye maeneo yenu sasa namna gani ya kuboresha. Kwa hiyo, kwa mtazamo wa kwamba ipo inafanyika, imechelewa kufanyika, ilipaswa ifanyike mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kwenye Serikali zetu za Mitaa nadhani ni rai sasa kwa Serikali kuzitazama upya Serikali zetu za Mitaa, vile vyanzo vingi ambavyo mmevinyang’anya mvirudishie ili viweze kujiendesha. Namna gani itaendesha, namna gani itatumikia wananchi, leo kuna baadhi ya halmashauri hata Vikao vya Baraza la Madiwani kwa mujibu wa sheria havifanyiki kwa sababu hakuna fedha, havifanyiki kwa sababu mapato ni madogo, yale yanayopatikana kidogo yanachuliwa. Siyo tu kuchukuliwa wakati mwingine maagizo yanayokuja kwa kiwango kikubwa kinaenda kufanya nini, kuharibu bajeti ambayo imewekwa kwenye Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, bado Serikali zetu za mitaa zina hali mbaya zinapaswa kwa kweli kwa kiwango kikubwa kubebwa na kusaidiwa na kurudishiwa fedha zile ambazo zitakusanywa na Serikali Kuu, zinazotakiwa kurudi kwa mujibu wa sheria zikarudi zikatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo machache, nashukuru sana kwa nafasi ahsante sana. (Makofi)