Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kidogo, nafikiri mchango wangu utakuwa siyo mrefu sana. Kwanza kabisa kama ambavyo wenzangu wametangulia, tupongeze kwa jitihada kubwa ambazo zimefanywa katika Awamu hii, mambo mengi yamefanyika tukianza kwenye majimbo yetu, mambo makubwa yamefanyika ambayo kwa kweli kwa muda mfupi Serikali imeonesha jinsi ambavyo fedha zimetumika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kujikita kwenye viwanda, niipongeze Serikali yetu kwa jinsi ambavyo iliamua kujikita kwenye suala zima la viwanda, kazi imefanyika na niseme wazi kwamba jitihada zimefanyika na viwanda vingi vimeanzishwa. Kikubwa ambacho ningependa kujua, mpaka sasa ni viwanda vingapi tayari vimeshaanzishwa? Kwa maana ya viwanda vikubwa ambavyo vinaenda kusaidia kuuinua uchumi wetu; viwanda vya kati na vidogo na je, sheria tumeshatunga za kulinda viwanda vyetu, kwa mfano, malighafi na upatikanaji wake? Nasema hivi kwa sababu ukiangalia viwanda vingi vitakuwa vikitegemea malighafi aidha kutoka ndani au nje, tumejipangaje kubadili sheria kwa sababu kwenye sheria, nyingi zimebaki kama zilivyokuwa kwa mfano sheria za kusafirisha malighafi nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kuna Kiwanda kama cha Pareto pale Mafinga. Kiwanda kile kinategemea malighafi ya Tanzania, lakini sheria zamani hazikatazi malighafi hiyo pareto maua yale kusafirishwa nje, kuuzwa nchi zingine na tumeshuhudia sasa kiwanda kama hicho kinakosa malighafi na hivyo kushindwa kujiendesha kama ambavyo inatakiwa. Kwa hiyo, niombe tu tuangalie upya sheria zetu, lakini pia tuangalie hata bei za umeme kwa viwanda vyetu ambavyo vinakuja pamoja na kuwa tuna mategemeo makubwa baada ya kumaliza ujengaji wa bwawa, lakini tunatakiwa tuangalie mapema kwamba tutavilinda vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kodi; tuangalie sasa kama tutakuwa tumejenga viwanda na kuna malighafi ambazo zinatoka nje, tuangalie jinsi ambavyo tunaweza tukasaidia viwanda vyetu kupunguza kodi ili waweze kuingiza malighafi ili viwanda vyetu vijiendeshe, bila kufanya hivyo itakuwa hakuna tulichokifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka tu kujua kwa sababu tuko kwenye Mpango huu, nijue hali ya ushiriki wa watu akinamama na watu wenye ulemavu kwenye viwanda vyetu jinsi ambavyo watalindwa, kwa sababu ukiangalia unaweza ukakuta watu wenye ulemavu hawajawekewa mpango maalum na wao ni binadamu na wengine wana akili zaidi ya watu ambao wazima. Kwa hiyo Serikali iwe na mpango mkakati kabisa kwamba kiasi gani na asilimia ngapi wataajiriwa kwa sababu walio wengi siyo kwamba hawana uwezo kabisa, wana uwezo wa kushiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa tuangalie vilevile ni kuhusu unyanyaswaji wa wanawake na watoto katika Mpango wetu, kwa sababu ukiangalia wanawake na watoto ni watu ambao wamekuwa wakinyanyaswa kila pande na wao ukiangalia ndiyo ambao wanasaidia kwenye uchumi wetu, hasa huu wa viwanda. Ajira nyingi sana zinategemea akinamama wengi wataajiriwa, lakini tusipowawekea mkakati madhubuti wa kuhakikisha tunalinda usalama wao inawezekana uchumi wetu ukawa na shida. Nasema hivi kwa sababu tumeangalia Jeshi la Polisi ambavyo limekuwa likifanya kuanzisha Dawati la Jinsia jinsi ambavyo limeweza kusaidia kuinua maisha ya mwanamke hasa vijijini na kuongeza pato la watu. Kwa hiyo tuangalie hata katika Viwanda vyetu si mbaya kukawa na kuna Madawati ya Jinsia ili kulinda wafanyakazi na akinamama ambao wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa China mwaka 1978, uchumi wao ulikuwa sawa na sisi sasa, miaka 41 iliyopita, lakini leo wameshakwenda mbali kama ulivyosema na hii siyo kwamba lelemama, kuna vitu vya msingi vimefanyika. Ukiangalia China suala la rushwa hakuna ukikamatwa na rushwa unachinjwa, ukifanya kosa unapata adhabu ambayo inaonekana. Kwa hiyo na sisi lazima tujifunge mkanda, tunaweza tukapata tabu sasa, kwa sababu hata wale waliojenga reli walikuwa wamekuja wanavaa suruali ambazo zilikuwa zina viraka zinazofanana, lakini leo hii waliumia wale kwa ajili ya watu wengine ambao wanakula bata sasa. Kwa hiyo na sisi haya ambayo yanapita sasa tukubali, kuna maumivu yake kwa sababu ni mambo mapya. Kwa hiyo tukiumia, tukubali kuumia kwa ajili ya vizazi vyetu ambavyo baadaye vitakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Mheshimiwa Rais juzi alivyokuwa ziarani kule mpakani mwa Zambia, alitoa msaada pale, kwa hiyo haya tusishangae, baada ya miaka mitano, kumi ijayo na sisi tutakuwa tunatoa misaada kwenye nchi nyingine badala ya kuendelea kuomba misaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kuliongelea ni kwa mujibu wa Sheria za Usajili wa Makampuni, Na. 12 ya mwaka 2002; Kampuni iliyosajiliwa inatakiwa katika kipindi cha kuanzia mwaka mmoja ifanye marejesho kwa Msajili maana yake BRELA yapo makampuni mengi yanayotaka kulipa marejesho ya Serikali kwa awamu kama ilivyo katika Mamlaka za TRA na Ardhi. Sasa kwa nini Serikali isikubali makampuni hayo yakalipa kwa awamu, kwa sababu ukiangalia kuna utoroshwaji mwingi wa fedha na yanashindwa kulipa, sasa matokeo yake kuna makampuni yanadaiwa mpaka miaka kumi hayajarejesha. Kwa hiyo nafikiri ni vizuri sasa sheria hii ikaangaliwa upya ili wao pia walipe kama vile ambavyo TRA inayatoza makampuni yale kulipa kwa awamu kwa sababu mzigo unapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi kubwa ambayo wanafanya, kama wanavyosema wengine ni kwamba mwanzo tulikuwa hatuwaelewi, tulikuwa tunawachukia sana, lakini sasa hivi tunawapongeza, endeleeni kukaza uzi ili nchi hii iende. Ahsante. (Makofi)