Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja ya Mpango iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi njema anayofanya pamoja na Serikali yake. Kipekee pia namshukuru Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake, tumekuwa tukipambana huko kwenye Kamati ya Bajeti, kwa kweli tunakushukuru wakati mwingine unasikiliza maneno yetu na mapendekezo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu tunaokwenda kuutekeleza au tunaouandaa ni mpango wa mwisho kwenye Mpango wa Miaka Mitano; na mambo yote inayoyazungumza yalitokana na Mpango wa Miaka Mitano, ule wa 2016/2017 – 2020/2021. Mambo mengi tuliyojiwekea kule, sasa tunakwenda kumaliza kuyatekeleza.

Mheshimiwa Spika, napenda niseme mambo mazuri ambayo Serikali imeyafanya, ni pamoja na miundombinu. Kama nilivyosema mwaka 2018, ukitaka kujenga nchi ya viwanda ni lazima uwe na miundombinu. Kwa kweli Serikali imefanya vizuri sana kwenye ujenzi wa reli, barabara, chanzo cha umeme na miundombinu mingine inafanywa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto kidogo ambapo nitatoa ushauri kidogo kama wenzangu walivyosema, kwamba Serikali ichapue kidogo, iongeze speed kidogo katika kutekeleza ujenzi wa miundombinu. Naomba tena na mwaka 2018 nilisema, Mpango huu basi mwangalie, kuna barabara nyingine za kiuchumi kama barabara ile inayotoka Shinyanga, inapita katikati ya Igunga inaelekea Mbeya.

Mheshimiwa Spika, kuna mabasi huwa yanatoka Shinyanga yanaenda Mbeya kupitia katikati ya Igunga. Hii barabara naomba iwekwe kwenye Mpango, nasema tena kwa sababu barabara hii inatoka Ukenyenge, inakuja Igurubi, inapita Mwamakona, inakwenda Igunga, inaenda Rugubu, inaenda Itumba, inenda Loya, inaenda Tura, inaenda kuunganisha na barabara inayotoka kwa wachimbaji madini kule Mbeya na barabara inafika Mbeya. Najua kwa upande wa kule imeletwa mpaka Rungwa. Naomba sasa iunganishwe barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii sasa hivi kuna kipande cha kutoka Igunga kwenda Itumba, kimepewa fedha kidogo, lakini utekelezaji umcheleweshwa. Naomba basi katika Mpango, hii barabara ni ya kiuchumi inapita kwenye pamba, kwenye mpunga na kwenye ufugaji wa ng’ombe. Ni muhimu sana tuharakishe miundombinu ili tuweze kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la miundombinu ya maji. Kama Waheshimiwa Wabunge wengine wanavyosema, maji ni shida kubwa katika nchi yetu. Tunaishukuru sana Serikali kuanzisha ule mradi wa maji wa Ziwa Viktoria na sasa hivi unakwenda Tabora – Igunga
– Nzega. Ahsante sana Serikali kwa kutukumbuka. Igunga ni nchi kame sana, lakini nadhani maji haya yatatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kwenye Mpango huu basi tuongeze fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye zile kata ambazo zimebaki. Sasa hivi tunapata kata kama nane hivi; zinabaki nane kwenye Jimbo la Igunga. Pia kuna Kata nyingine nyingi zinabaki kwenye Jimbo la Manonga ambalo ni Wilaya ya Igunga. Basi tuweke Mpango mwaka 2010 tumalizie kwani wananchi hawa wako kwenye ukame mkubwa, waweze kupata maji. Tutawashukuru sana Serikali mkitukumbuka mkaweka kwenye Mpango jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda ni suala ambalo Serikali ilijiwekea kwenye mpango wa mwaka 2016/ 2017 mpaka 2021. Ilieleza mambo machache mle ndani yakiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati. Miradi mingi ya kimkakati imeshindikana kutekelezwa. Mwaka wa tano leo au mwaka wa nne tunamalizia, mingi bado inasuasua. Naiomba Serikali tena, tuendelee kuiweka kwenye mpango na tutafute fedha ya kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, miradi ya kuendeleza maeneo maalum, kwa mfano, mradi wa kuendelea eneo la Mtwara ambako kuna gesi; tulianza vizuri, lakini kuna mahali tukalega tukaenda pembeni. Kwa hiyo, mradi wa LNG unahangaika, leo mwaka wa tano haujatekelezeka. Naiomba Serikali, hebu malizieni mazungumzo na hawa wawekezaji. Mradi huu ni muhimu, tutapata gesi ya kutumia ndani na pia tutapata gesi ya kupeleka nje tupate fedha za kigeni. Ni jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi hiyo pia tutaweza kujenga kiwanda cha mbolea, ambacho kimetajwa vizuri sana kwenye Mpango, lakini leo mwaka wa nne tunasema tu. Naiomba Serikali, hebu yaangalieni mambo haya, maeneo haya yako mengi, ila Mtwara kwa kweli, hebu tulitazame vizuri, hii gesi itumike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine tumeusema sana kwa muda mrefu, ambao ni mradi wa Mchuchuma, Liganga. Pale kuna chuma cha kutosha kinachoweza kututosha nchi hii kujengea barabara zetu, reli, madaraja na kujenga maghorofa kama tukichimba kile chuma. Kwa miaka mitano sasa hatujaweza kutekeleza. Naomba tena kwenye Mpango isisitizwe na tuweke fedha kidogo huu mradi uweze kutekelezeka. Vinginevyo kwa sababu viwanda vinategemea sana viwanda vya chuma, tutaweza kuwa na chuma cha kuenea kwenye viwanda vingine vyote vya chuma katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililosemwa kwenye Mpango ule wa miaka mitano na Mpango wa mwaka 2018 na wa mwaka huu 2019, limesemwa vizuri, ni jambo la kufundisha wataalam na kuchukua teknolojia, hasa wataalam wa ngazi ya kati. VETA tunafanya vizuri, tunapata mafundi mchundo vizuri sana. Na mimi Wilaya ya Igunga tumeletwa ujenzi wa VETA, tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ngazi za kati, mafundi sanifu, Vyuo vya Mafundi Sanifu vimekuwa vichache na bahati mbaya wakati mwingine Serikali inavigeuza hivi vyuo kuwa Vyuo Vikuu au inaviruhusu vianze kutoa degree.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni Chuo cha Madini Dodoma, kilianzishwa ili kupata mafundi mchundo, nami nilishiriki kukianzisha wakati nikiwa Serikalini, lakini sasa hivi kinalelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Matokeo yake ni kwamba kitakuwa na hamasa na tamaa ya kuwa Chuo Kikuu na kukibadilisha kuwa Chuo Kikuu. Tutakosa mafundi mchundo watakaoshiriki katika ujenzi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali mliangalie jambo hili kwa makini kidogo. Nakumbuka nilihudhuria Kamati ya Madini na Nishati, pamoja na Wabunge wengine wa kamati hiyo, tulisema maneno haya kwamba msiwe na hamu na haja ya kubadilisha hivi vyuo kuwa Vyuo Vikuu, mtachelewesha uanzishwaji na uimarishaji wa viwanda vyetu kwa sababu tutakosa mafundi sanifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kilimo. Ukiangalia kwenye Mpango, tulijiwekea mipango mizuri sana. Kilimo kinaweza kuendeleza viwanda sana kwa sababu malighafi nyingi zinatoka kwenye kilimo. Kwa mfano, pamba; tuna mkakati wa C to C (Cotton to Clothing) ambao unasema tuzalishe pamba kwa wingi, tutengeneze nyuzi hapa hapa na tutengeneze nguo hapa hapa, lakini mpango huo hauendelei kabisa. Hiyo C to C imekuwa document ambayo iko kwenye shelf. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara pamoja na Idara zake na Wizara ya Kilimo kwa umuhimu wake muufufue huu Mpango, pamba itumike kujenga viwanda. Tusifikirie tu kuuza pamba nje. Tunapata taabu sasa hivi hatujalipa wakulima wetu, lakini tungekuwa na viwanda hapa hili tatizo la pamba, tatizo la bei lisingekuwa shida kubwa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la mifugo kwa mfano na lenyewe kwa kuwa tuna mifugo mingi, tunaweza kuwa na viatu hapa hapa, lakini hatutazami. Mpango huu uyatazame mambo haya tena ya kujenga viwanda kwa kutumia malighafi katika nchi yetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Malizia Mheshimiwa.

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niseme tena kwamba, Mpango umalizie yale mambo ambayo umeyaacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)