Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuweza kuwa mchangiaji wa mwisho katika hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango. Napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli naipongeza sana Awamu ya Tano kwa maana ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mipango pamoja na Mawaziri wenzake kwa kazi nzuri ambayo wanaitendea haki Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulipoenda kwenye uchaguzi mwaka 2015 tulikuwa tunawaahidi wananchi maendeleo. Kusema kweli, mimi binafsi Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, nikizungumzia katika Jimbo langu la Musoma, ingekuwa leo ndiyo tunaenda kwenye uchaguzi hasa tukiwa tunazingatia yale tuliyoyaahidi, basi naweza nikasema utekelezaji umefanyika kwa zaidi ya asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni ukweli usiopingika, hata unaposafiri barabarani utakutana na magari mengi ya nguzo kwa maana ya nguzo ya umeme, mabomba ya maji, lakini hayo yote ni mambo ambayo yanafanyika katika lengo zima la kuhudumia wananchi. Ndiyo maana hata ndugu yetu Mheshimiwa Bwege pale, yeye mwenyewe ameshukuru na ameweza kusema wazi kwamba mambo ambayo yamefanyika katika awamu hii ni mambo ambayo ni ya wazi wazi kwa maana ya mambo ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wasiwasi wangu ni mmoja tu ambapo katika Mpango huu wa leo sijaona kama tumeuzungumza sana. Pamoja na juhudi hizi kubwa za maendeleo tunazofanya, lakini bado mahitaji hata tungepeleka maji, hata tungetengeneza barabara pamoja na elimu, lakini mahitaji mwaka baada ya mwaka yapo pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mifano michache. Pale kwenye Jimbo langu la Musoma, ile mwaka 2005 tulijitahidi sana kujenga sekondari karibu kila Kata, lakini ndani ya muda mfupi tu, leo kuna Kata ambazo zina sekondari zaidi ya tatu. Hapo ni kwamba mahitaji ya sekondari bado yako pale pale. Ukienda kwenye Shule za Msingi, leo unakuta kwa sababu ya ufinyu wa maeneo ya kujenga, pale pale tumezibananisha, ilikuwa ni shule moja, sasa ziko shule mpaka nne. Kwa hiyo mahitaji haya, mashaka yangu ni kwamba inaonekana hayatakaa yapungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, sijui labda hili watu wengi tunaogopa kulisema, maana nimejaribu kuangalia hata katika nchi za wenzetu zinazoendelea, suala la uzazi wa mpango; ni kwamba kwa namna ambavyo Watanzania tunaongezeka siku kwa siku, katika mtazamo wangu ni kwamba pamoja na juhudi zote ambazo tutazifanya, lakini bado mahitaji yataendelea kubaki pale pale. Kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba, hata kama tunadhani kama hatulioni; nitoe mfano kwetu sisi watu wa Mara ambao tunaruhusiwa kuoa wanawake mpaka watano, maana yake ni kwamba familia zetu zinaendelea kupanuka siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ninyi Wasukuma, upanuzi wa familia unaendelea siku hadi siku. Sasa hayo yote ukiyaangalia, kama hatuwezi ku- address suala la uzazi wa mpango ni tatizo ambalo ninaamini kwamba pamoja na juhudi za awamu hii, lakini mahitaji bado yataendelea kubaki kama yalivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia wale wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba, maana kwa namna ninavyoliona ni tatizo la ajira. Wanafunzi wanamaliza Darasa la Saba, zaidi ya asilimia 50 wanaingia mtaani. Wanafunzi wanamaliza Kidato cha Nne, zaidi ya asilimia 70 wanaingia mtaani; wanafunzi wanamaliza mpaka Vyuo Vikuu, zaidi ya asilimia 80 hakuna kazi. Hii yote, katika mtazamo wangu ni kwamba wanafunzi wote hawa wanakosa ajira kwa sababu hawana skills. Yaani asilimia kubwa ya wanafunzi hawana mafunzo yoyote yanayoweza kuwawezesha hata kujiajiri. Hali hii ni hali ambayo inaendelea. Sasa nini kifanyike katika huu Mpango wa muda mfupi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali awamu hii, ilianzisha mpango wa kuchukua wanafunzi wengi au vijana wengi kwenda JKT. Kusema kweli wale vijana wamekaa kule miaka mitatu na wamejifunza mafunzo mbalimbali; mafunzo ya ukakamavu na badhi ya mafunzo mengine labda ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika mtazamo wangu, Serikali inapaswa iongeze nguvu zaidi. Nini kifanyike? Moja, wale vijana wanaoenda JKT, kwanza waendelee kuchukuliwa wengi zaidi, nami nakubali kwamba wakae miaka mitatu. Pia katika kipindi cha miaka mitatu hiyo wajifunze mafunzo mbalimbali; ujasiriamali, mifugo na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kila mwezi tuwe na utaratibu kama tunawalipa mshahara, lakini fedha hizo tunaziweka kule. Hata kama tungekuwa tunawawekea shilingi 200,000/=, baada ya miaka mitatu, yule kijana atakuwa na pesa zisizopungua shilingi milioni saba. Sasa ile siku tunapomwambia sasa kijana umemaliza miaka mitatu JKT, hebu nenda kaendelee na maisha, tafsiri yake ni kwamba akiondoka pale na shilingi milioni saba na huku ameshajifunza mafunzo mbalimbali, lazima atapata mahali pa kuanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, baada ya miaka mitatu tunawaambia, tunawachukua wachache Jeshini, wachache Polisi, halafu wengine tunawaambia wakaanze maisha. Kwa kweli tunawapa ugumu wa maisha. Hii sioni kama inawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akaliangalia na hilo aliweke katika Mpango tuone namna ya kuchukua vijana wengi zaidi kwenda JKT wakajifunze, lakini mwisho wa siku waondoke na chochote, waondoke na ujuzi ili wakaanze maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naona na lenyewe tunahitaji kuliweka katika Mpango, tunajitahidi sana kuwasomesha vijana mpaka kwenye elimu ya juu. Tunapowapeleka mpaka kwenye elimu ya juu, kuna baadhi ya degree ambazo vijana wakitoka nazo kule ukimleta kwenye maisha ya kawaida anazidiwa na kijana ambaye ametoza VETA au mwenye Diploma ya Mifugo. Hii yote ni kwa sababu kuna baadhi ya degree ambazo kama hakupata ajira ya Serikali, hawezi kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kama ambavyo tumejitahidi sana kujenga shule za sekondari, kama ambavyo tumejitahidi sana kujenga Vyuo Vikuu, hebu tuwe na mikakati mahsusi ya kujenga hivi vyuo katika maeneo yetu. Mfano Vyuo vya Mifugo, Vyuo vya Kilimo, Vyuo vya VETA na Vyuo vya Ufundi Uchundo. Tunadhani kwamba hawa vijana wanaomaliza Darasa la Saba, wanaomaliza Kidato cha Nne, wakiondoka na huo ujuzi, basi unaweza ukawasaida zaidi kwenda kuanzisha maisha kuliko katika hali ya sasa ambayo wanaendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ndiyo maana vijana wetu wengi leo wakishamaliza hizi elimu mbalimbali, unawakuta tu wako Mitaani wala hawajui wafanye nini. Ndiyo maana sasa kila ukiwauliza kila kijana anazungumza hali ya maisha ni ngumu kwa sababu anashindwa namna gani anavyoweza kuendesha maisha yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu mwingine ambao Mheshimiwa Dkt. Mipango aendelee kuuweka katika mipango ni huu utaratibu wa uendelezaji wa bandari. Bahati nzuri tumeendeleza Bandari kama ya Dar es Salaam, ya Mtwara na Tanga. Ziko bandari ambazo leo zimesinzia. Ukienda kama kule Kanda ya Ziwa, pale Musoma bandari imelala; ukienda Mwanza bandari zimelala na ukienda Bukoba bandari zimelala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa najaribu kuangalia Serikali ilipoanzisha utaratibu wa bulk procurement, huu wa ununuzi wa mafuta kwa pamoja. Katika utaratibu wake wa kudhibiti nadhani kama magendo na vitu kama hivyo na kuwa na mafuta bora; ilichokifanya, ilianzisha kwenye eneo moja tu la Dar es Salaam. Ikafika mahali ikafanya vizuri, Serikali eneo la Tanga ikafika mahali wakafanya vizuri na Serikali imepeleka Mtwara, imefika mahali wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia kule Kanda ya Ziwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Ulikuwa na hoja nzuri sana, muda ndio huo.

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)