Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo Mwaka 2020/ 2021. Awali ya yote nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu, mpendwa wetu Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kulifanyia Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, yeye pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na timu nzima ya pale Wizarani kwa kazi kubwa wanayoifanya, kazi kubwa waliyoifanya katika kutuandalia mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni muendelezo wa Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ulioanza mwaka 2016/2017 unakuja kuishia katika mpango huu tunaojadili leo 2020/2021. Mpango huu unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, chama ambacho ndio chama tawala; ilani ya uchaguzi imeeleza inataka kuwafanyia nini Watanzania, kubwa inalotaka kuwafanyia Watanzania ni kuwavusha Watanzania kutoka kwenye hatua tuliyonayo sasa na kutupeleka kwenye nchi ya uchumi wa kati, inataka kutuvusha kupitia viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii imepangiliwa vizuri sana na Wizara husika, kwamba, ili tuweze kufika huko, ili viwanda vyetu viweze kusaidia kuivusha nchi hii kutoka hapa kwenda kwenye uchumi wa kati ni lazima mambo fulani fulani yawekwe sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu uko vizuri kabisa, umejipanga vizuri kabisa kwamba tunahitaji tuwe na umeme wa kutosha, tuwe na umeme wa bei rahisi ili tuweze kuzalisha bidhaa zenye bei ambazo zina ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali tuliyonayo sasa, tunazalisha mazao mengi; tunazalisha pamba na tunasafirisha pamba ghafi, lakini tunaweza tukasafirisha pamba ambayo imekuwa semi processed kwa kiasi fulani. Shida kubwa inakuwa wapi? Gharama ya uzalishaji inakuwa juu. Unakuta mtu anaona akinunua pamba ghafi akaenda kui-process mwenyewe, gharama ya ku-process kwake inakuwa ni ndogo. Kwa hiyo, anaona bora anunue pamba ghafi. Tukisema tui-process kidogo kuiongeza thamani, gharama inakwenda juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imeliona hili ikasema hapana, lazima tuwe na mkakati wa kuzalisha umeme wa kutosha na wa bei rahisi. Ndiyo ikaja na mpango mzima wa Stiegler’s Gorge. Uzalishaji wa umeme wa megawat 2,115 ni umeme mwingi sana utakaosaidia kushusha gharama ya umeme na kuhakikisha viwanda vinapata umeme na kufanya kazi ya uzalishaji kuwa rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaenda sambamba na mpango wa Serikali vilevile kuhakikisha kwamba wananchi wanapata umeme kote nchini. Mpango wa mwaka 2021 nchi nzima, vijiji vyote, vitongoji vyote wananchi wote wawe wamepata umeme ni mpango unaoenda sambamba na ujenzi wa Stieglers Gorge ili umeme uwepo wa kutosha tusije tukajikuta tumesambaza umeme kwa maana ya nguzo na waya kufika kila sehemu lakini tunafika mahali fulani, umeme wa kuwapa wananchi unakuwa haupo. Kwa hiyo, naupongeza sana mpango huu, ni mpango uliokaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la usafirishaji, kusafirisha malighafi kutoka sehemu moja hadi nyingine, kusafirisha end products, yaani mazao tunayozalisha katika viwanda vyetu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine pia ni kitu cha muhimu sana ambacho Serikali yetu imeliona na imelifanyia kazi nzuri sana. Tunaona barabara zetu nyingi sana zimewekwa lami sasa. Nchi yetu sasa hivi imeunganishwa kwa sehemu kubwa sana, jambo ambalo linafanya usafiri unakuwa rahisi, mtu anatoka hapa asubuhi anajikuta jioni yuko Mwanza. Ni jambo lilikuwa siyo rahisi sana, unafikiria kwenda siku mbili tatu ukiwa barabarani, lakini mtu anatoka hapa kwenda Songea, kwenda Njombe, kwenda Mbamba Bay huko kwa muda mfupi sana. Tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, katika suala la usafirishaji wa bidhaa, usafirishaji wa mizigo mbalimbali tukaona kwamba reli ya kati ifanyiwe uboreshaji. Tukaja na wazo la SGR ambapo sasa tunaipongeza Serikali. Kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kimeshafika asilimia 63, ni jambo la kuipongeza sana. Kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora hapa Dodoma, nacho kimefikia asilimia 16. Tunaipongeza sana Serikali kwa hilo. Mipango yote hii inaonyesha jinsi gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inakwenda na ratiba yake iliyojiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la afya. Tukienda kwenye kitabu cha mwongozo wa Mpango ukurasa wa 17 kipengele cha 58, imeongelewa kwa uzuri kabisa na kwa kina, lakini mimi niseme kitu kimoja; afya ndiyo kila kitu. Tunahitaji wananchi wetu wafanye kazi ili waweze kuzalisha mashambani. Tunahitaji watu wetu wawe na afya bora ili waweze kufanya kazi viwandani. Kwa hiyo, suala la afya ni suala la muhimu sana, naipongeza Serikali. Hadi sasa tunazungumzia Vituo vya Afya zaidi ya 352. Hadi sasa tunazungumzia Hospitali za Wilaya 67 tumekwenda hatua kubwa sana. Naipongeza sana Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maboma. Wananchi wetu wamejitoa, wamefanya kazi kubwa sana huko vijijini. Wamejenga majengo ambayo wameshindwa kuyamalizia. Wanaweza kutoa nguvu zao wakasaidia kujenga, lakini inafika mahali fulani wanashindwa kumalizia. Naiomba sana Serikali, hebu iangalie, hakuna Halmashauri ambayo haipendi kukamilisha haya maboma, lakini Halmashauri hazifanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, hebu aliangalie hili kwa kina, Halmashauri ambazo hali yake siyo nzuri sana kimapato, zipewe support ya kumalizia haya maboma. Tunawavunja nguvu sana wananchi katika kazi ya kujitolea na kujenga maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu liko hivyo hivyo, nalo lina maboma ambayo ningependa kabisa nayo yafanyiwe kazi katika mpango huo niliosema hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji haliko mbali na hivyo nilivyosema. Suala la maji kwa ujumla wake limetekelezwa kwa asilimia 82.6. Naipongeza sana Serikali. Pamoja na kwamba bado maeneo mengine, suala la maji safi na salama ni tatizo, lakini Serikali imefanya kazi kubwa sana, naipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, ukienda kwenye kitabu cha Mwongozo kile ukurasa wa sita jedwali 1.2 linaonyesha uuzaji wetu nchi za nje ulishuka kwa asilimia 4.2, lakini ununuzi wetu wa bidhaa kutoka nje ulipanda kwa asilimia 8.9. Hii maana yake ni kwamba tumeshindwa kusafirisha bidhaa kwenda nje. Nami mtazamo wangu ni kilimo. Kilimo kisiposimamiwa vizuri kikatuletea bidhaa za kutosha kusafirisha nje, basi hali hii itaendelea kujitokeza mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, kuna suala zima la mabwawa ya umwagiliaji sehemu mbalimbali, hebu Serikali ije na majibu yanayoeleweka. Kuna mabwawa ya zamani, tumeshazungumza sana humu Bungeni suala la ukarabati wa mabwawa ya zamani. Serikali imekuja na mipango mingi sana kwamba watayaangalia waone ni namna gani wa kuyaboresha haya masuala. Basi iwe na kauli ya kusema ili huko kwa wananchi tujue nini cha kufanya. Mabwawa hayatengenezwi, maji hayapatikani, umwagiliaji umeshuka chini na suala zima la uzalishaji wa kilimo unashuka chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwanza kabisa kwa kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pili nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kumkaribisha Mheshimiwa Rais kwa mikono miwili hapa Dodoma. Juzi alikuja kujiandikisha pale Chamwino kwamba sasa yeye ni mkazi wa Chamwino rasmi. Katika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Makanyaga kwa mchango wako mzuri na ushauri.

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.